Azam ya ubingwa hii hapa

Muktasari:
- Katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), nako ilikumbana na majanga. Azam ilikuwa haijawahi kutolewa hatua za awali za michuano hiyo tangu ipande Ligi Kuu 2008-2009. Mbeya City ndio iliyowatibulia kwa kuitupa nje kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ya dakika 90 ya pambano la hatua ya 32 Bora.
AZAM FC ni kama imemaliza msimu mapema. Ilianza kung’olewa katika Ligi ya Mabingwa Afrika iliyorejea msimu huu baada ya kupita miaka 10 tangu ilipoicheza mara ya kwanza na mwisho 2015. Waliowatibulia walikuwa Wajeda wa APR ya Rwanda.
Katika michuano ya Kombe la Shirikisho (FA), nako ilikumbana na majanga. Azam ilikuwa haijawahi kutolewa hatua za awali za michuano hiyo tangu ipande Ligi Kuu 2008-2009. Mbeya City ndio iliyowatibulia kwa kuitupa nje kwa penalti 4-2 baada ya sare ya 1-1 ya dakika 90 ya pambano la hatua ya 32 Bora.
Huko katika Ligi Kuu Bara licha ya kuanza kwa kasi na kuonekana kama inalitaka taji, ghafla upepo uliwabadilikia kwa kushindwa kushikilia bomba mbele ya Simba na Yanga zinazochuana kwa sasa katika nafasi mbili za msimamo wa ligi hiyo.
Kwa sasa Azam inachuana kumaliza nafasi ya tatu dhidi ya Singida Black Stars na si tena kuwania taji.
Hao ndio Azam FC ambao ni moja ya timu zenye kila kitu kinachotakiwa kwa timu inayoendeshwa kisasa. Ina uwanja binafsi wa Azam Complex, uliopo Chamazi ukiwa umejitosheleza kwa kila kitu. Ina msuli mnene wa kifedha unaoiwezesha kuajiri au kusajili kocha na mchezaji wa aina yoyote.
Hata hivyo, imekuwa ikikwama njiani. Ina taji moja tu la ubingwa wa Ligi Kuu Bara, iliyolinyakua msimu wa 2013-2014 kwa rekodi ya aina yake ya kutopoteza mchezo hata mmoja.
Ndio, Azam hiyo iliyopita chini ya makocha wawili, Stewart John Hall kisha Joseph Omog, ilitisha. Ilizisimamisha Simba na Yanga na kubeba ubingwa ikiingia katika historia ya moja ya klabu tisa zilizotwaa taji la Ligi Kuu Bara tangu mwaka 1965.

Mwanaspoti inakuletea kumbukumbu ya ubingwa huo wa Azam na na walipo kwa sasa mastaa waliounda skwadi zima lililoiheshimisha timu hiyo nchini.
Kama hujui Azam mbali na kubeba ubingwa msimu huo, pia iliifikia rekodi ya Simba iliyoiweka msimu wa 2009-2010 wa kubeba taji la Ligi bila kupoteza, kisha ikajiongeza kwa kuendeleza moto na kuandika rekodi mpya ya kucheza jumla ya mechi 38 bila kupoteza kabla ya kuja kuvunjwa na Yanga iliyocheza mechi 49 bila ya kupoteza.
TAJI LILIPATIKANA MBEYA
Kama hujui, Azam ilibeba taji la Ligi Kuu msimu wa 2013-14 ikiwa kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya kwa kuitungua Mbeya City iliyokuwa mwenyeji kwa mabao 2-1.
Baada ya kuifunga Mbeya City mabao 2-1, Aprili 13, 2014, huku ikiwa imesaliwa na mechi moja mkononi dhidi ya JKT Ruvu (sasa JKT Tanzania) ambao pia ilishinda kwa bao 1-0, ilikabidhiwa taji la Ligi Kuu Bara Aprili 19, 2014.
Ushindi huo dhidi ya Mbeya City uliifanya Azam kufikisha pointi 59 ambazo zilikuwa haziwezi kufikiwa na timu yoyote wakiwamo waliokuwa watetezi Yanga waliokuwa wakichuana nao kileleni kwa muda mrefu, mbali ya Simba na Mbeya City.
Azam ilimaliza msimu huo kwa kuvuna jumla ya pointi 62 kupitia mechi 26, ikishinda 18 na kutoka sare nne, ikifunga mabao 51 na kufungwa 15.
Yanga ilimaliza ya pili kwa pointi 56 na Mbeya City ikafuata na alama 49, huku Simba ikimaliza ya nne ikivuna pointi 38 tu kupitia mechi 26.
Mabao ya ushindi yaliyowapa taji Azam msimu huo, yaliwekwa kimiani na Gaudence Mwaikimba aliyekwamisha la kwanza katika dk43 akimalizia pasi ya beki wa kulia wa wakati huo, Erasto Nyoni na kudumu hadi mapumziko.

