Bandari ya Kwala kuanza kupokea mizigo Januari 2023

Muktasari:

Ujenzi wa bandari kavu ya Kwala mkoani Pwani wamefikia asilimia 95, Serikali yasema itaanza kutumika rasmi kuanzia Januari mwaka 2023.

Dar es Salaam. Serikali imesema bandari kavu ya Kwala iliyopo mkoani Pwani itaanza kupokea mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam Januari mwaka 2023.

 Kwa sasa ujenzi wa bandari kavu ya Kwala umefikia zaidi ya asilimia 95 na unatarajiwa kukamilika Disemba 30 mwaka huu.

Hayo yalielezwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, anayesimaia sekta ya uchukuzi, Gabriel Migire katika taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na wizara hiyo leo Jumapili Desemba 4, 2022.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Migire ameeleza hayo baada ya kukagua ujenzi wa barabara yenye urefu wa kilometa 15 kutoka Vigwaza hadi bandari ya  Kwala  inayojengwa kwa kiwango cha zege na kusimamiwa na Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads).

“Kuanza kutumika kwa bandari hii kutapungza msongamano wa mizigo na magari makubwa katika bandari ya Dar es Salaam,” amesema Migire.

Migire amesema bandari kavu ya Kwala itatumika kuhifadhi makasha ya kwenda nchi jirani za Burundi, Rwanda, DRC Congo, Uganda, Zambia na Malawi.

Mhandisi Joseph Marandu wa Suma-JKT anayesimamia ujenzi huo amesema mchakato huo katika hatua nzuri na wanatarajia kukamilisha ujenzi Desemba 30, 2022 akisema kwa sasa wanaendelea na kazi ya kuweka taa, kamera pamoja na kumalizia kuweka sakafu ngumu ya kuhifadhia Makasha.


Naye, mhandisi Jacob Mambo kutoka wakala wa Barabara hapa nchini (Tanroads), anayesimamia ujenzi wa barabara ya kutoka Vigwaza hadi bandari ya Kwala amesema hatua iliyobaki ni kuweka alama za barabarani pamoja na mzunguko eneo la Vigwaza shughuli itakayokamilika Desemba 7 mwaka huu.

“Tunategemea kupata maendeleo ya kijamii na kuongeza  kipato kwa mwananchi mmoja mmoja na kwa mustakabali wa maendeleo ya   Kwala na  mkoa wa Pwani,” amesema Mkazi wa Kwala Lilian Molel