Boris adai Putin alitishia kumuua

London. Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza, Boris Johnson ametoka hadharani akidai Rais wa Russia, Vladimir Putin alimtishia kumuua kwenye mazungumzo yao kwenye simu kuhusu vita vya Ukraine.

Johnson akiwa Waziri Mkuu wa Uingereza alizungumza na Putin Februari 2022 kwa njia ya simu, akilaumu uamuzi wa nchi hiyo wa kuivamia Ukraine kutasababisha iwekewe vikwazo.

“Alinitishia mimi akasema, Boris, sitaki kukuumiza, lakini kwa kombora itakuwa dakika moja tu,” alisema Johnson akinukuu maneno ya Putin kwenye mazungumzo yao kwa simu.

Johnson kwa maelezo yake alikuwa akimuonya Putin kuhusu uamuzi wake wa kuivamia Ukraine kwamba Russia ingewekewa vikwazo visivyo na ukomo.

Kwa mujibu wa Johnson, tishio hilo lilitolewa baada ya yeye kuutembelea mji mkuu wa Kyiv, nchini Ukraine na kumuhakikishia Rais Volodymyr Zelensky kwamba Serikali ya Uingereza itaungana naye iwapo Russia itaivamia.

Johnson alisema baada ya kurejea Uingereza alifanya mazungumzo ya muda mrefu kwenye simu na Putin ambapo kiongozi huyo alikataa kuwepo mipango ya kuivamia Ukraine, licha ya wanajeshi wake kuwa tayari mpakani.

Alisema, alimwabia Putin kuwa vita hivyo vitasababisha ‘jangwa’ na kulazimisha kuwekewa vikwazo.

Johnson akimnukuu Putin alisema: “Boris, umesema Ukraine haijiungi na Nato (Umoja wa kujihami wa nchi za magharibi) wakati wowote sasa…nini maana ya wakati wowote sasa?”

Na nilimwambia, “haitajiunga Nato kwa muda ujao unaojulikana.

Johnson aliongeza kuwa alimweleza Putin kama atavamia Ukraine wataweka vikwazo kwa mafuta na gesi.

“Tunaweka vikwazo kila kitu, tutazuia boti zenu za starehe,” alisema Johnson akimwambia Putin.

Si kawaida kwa Rais wa nchi, tena ambaye ni mjumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kutoa matamshi binafsi ya kumtishia kumuua kiongozi wenzake wa nchi nyingine.

Russia na Uingereza ni miongoni mwa wajumbe watano wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Wajumbe wengine ni China, Ufaransa na Marekani.

Hata hivyo, Russia jana imekanusha madai ya Johnson ikisema amedanganya kwa kusema Rais Putin alitishia kumuua kwenye mazungumzo yao ya simu ya Februari mwaka jana.

Msemaji wa Ikulu, Dmitry Peskov akizungumza na waandishi wa habari jana alisema Johnson ameongeza chumvi kwenye madai yake hayo.

“Alichosema Johnson si kweli. Si kweli. Kwa usahihi zaidi ni uongo…hakukuwa na tishio la kombora,” alisema Peskov.

Marufuku Russia

Baada ya mazungumzo ya simu ya viongozi hao ya Februari, baadaye Russia ilitangaza kumpiga marufuku Johnson kuingia nchini humo.

Serikali ya Russia ilitangaza kumpiga marufuku Johnson na maofisa wengine 12 wa Serikali ya Uingereza kuingia nchini humo, baada ya London kuiwekea vikwazo Moscow kutokana na operesheni yake ya kijeshi nchini Ukraine.Russia ilitoa tamko hilo kupitia waziri wake wa mambo ya nje.

Pia, ilimpiga marufuku Waziri wa Mambo ya Nje, Liz Truss (baadaye alikuja kuwa Waziri Mkuu aliyekaa kwa muda mfupi), Waziri wa Ulinzi, Ben Wallace pamoja na wafanyakazi wengine 10 wa Serikali ya Uingereza.

Viongozi wengine wa Uingereza waliopigwa marufuku kuingia nchini Russia ni Dominic Raab, Grant Shapps, Priti Patel, Rishi Sunak (ambaye ni Waziri Mkuu wa sasa), Kwasi Kwarteng, Nadine Dorries, James Heappey, Nicola Sturgeon, Suela Braverman pamoja na Thereza May (aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza).

Pia, Julai 2022, wakati Johnson alijiuzulu uwaziri mkuu, Russia ilionekana kufurahia ambapo msemaji wa Rais Putin, Peskov alisema “Johnson hatupendi kabisa na sisi (hatumpendi) pia.”
Peskov alisema Russia ina matumaini watu wenye taaluma zaidi ambao wanaweza kufanya maamuzi kupitia mazungumzo watachukua nafasi ya uwaziri mkuu iliyoachwa na Johnson.

Mbali na kauli ya Peskov, msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Russia, Maria Zakharova alimkejeli Johnson kwamba kuondoka kwake madarakani kumetokana na bomu alilolitengeneza mwenyewe na kwamba hilo ni funzo la ‘usitafute kuiangamiza Russia.’