Migongano ya binadamu na wanyamapori yazidi kuongezeka, suluhisho latajwa

Muktasari:

  • Mambo yanayotajwa kusababisha migongano kati ya binadamu na wanyamapori ni pamoja na watu kujenga makazi kwenye shoroba za wanyamapori, kukosekana kwa mpango bora ya matumizi ya ardhi, mifugo kuingia kwenye hifadhi, mabadiliko ya tabianchi na kupuuzwa kwa ushauri wa wataalamu.

Bagamoyo. Matukio ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu yamekuwa yakiongezeka mwaka hadi mwaka kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo watu kujenga makazi kwenye shoroba za wanyamapori.

Mwingiliano huo umekuwa ukisababisha athari kwa binadamu na wanyamapori ikiwemo kuharibiwa kwa mazao, watu kujeruhiwa, kuuawa na wanyama hao na pia kubadilika kwa tabia za wanyamapori.

Hayo yamebainishwa na Ofisa Uhifadhi kutoka Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori (Tawa) anayesimamia udhibiti wa wanyama wakali na waharibifu, Isaack Chamba wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu migongano kati ya binadamu na wanyamapori.

Mafunzo hayo yaliaandaliwa na  Chama Cha Waandishi wa Habari za mazingira Tanzania (JET) kwa ufadhili wa Mradi wa Kupunguza Migogoro Baina ya Binadamu na Wanyamapori Tanzania, unaotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) kwa niaba ya Serikali ya Ujerumani (BMZ).

Chama amesema migongano kati ya binadamu na wanyamapori ni ya kihistoria na ilikuwa ikishughulikiwa na Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii na baada ya kuanzishwa kwa Tawa, ikabeba jukumu hilo.

Amesema takwimu za Tawa zinaonyesha kwamba mwaka 2016/17 kulikuwa na matukio 833 ambapo mwaka 2017/18 yaliongezeka hadi kufikia 997 na mwaka uliofuata wa 2028/19 yaliongezeka zaidi hadi kufikia 1510.

Mwaka 2019/20, matukio ya wanyama kuingia kwenye makazi ya watu yalipungua kidogo hadi kufikia 1426, mwaka 2020/21 yalifika 1706 na mwaka 2021/22 yalikuwa 2304 na mwaka 2022/23 yalikuwa 2817.

Ofisa huyo amesema ongezeko wa matukio hayo ni sawa na wastani wa asilimia 23.76 kwa mwaka wakati uharibifu wa mazao pia ukiwa ni ongezeko la wastani wa asilimia 118.1 kwa mwaka.

“Mwaka 2018 kulikuwa na ongezeko kubwa la matukio ya migongano. Ongezeko hilo liliisukuma Wizara ya Maliasili na Utalii kuandaa Mkakati wa Taifa wa Kusimamia Migongano kati ya Binadamu na Wanyamapori (2020 - 2024).

“Mkakati huo ulizinduliwa Oktoba 5, 2020 na unatekelezwa na Tawa, Tanapa (Mamlaka ya Hifadhi za Taifa), NCAA (Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro), TFS (Wakala wa Misitu Tanzania), Tawiri (Mamlaka ya Utafiti wa Wanyamapori) na wadau wengine,” amesema Chamba.

Chamba amesema hadi sasa wilaya 44 zinakabiliwa na changamoto ya wanyamapori kuingia kwenye makazi ya watu na kusababisha uharibifu wa mazao, mali, kujeruhi na hata kusababisha vifo kwa binadamu au wanyama wenyewe kuuawa na wananchi.

Amebainisha baadhi ya wilaya hizo kuwa ni Busega, Kilosa, Meatu, Nachingwea, Rufiji, Lindi, Manyoni, Itilima, Tunduru na Bunda.

“Mnyama anayeongoza kwenye matukio haya ni tembo, asilimia 80 ya matukio hayo alihusika. Asilimia 20 iliyobaki ni wanyama wengine kama simba, fisi na nyani,” amesema Chamba akifafanua takwimu hizo.

Amebainisha mambo yanayosababisha migongano hiyo kuwa ni pamoja na watu kujenga makazi kwenye shoroba za wanyamapori, kukosekana kwa mpango bora ya matumizi ya ardhi, mifugo kuingia kwenye hifadhi, mabadiliko ya tabianchi na kupuuzwa kwa ushauri wa wataalamu.

