CCM Kiteto wakerwa na migogoro ya wakulima na wafugaji

Mwenyekiti wa CCM  Kiteto Hassan Hassani Losioki katika maadhimisho ya kutimiza miaka 46 ya CCM.

Muktasari:

  • Chama cha Mapinduzi wilayani Kiteto kimemwagiza Mkuu wa wilaya hiyo, Mbaraka Batenga kutatua migogoro ya wakulima na wafugaji na kusimamia kikamilifu watumishi wa Serikali.

Kiteto. Kutokana na migogoro ya ardhi Kiteto kati ya wakulima na wafugaji iliyokithiri wilayani Kiteto Mkoa wa Manyara, CCM kimemwagiza Mkuu wa wilaya hiyo, Mbaraka Batenga kutafuta suluhu ya kudumu ya kero hiyo.

 Akizungumza katika shughuli za kuelekea maadhimisho ya miaka 46 ya CCM leo Februari 3 wilayani hapa, Mwenyekiti wa chama hicho wilaya, Hassan Losioki amesema chama hicho hakina furaha kutokana na migogoro hiyo.

"Kwa nini migogoro ya ardhi kila mara Kiteto hasa wakati wa kilimo? Kuna ambao hawatimizi wajibu wao, chama tunataka Serikali itatue migogoro hii haraka," alisema.  

Akizungumzia suala hilo, Mkuu wa Wilaya hiyo, Mbaraka Batenga amewataka wakulima na wafugaji kutafuta shughuli nyingine zitakazowanufaisha kuliko kung’ang’ana na migogoor hiyo.

"Kuna wenzenu wananufaika na hewa ya ukaa, tena fedha ni nyingi sana wanazopata kuliko halmashauri kwa mwaka, hivyo angalieni kipi bora ili kilete manufaa ya haraka kwenu

"Mnahitaji fedha kwa ajili ya kumalizia hata miradi yenu mnakosa mngekuwa na miradi ya hewa ya ukaa mngepata fedha nyingi na kwa haraka mngetatua changamoto zinazowakabili sasa" amesema Batenga.

Akizungumzia fedha ambazo Serikali imetoa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Mbunge wa Jimbo la Kiteto Edward Lekaita amewaambia wananchi hao kuwa Serikali ina nia njema na wananchi, kwani ina mpango wa ujenzi wa barabara ga lami kutoka Narco- Kiteto na ambayo itakuwa chachu ya maendeleo.