RC Dendego: Msiende kuwa viongozi wa ofisini

Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Selekwa akiapishwa

Muktasari:

  • Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amemwapisha Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa huku akiwaasa wakuu wa wilaya kushuka chini kwa wananchi badala ya kuwa viongozi wa ofisini.

Iringa. Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego amemuapisha Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Dk Linda Salekwa huku akiwaagiza wakuu wote wa wilaya kusimamia miradi mbalimbali ikiwemo elimu kwa kuhakikisha kila mwanafunzi anayetakiwa kuwa darasani anaingia.

 Pia amewataka wakuu hao kufanya ziara za kukagua miradi ya maendeleo vijijini na kuwahakikishia wananchi maendeleo badala ya kuwa viongozi wa ofisini.

Akizungumza wakati akimuapisha Dk Salekwa, Dendego amesema katika ndani ya siku saba zijazo kila mwanafunzi ambaye anatakiwa kuingia darasani anapaswa kuwa ameshaingia.

“Nendeni mkahakikishe watoto wote wanakwenda shuleni, msiwe na huruma katika hilo bali shukeni chini kwa wananchi.

“Wakazi wa Iringa ni wapole, wakarimu na wachapa kazi, nendeni mkafanye kazi,” amesema Dendego.

Aliwataka wakuu hao wa wilaya kuwa na uongozi wa kimkakati sambamba na kuhakikisha wanatenda haki bila kumuonea huruma mtu ambaye kwa maksudi anavunjasheria.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Veronica Kessy aliwakumbusha viongozi kufanya kazi kwa umoja, upendo na ushirikiano.

Alisema umoja huo utasaidia kuleta katika kuwaletea wananchi maendeleo ya kweli.