Mhifadhi huyo ameeleza kwamba inapotokea wanyama wameingia kwenye makazi ya watu, wananchi wana jukumu la kuwataarifu Tawa na siyo kuwaua, kwani kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Amesema Tawa huwaswaga wanyama hao kuwarudisha hifadhini na walioshindikana  huuawa ili wasilete madhara zaidi.

“Mwaka 2017/18 hadi 2022/23, simba 60 na fisi wawili walihamishwa kutoka kwenye makazi ya watu na kurudishwa kwenye hifadhi. Mwaka 2022, tuliwarudisha tembo 270 kutoka kwenye jamii na kuwarudisha hifadhini Liwale na Nachingwea,” amesema.

Kwa upande wake, mtaalamu wa migongano kati ya binadamu na wanyamapori, John Noronha amesema licha ya kwamba kumekuwa na migongano hiyo, kuna umuhimu wa pande hizo mbili kuishi pamoja katika mazingira yao.

Amesema inawezekana binadamu akaishi na wanyamapori pindi wanapoingia kwenye makazi yao na wasisababishe madhara, hiyo ni pamoja na kutumia njia za kujikinga kama vile kujenga uzio imara, kulima mazao yasiyoliwa na tembo, kupanda pilipili au kufuga nyuki.

“Hata hivyo, ifahamike kwamba njia hizo zinaweza kufanya kazi sehemu moja lakini sehemu nyingine zisifanye, kwa hiyo ni muhimu kujua mazingira husika yanafaa kutumia njia gani za kudhibiti uharibifu unaofanywa na wanyamapori,” amesema.

Mtaalamu huyo amesisitiza kwamba ni muhimu pia jamii ikabadilisha fikra zao kuhusu wanyamapori kwa kuwaona ni wavamizi wa makazi yao, kumbe wanapita kwenye njia zao za asili na binadamu ndiyo waliovamia maeneo yao.

Serikali na fidia

Akiwa wilayani Same, mkoani Kilimanjaro hivi karibuni, Waziri wa Maliasili na Utalii, Angellah Kairuki alisema Serikali iko kwenye mchakato wa kutangaza  viwango vipya vya vifuta jasho kwa wananchi walioathirika na maafa ya wanyamapori nchini.

Alisema zaidi ya Sh7.1 bilioni zimeshatolewa kama vifuta jasho.

“Tumeshawasilisha Wizara ya Fedha kiwango cha fidia tulichopendekeza kama Serikali itaridhia  muda siyo mrefu tutatangaza kiwango hicho kipya.”

Wananchi katika maeneo yaliyo jirani na hifadhi wamekuwa wakilalamika kulipwa fidia ndogo ambayo haiendani na uharibifu wanaopata au kupoteza wapendwa wao,  pia kwamba fidia hiyo haitolewi kwa wakati.

Kupitia sheria iliyotolewa na Serikali  kwa mujibu wa kanuni za kifuta jasho na machozi ya mwaka 2011 ni kwamba mtu aliyeuawa na mnyamapori anapaswa kulipwa fidia ya Sh1 milioni   na aliyejeruhiwa ni Sh500,000.

Waziri Kairuki aliwahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kuwa malalamiko hayo ameyachukua kwa uzito wake na atayafanyia kazi ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa elimu kwa wananchi na kuhakikisha changamoto hiyo inatatuliwa kwa njia mbalimbali.

“Niwaombe na niwape pole  ndugu zangu wa Same niwahakikishie tumelipokea kwa uzito mkubwa, tumeshaanza kujenga baadhi ya mabwawa hifadhi ya Mkomazi na tutaendelea kufanya hivyo katika maeneo mengine ili wasilazimike kutoka nje ya hifadhi  kufuata maji, kwa sababu wakitoka nje kufuata maji watakutana na wananchi wetu na mazao ya wakulima.

“Kama Serikali hatufurahii kuona tembo hao wanakuja kumjeruhi mtu yeyote au kupoteza maisha ya wananchi wetu, tunachokifanya hivi sasa chini ya maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan, tunaangalia kiini au chanzo kinachofanya tembo watokea hifadhini na kuingia kwenye makazi ya watu ni nini,” alisema Kairuki.