Mbunge ataka ulinzi watoto wa kiume

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maaalum, Dk. Dorothy Gwajima akitolea ufafanuzi na kujibu maswali ya wabunge Dodoma jana

Muktasari:

  • Mbunge wa Iramba Mashariki, Isaack Mtinga amesema utafika wakati Tanzania itaanza kuwatafuta wanaume kwani dunia haiwezi kukamilika bila kuwa na mwanaume.

Dodoma. Wakati wabunge wakivutana kuhusu suala la kuwalinda vijana na watoto wa kiume katika maadili, Mbunge wa Iramba Mashariki, Isaack Mtinga (CCM) amesema bila umakini Taifa litakuwa na kibarua cha kutafuta wanaume rijali kwa siku za usoni.

 Mtinga amesema Serikali imewekeza zaidi nguvu kubwa kwa kuwalinda watoto wa kike, huku wanaume hakuna anayejali na hata wazazi wanaporudi majumbani huwauliza watoto wa kike lakini wakiume hawafuatiliwi muda wa kurudi nyumbani.

Akichangia hoja katika Taarifa ya Kamati ya Huduma za Maendeleo ya Jamii jana Februari 2, 2023, Mtinga amesema kwa sasa watoto wa kiume wamesahaulika na kuachwa kama kuku wa kienyeji jambo ambalo ni hatari kwa siku za usoni.

“Wabunge wanawake mnatakiwa kuvaa uhalisilia huu, jiwekeni kwenye sura ya uzazi lakini bila kufanya hivyo, tutambue kuwa tunatengeneza bomu kwa siku za usoni,” alisema Mtinga.

Mtinga amesema dunia haiwezi kukamilika bila kuwa na wanaume na kwa hiyo vijana wa kiume siku za mbeleni wengi watakuwa wameshughulikiwa akahoji wanaume watapatikana wapi.

Akimpa taarifa mbunge huyo, Mbunge wa Viti Maalumu, Ester Matiko alisema hakuna ubaya kwa Serikali kuendelea kuwasaidia watoto wa kike kwani walishasahaulika siku nyingi.

“Nataka kumpa taarifa mheshimiwa mbunge kuwa, aangalie hata humu ndani ataona idadi ya wabunge wanawake ni wachache ukilinganisha na wanaume lakini hata baraza la Mawaziri idadi hailingani kwa hiyo aache kusema watoto wa kike wanapendelewa kuliko wanaume,” alisema Matiko.

Spika wa bunge Dk Tulia Akson aliingilia katika kwenye mjadala huo na kumuuliza maswali Mtinga “je ukiwa na mtoto wa kike na kiume yupi utamlipia ada ya shule”. Mtinga alijibu; “wote.”

Dk Tulia alihoji pia, ikiwa ndiyo, je enzi za wazee wenye umri wa mzazi wa Mtinga wangefanyaje? Ndipo akasema ni wakati kwa mtoto wa kike kuendelea kuangaliwa zaidi wakati huu kuliko kipindi kingine.

Akichangia wakati wa kuhitimisha hoja hiyo, Waziri wa Maendeleo ya Wanawake, Jinsia na Makundi Maalumu Dk Doroth Gwajima alisema serikali haijawatenga watoto wa kiume lakini inachofanya ni kuwa karibu na watoto wa kike ili nao kuwapa nafasi.

Hata hivyo, Dk Gwajima alikiri kuwepo na changamoto ya watoto wa kiume kwa sasa ambapo na ulinzi kwa watoto wote uangaliwe pamoja na kuwasikiliza watoto na kucheza nao kwa upendo.