Precision air watoa shukrani Bukoba

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Patrick Mwanri amesema, wanatoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na wakazi wa Bukoba kwa kuwasaidia wakati wa ajali ya ndege yao aina ya PW 494 iliyotokea Novemba 6, 2022.

Dar es Salaam. Shirika la ndege la Precision Air, limetoa msaada wa chakula na mahitaji mengine muhimu kwa vituo vitano vilivyomo Bukoba mkoani Kagera pamoja na mchango kwa vikundi vya wavuvi vilivyopo kando ya ziwa Victoria.

Akizingumza wakati wa kukabidhi msaada huo pamoja na mchango leo Februari 3, Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Patrick Mwanri amesema, wanatoa shukrani kwa Mwenyezi Mungu pamoja na wakazi wa Bukoba kwa kuwasaidia wakati wa ajali ya ndege yao aina ya PW 494 iliyotokea Novemba 6, 2022.

Ajali hiyo iliyotokana na hali mbaya ya hewa ilisababisha vifo vya watu 19 waliokuwemo kwenye ndege hiyo, huku wengine 26 wakiokolewa.

 “Hatuna budi kusema asante kwa namna Mwenyezi Mungu ameendelea kutupatia nguvu na ujasiri kwa wakati wote, na kidogo hiki tunachotoa kinabeba shukrani zetu za dhati,” amesema.

Ameongeza kuwa pia ushujaa ulionyeshwa na wavuvi waliojua karibu na eneo la tukio hauwezi kulipwa kwa thamani yeyote ila amewaomba wapokee mchango huo kidogo kama ishara ya kitambua juhudi zao.

Shirika hilo limetoa msaada wenye thamani ya Sh10 milioni na mchango kwa vikundi vya wavuvi wa Sh10 milioni.

Akizungumzia msaada huo, Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Erasto Sima amewapongeza Precision Air kwa kufanya jambo la kiungwana nakuwataka kuendelea na moyo huo wa kuwakumbuka wenye mahitaji.

Pia amewatoa hofu wananchi na kuwataka kuendelea kusafiri na Precision Air kwa usafiri huo ni salama na kwamba ajali iliyotokea inaweza kutokea kwa shirika lolote duniani.