Wafanyabiashara walia vifaranga vya kuku kutoka nje, Serikali yafafanua

Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya kuzalisha vifaranga ya Organia, Albert Momdjian (wa pili kushoto) akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Disemba 04, 2022, kuhusu changamoto wanazokutana nazo wazalishaji wa vifaranga kutokana na kupanda kwa bei ya vyakula vya kuku.

Kutoka kulia ni Meneja rasilimali watu wa kampuni hiyo, Shecky Mohamedi, Meneja huduma kutoka Tanzania Poultry Farm (TPF), Thabit Batebga na Ofisa masoko wa Organia, Martha Kimambo

Muktasari:

Wafanyabiashara wa kuku na wauzaji vifaranga wameiomba Serikali kusitisha biashara ya vifaranga vinavyoletwa kutoka nje ya nchi kwa kuwa vimechangia kushuka kwa bei ya kuku sokoni na kuwapa hasara katika biashara hiyo.


Dar es Salaam. Wafanyabiashara wa kuku na wauzaji vifaranga wameiomba Serikali kusitisha biashara ya vifaranga vinavyoletwa kutoka nje ya nchi kwa kuwa vimechangia kushuka kwa bei ya kuku sokoni na kuwapa hasara katika biashara hiyo.

Wakati wafanyabiashara wakizungumza hayo, Serikali imesema kampuni zilizoruhusiwa kuingiza vifaranga hao zinakoma kufanya kazi hiyo Desemba mwaka huu.

Akizungumza leo Jumamosi Desemba 3, 2022 Mkurugenzi wa Huduma za Mifugo kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Profesa Hezron Nonga amefafanua kuwa wanaoingiza sasa vifaranga hivyo ni kati ya kampuni ziliruhusiwa kuagiza bidhaa hizo kipindi cha uhaba wa vifaranga nchini mwaka 2020 na 2021 wakati ugonjwa wa Uviko.

Hata hivyo amesema Agosti mwaka huu Serikali imesitisha uagizaji huo, lakini kampuni hizo zilifikisha malalamiko yao Serikalini kuwa walikuwa wameshavilipia na hivyo kuamuliwa wamalizie oda zao ambapo kwa wiki huingiza vifaranga 15,000.

Profesa Nonga amezitaja kampuni hizo kuwa ni The One Agro Enterprises Ltd iliyoruhusiwa kuingiza vifaranga 494,000 na Wolowolo Animal Center vifaranga 150,000 na wote wameshaingiza, idadi iliyobaki hadi sasa ni vifaranga 364,000.

Akizungumzia changamoto hiyo Mkurugenzi  Mtendaji wa kampuni ya kuzalisha vifaranga ya Organia, Albert Momdjian  leo  jijini Dar es Salaam amesema vifaranga vinavyoletwa kutoka nje vinauzwa kwa bei ya Sh1,000 na vinavyopatikana Tanzania vikiuzwa Sh1,800 na hivyo kufanya kutokuwa na usawa wa ushindani katika soko.

Momdjian amesema wamekuwa wakiingia gharama inayochangiwa na kupanda kwa bei ya chakula cha kuku, upatikanaji wa maji na umeme wa uhakika.

"Kusema ukweli hali siyo nzuri kwa sasa katika biashara hii kwani sio sisi tu tunaoumia bali na wateja wetu hivyo tumeamua kusimama nao kwa kuwa bila wao sisi ni bure,"amesema.

Mwenyekiti wa Chama cha Wafuga Kuku (TABROFA), Costa Mrema amesema uingiaji wa vifaranga hivyo  umeporomosha soko la kuku kutoka Sh5,300 hadi Sh5,500

Naye, Flora Kamote ambaye ni mfugaji kuku amesema amelazimika kuacha biashara hiyo tangu mwezi wa kumi baada ya kupata hasara ya zaidi ya kuku 2,000 kwa kuwauza kwa bei ya hasara ya Sh5,000.

"Hasara hiyo sijaisahau hadi leo hivyo sijataka kusikia kufuga tena licha ya kuwa haijaniathiri mimi tu bali na watu wengine niliokuwa nimewaajiri kupitia kazi hii ambayo wanaitegemea katika kuendesha maisha yao na familia zao.