Papa Francis kuhimiza amani Sudan Kusini

Papa Francis akisalimiana na Rais wa Sudan Kusini, Salva Kiir Mayardit.

Muktasari:

  • Papa Francis amehimiza  amani na maridhiano nchini Sudan Kusini wakati nchi hiyo ikitazamwa kwa makovu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.

Juba. Papa Francis amewasili Sudan Kusini leo Februari 3, 2023 katika ziara ya siku tatu ya kuhimiza amani na maridhiano katika nchi ambayo bado ina makovu ya vita vya wenyewe kwa wenyewe

Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP,  Papa Francis ametua Juba saa tatu usiku, katika ziara ya kwanza nchini humo tangu Taifa hilo lenye Wakristo wengi kupata uhuru kutoka kwa Sudan yenye Waislamu wengi mwaka 2011 baada ya miongo kadhaa ya mapambano ya umwagaji damu.

Amani imekosekana katika nchi ya Sudan Kusini, huku vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka mitano vikisababisha vifo vya watu zaidi ya 380,000, huku zaidi ya watu milioni nne wakiyahama makazi yao.

Papa mwenye umri wa miaka 86 anatarajiwa kukutana na waathiriwa wa mzozo huo, pamoja na viongozi wa kisiasa na makanisa nchini humo, katika maombi na misa ya nje inayotarajiwa kuvuta umati mkubwa wa watu.

Ziara hiyo ya tano kwa Francis barani Afrika ilikuwa imeratibiwa kufanyika 2022 lakini ilibidi iahirishwe kwa sababu ya matatizo ya papa katika goti lake

Papa ataungana nchini Sudan Kusini na Askofu Mkuu wa Canterbury na msimamizi wa Baraza Kuu la Kanisa la Scotland katika kile kinachoelezwa kuwa ni hija ya amani.

Ziara hiyo imekuwa ikitarajiwa kwa muda mrefu katika nchi yenye watu milioni 12 wacha Mungu ambapo kanisa hilo ni taasisi inayoheshimika na yenye historia ndefu ya kujenga amani.

Papa Francis aliahidi mwaka wa 2019 kusafiri hadi Sudan Kusini alipowakaribisha viongozi wawili wanaopigana katika makao makuu ya Vatican na kuwataka kuheshimu usitishaji mapigano uliopiganwa kwa bidii kwa watu wao.

Katika matukio ambayo yalijiri nchini Sudan Kusini, ambapo asilimia 60 ya watu ni Wakristo, kiongozi huyo alipiga magoti na kumbusu miguu ya maadui wawili ambao majeshi yao yalikuwa yameshutumiwa kwa ukatili wa kutisha.