Bakwata yamng’oa Sheikh Alhad Dar

Muktasari:

  • Baraza la Ulamaa limetengua uteuzi wa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum na kumteuwa Sheikh Walid Omar kukaimu nafasi hiyo.

Dar es Salaam. Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata) kupitia Baraza la Ulamaa limetengua uteuzi wa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Alhad Mussa Salum na kumteua Sheikh Walid Omar kukaimu nafasi hiyo.

 Uamuzi wa kumtengua Sheikh Alhad umekuja ikiwa imepita wiki moja tangu, kiongozi huyo alipotangaza kuivunja ndoa hiyo ya mtaalamu wa tiba mbadala, Juma Mwaka Juma maarufu kwa jina la Dk Mwaka na mkewe Queen Masanja Januari 25 mwaka huu, kufuatia ombi la mwanamke huyo kudai talaka.

Hata hivyo, siku mbili baadaye, yaani Januari 27, Baraza la Ulamaa lilikutana kwa dharura na kubatilisha uamuzi huo.

Akisoma taarifa hiyo iliyosainiwa na katibu wa baraza hilo, Hassan Chizenga leo Februari 2, 2023, Mjumbe wa Baraza hilo, Issa Othman alisema umetokena na kikao chao cha Februari 1 na 2, mwaka huu amesema uamuzi huo umefuatia kikao chake kilichofanyika Februari 1 na 2 jijini hapa chini ya Mwenyekiti wake, Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania Dk Abubakar Zubeir bin Ally.

“Baraza la Ulamaa katika kikao chake kilichofanyika Februari 1 na 2 jijini Dar es Salaam chini ya Mwenyekiti wake Mufti na Sheikh Mkuu wa Tanzania, Dk Abubakar Zubeir bin Ally limetengua uteuzi wa Sheikh Alhad Mussa Salum kama Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia leo Februari 2, 2023,” amesema.

Ameendelea kusema kuwa Mufti na Sheikh Mkuu, amemteua Sheikh Walid Alhad Omar kukaimu nafasi ya Sheikh wa Mkoa wa Dar es Salaam kuanzia leo Februari 2, 2023.