Watu 8 wauawa wakisherehekea siku ya kuzaliwa Afrika Kusini

Muktasari:

  • Watu wanane wameuawa wakisherehekea siku ya kuzaliwa ya mwenzao kufuatia shambulizi la ufyatuaji risasi lililofanywa na watu wawili nchini Afrika Kusini.

Dar es Salaam. Watu wenye silaha walifyatulia risasi kundi la watu waliokuwa wakisherehekea siku ya kuzaliwa mwishoni mwa juma katika kitongoji kimoja nchini Afrika Kusini, na kuwauwa watu nane na kuwajeruhi wengine watatu, polisi nchini humo wamesema leo Jumatatu.

Msherehekeaji wa siku ya kuzaliwa ni miongoni mwa waliouawa kwa kupigwa risasi katika mji wa Gqeberha, ambao zamani ulikuwa ukiitwa Port Elizabeth.

"Mmiliki wa nyumba hiyo alikuwa akisherehekea siku yake ya kuzaliwa wakati watu wawili wasiojulikana wenye bunduki waliingia ndani Jumapili jioni na kuanza kuwafyatulia risasi wageni," polisi wamesema katika taarifa yao.

“Watu wenye silaha waliwafyatulia risasi wageni. Watu wanane wamefariki huku wengine watatu wakiendelea kutibiwa hospitalini. Mwenye nyumba ni miongoni mwa waliofariki," imesema taarifa ya polisi.

Kwa mujibu wa VOA, Nomthetheleli Mene, Mkuu wa Polisi wa Mkoa wa Eastern Cape, amelaani mauaji hayo ambayo ameyaita ni ukatili wa kibinadamu.

Uchunguzi umeanzishwa kuhusu shambulio hilo na polisi wamesema msako wa kuwasaka wahusika unaendelea.

Mwaka jana Afrika Kusini ilishuhudia mfululizo wa matukio ya ufyatuaji risasi na kuua makumi katika baa tofauti katika vitongoji vya wafanyakazi huko Johannesburg na katika Jiji la mashariki la Pietermaritzburg.

Waziri wa Polisi Bheki Cele, Kamishna wa Polisi wa nchini humo, Fannie Masemola na wataalamu wa uhalifu wamekwenda eneo la shambulio ili kubaini madhara zaidi yaliyojitokeza.