Mutafungwa aonya upandishaji bei stika vyombo vya moto

Kamanda wa Polisi mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa akizungumzia tukio la mwanamke kummwagia mpenzi wake maji ya moto baada ya kumtuhumu kuwa katika mahusiano ya kimapenzi na wanawake wengine. Picha na Mgongo Kaitira

Muktasari:

  • Kamati ya Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza imekasimiwa jukumu la kuadhimisha wiki ya 'Nenda kwa Usalama Barabarani' kitaifa, ambapo elimu ya usalama barabarani itatolewa kwa abiria na madereva huku vyombo hivyo viwekewa stika maalum baada ya kukaguliwa.

Mwanza. Mwenyekiti wa Kamati ya Usalama wa Barabarani Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa amewaonya maofisa wa polisi na wakaguzi watakaopandisha bei za stika za usalama barabarani kiholela, huku akiwataka wamiliki wa vyombo hivyo kulipia gharama iliyoelekezwa.

Mutafungwa ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza ametoa onyo hilo kwenye uzinduzi wa wiki ya 'Nenda kwa Usalama Barabarani' uliofanyika kitaifa katika viwanja vya Nanenane wilayani Ilemela mkoani Mwanza.

Ametaja bei elekezi ya stika hizo zinazopachikwa kwenye vyombo vya moto ambavyo vimekaguliwa kuwa ni Sh7,000 kwa magari makubwa yakiwemo ya abiria, magari binafsi (Sh5,000) na pikipiki zikiwemo bajaji za matairi matatu (Sh2,000).

“Kati ya mambo yanayochangia ajali ni tabia na hulka za kibinadamu kama ulevi na kuendesha chombo cha moto, pia kukubali vyombo vibovu kutembelea barabarani.

"Stika kama gharama ambayo imetolewa na baraza (RSA) naomba mzingatie hela elekezi ya kwenye hiyo stika na si kinyume cha hapo. Na stika itolewe baada ya kupata elimu na chombo kufanyiwa ukaguzi," amesema Mutafungwa.

Kwa upande wake, Mkuu wa Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim ametaja maeneo ya ukaguzi mkoani Mwanza kuwa ni viwanja vya Nanenane wilayani Ilemela, Stendi za mabasi yaendayo mikoani, stendi za mabasi yanayotoa huduma usafiri ndani ya mkoa huo na katika vituo vya Polisi mkoani hapa.

"Mkoa wetu umeteuliwa kuadhimisha wiki hii kitaifa naomba vyombo vya moto viletwe kwa wingi katika maeneo ambayo yameainishwa kwa ajili ya kukaguliwa.

“Maofisa wetu wana ari ya kutosha kutekeleza hilo ili mwisho wa siku kauli mbiu ya 'Tanzania bila ajali inawezekana' itekelezwe kwa vitendo," amesema Ibrahim ambaye ni Katibu wa Kamati hiyo mkoa wa Mwanza.

Naye, dereva wa lori la kubeba mchanga, Moses Andrew akizungumza baada ya gari yake kukaguliwa na kuwekewa stika amesema ukaguzi huo utasaidia kubaini vyombo vya moto vilivyochakaa na kuyachukulia hatua ikiwemo kuviondoa katika utoaji wa huduma ya usafirishaji ili kuepusha ajali.

"Madereva tutii maagizo na sheria za usalama barabarani ikiwemo kupeleka vyombo vyetu kukaguliwa. Hili ni jambo la busara magari yasipokaguliwa tunakuwa tunaendesha bila kujiamini kwani huwezi kujua status ya chombo cha mwenzako kwenye barabara," amesema