Kamanda wa Polisi apigwa butwaa wanawake kukutwa na nyama pori

Jeshi la Polisi wilayani Kiteto mkoani Manyara linawashikilia wanawake wawili kwa kukutwa na nyara za Serikali akiwemo digidigi aliye hai. Picha na Mohamed Hamad Kiteto

Muktasari:

  • Walikutwa na mnyama aina ya Mbawala wa thamani ya Sh1.4 mil na mnyama aina ya digidigi akiwa hai wa thamani ya Sh583,000.

Kiteto. Jeshi la Polisi wilayani Kiteto Mkoani Manyara, linawashikilia wanawake wawili wa eneo la Njutaa Kijiji cha Kimana wilayani Kiteto mkoani Manyara, kwa tuhuma za kukutwa na nyara za Serikali.

 Watuhumiwa hao walikamatwa na nyama aina ya mbawala (Pongo) na mnyama ana ya digidigi aliye hai wakiwa eneo la Njutaa Kijiji cha Kimana Kata ya Partimbo Kiteto.

Akizungumzia sakata hilo Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Manyara leo Machi 22, 2023, RPC George Katabazi amethibitisha tukio hilo na kuwataja watuhumiwa hao kuwa ni Veronica Paulo Mnubi (24) na Witness Paulo Mnubi (20) wote wakazi wa eneo la Njutaa Kijiji cha Kimana.

"Nyara hizi za Serikali ni nyama pori aina ya  Mbawala (Pongo) ambayo imekadiriwa kuwa na thamani ya Sh1.4 mil, lakini pia walikutwa na mnyama pori hai aina ya digidigi wa thamani ya Sh583,750," amesema Kamanda Katabazi.

Amesema watuhumiwa walikutwa na nyara hizo za Serikali kinyume cha sheria wakiwa ndani ya nyumba yao hapo kijijini usiku Machi 20, 2023 wakati polisi wakiwa kwenye doria ambapo walipata tarifa kwa wasamaria wema juu ya tukio hilo.

Tukio hilo limeibua gumzo kwa wananchi Kiteto kukamatwa kwa wanawake na nyara hizo ili hali imezoeleka kuwa wanaokutwa nazo ni wanaume.

RPC Katabazi alisema uhalifu wa sasa hauangalii jinsi ya mtu badala yake matukio hayo sasa yamekuwa yakifanywa na makundi yote na kuwataka wananchi kuacha tabia hiyo mara moja kwani ni kinyume cha sheria.

"Wanaume na wanawake wanaweza kujihusisha na uhalifu kwa hiyo tafsiri ya uhalifu huu unaweza kufanywa na mtu yeyote bila kuangalia jinsi yake," amesema Kamanda Katabazi.

"Alisema kitendo hiki cha wanawake kukutwa na nyara hizo za Serikali ni  aina mpya ya uhalifu kwa sababu nikiri tu kuwa wanaume ndiyo wanaofanya uhalifu wa namna hii, lakini kuna uwezekano mkubwa wa wanaume kuwinda na kuwapa wanawake nyama kuuza kwa sababu hawa hawakukutwa na nyara hizo porini bali walikutwa nazo nyumbani," amesema.

Amesema Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini wahusika pamoja na mtandao wao kuliko kukaa na wanawake hao ambao wamekutwa wakiwa ndani na nyara hizo za Serikali.