Papa ahimiza kumaliza mzozo DRC

Papa Francis wakati akiwasili Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo jana kwa ziara nchini humo.

Muktasari:

  • Papa Francis amewataka watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kusameheana na kutoa wito kwa Wakristo wanaohusika katika vita kuweka chini silaha zao.

Dar es Salaam. Papa Francis amewataka watu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kusameheana na kutoa wito kwa Wakristo wanaohusika katika vita kuweka chini silaha zao.

 Kwa miongo kadhaa migogoro ya kivita imeua mamilioni ya watu nchini humo.

Katika siku ya kwanza ya ziara yake, papa Francis ameongoza Misa ya wazi kwa umati wa watu waliokadiriwa kuwa zaidi ya milioni moja kwenye Uwanja wa Ndege katika mji mkuu Kinshasa.

Wakongo wameupokea ujio wa Papa nchini humo kwa mwitikio mkubwa baada ya kujitokeza kwa wingi na kuonyesha faraja zao.

Wanawake wengi walivalia nguo zenye picha yake, kama ilivyo desturi katika nchi nyingi za Afrika kuwaheshimu watu mashuhuri, huku watoto wakipanda kwenye ndege isiyotumika ili waonekane vizuri katika ibada hiyo iliyofanyika kwenye uwanja wa ndege.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, mzozo wa silaha umesababisha watu milioni 5.7 kuwa wakimbizi wa ndani na milioni 26 wakikabiliwa na njaa kali nchini humo.

Papa Francis amesema Mungu anataka watu kuwa na ujasiri wa kuwasamehe wengine kutoka moyoni.

"Inatufaa kusafisha mioyo yetu ya hasira na majuto, na kila dalili ya chuki na uadui!" amesema Papa na kuongeza,

"Na iwe wakati mzuri kwa ninyi nyote katika nchi hii mnaojiita Wakristo lakini mkishiriki katika vurugu. Bwana anawaambia: 'Weka mikono yako chini, kukumbatia huruma."

Alhamisi itakuwa siku yake ya mwisho katika ziara yake nchini Congo, kabla ya kuondoka Ijumaa kuelekea Sudan Kusini ambayo pia inayokabiliwa na migogoro na njaa.

Mashariki mwa Kongo imekumbwa na ghasia zinazohusishwa na anguko la muda mrefu na tata la mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 katika nchi jirani ya Rwanda. Congo inaishutumu Rwanda kwa kuunga mkono kundi la waasi la M23 linalopigana na wanajeshi wa Serikali mashariki mwa nchi hiyo jambo ambalo Rwanda imekanusha.