Kipindi cha pili Mbeya City, ilichomoa bao hilo katika dk70 kupitia Mwagane Yeya kabla ya John Bocco ‘Adebayor’ kufunga bao la ushindi dakika 86, bao lililosababisha nyota wa Mbeya City kumzonga mwamuzi Nathan Lazaro kutoka Kilimanjaro wakiamini mfungaji alifanya madhambi wakati anaupora mpira kwa beki wa wenyeji. Hata hivyo, refa huyo hakurudi nyuma badala yale alimlima kadi nyekundu Mwagane Yeya kisha kuendelea na yake baada ya fujo za dakika zisizozidi tatu.
Bao la Bocco liliandikisha rekodi nyingine tamu kwa straika huyo, kwani yeye ndiye aliyefunga mabao mawili yaliyoipandisha Azam Ligi Kuu 2008, mjini Dodoma katika fainali ya Ligi ya Taifa kwa kuifunga Majimaji 2-0.
Hata hivyo, siku hiyo mabingwa wapya hao wa Ligi Kuu msimu huo, walilazimika kutoka uwanjani kwa kusindikizwa na askari Polisi waliokuwa na kibarua cha kuwadhibiti mashabiki wa City walioliamsha uwanjani hapo kwa kukerwa na kipigo cha timu yao.
Kama hujui, Azam ilikuwa ni timu ya kwanza kuifunga Mbeya City kwenye Uwanja wa Sokoine, jijini Mbeya jambo lililowauma mashabiki wa klabu hiyo, lakini haikusaidia kuifanya Azam isiwe bingwa na kuwa timu ya kwanza tangu Mtibwa Sugar ilipotwaa mara mbili mfululizo 1999 na 2000 kubeba ndoo nje ya Simba na Yanga.
Na hadi unaposoma makala hii, hakuna timu nyingine tena iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu tangu Azam ibebe ndoo hiyo ya msimu wa 2013-14.

Katika pambano hilo lililoipa taji Azam ikiwa na mechi moja mkononi, vikosi vilipangwa hivi;
MBEYA CITY: David Burhan, Aziz Sibo/Hamad Kibopile, Hassan Mwasapili, Yussuf Abdallah, Yohana Morris, Anthony Matogolo, Mwagane Yeya, Steven Mazanda, Paul Nonga, Saad Kipanga/Alex Sethi na Deus Kaseke.
AZAM FC; Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadiel Michael, Said Morad, Aggrey Morris, Kipre Balou, Himid Mao, Salum Abubakar, Gaudence Mwaikimba, John Bocco na Kipre Tchetche/Kevin Friday.
KIKOSI BINGWA
AISHI MANULA
Ndiye aliyekuwa langoni katika pambano hilo la kibingwa akimkalisha benchi mkongwe, Mwadini Ali.
Kwa sasa Manula aliyewahi kuwa kipa Bora wa Ligi Kuu kwa misimu takribani minne mfululizo, yupo Simba iliyomsajili msimu wa 2017-2018 na kugeuka kipa tegemeo wa timu hiyo akiisaidia kuipa ubingwa kwa misimu minne mfululizo.
Hata hivyo, mabao matano aliyotunguliwa katika Dabi ya Kariakoo iliyopigwa Novemba 5, 2023 akitokea majeruhi, kisha kupigwa kamba mbili safi na Samson Mbangula kwenye Uwanja wa Jamhuri, mapema mwaka jana alimtibulia Manula na kuishia kuchomeshwa mahindi akiachwa benchini au jukwaani na kusalia kuwa kipa wa mazoezini tu.
Katika mechi hiyo ya kibingwa, Manula alikuwa langoni na kuokoa michomo mingi ya Mbeya City hata kipindi cha pili kabla ya kupangua vibaya shuti la Deus Kaseke na mpira kumfikia Mwagane Yeya aliyekwamisha bao la kusawazisha katika dakika ya 70.
ERASTO NYONI
Mkongwe huyo anayeendelea kukiwasha kwa sasa akikipiga Namungo anayoitumikia kwa msimu wa pili mfululizo kama beki wa kati, siku ya mechi iliyowapa taji Azam, alisimama kama beki wa kulia na aliupiga mwingi kama kawaida akiasisti bao la kwanza.
Bao hilo lilifungwa na straika aliyekuwa mrefu kuliko wachezaji wote, Gaudence Mwaikimba dakika mbili kabla ya mapumziko baada ya kupokea pasi murua ya Nyoni.

GADIEL MICHAEL
Beki wa kushoto aliyekuwa mkali wao katika nafasi ya pembeni alikinukisha siku hiyo kwa kukaba na kupeleka mashambulizi langoni mwa Mbeya City.
Kwa sasa beki huyo yupo Singida Black Stars baada ya kutoka kucheza soka la kulipwa huko Afrika Kusini, huku akiwa ameshapita timu kadhaa ikiwamo Yanga na Singida Big Stars, japo kwa sasa haonekani uwanjani, lakini jina lake lipo katika historia ya Azam kwa kuiwezesha kubeba ubingwa wa Ligi Kuu Bara kabla ya kusajiliwa na Yanga baadaYe.
SAID MORAD
Beki mtu kazi aliyekuwa na sura ya kimanga, lakini katili miguuni, ndiye aliyesimama kati sambamba na Aggrey Morris na kuwazuia washambuliaji hatari wa Mbeya City kama Paul Nonga, Mwegane Yeya na wengine waliokuwa tishio tangu timu hiyo ilipopanda daraja.
Kwa sasa Morad ameachana na soka la ushindani, akiendelea na ishu zake binafsi, lakini hawezi kusahaulika kirahisi, kwani ni mmoja ya waliochangia Azam kubeba ubingwa bila kupoteza mechi yoyote na kuziduwaza Simba na Yanga zilizokuwa zikipokezana taji.
AGGREY MORRIS
Beki kitasa aliyekuwa akicheza kwa akili, nguvu na maarifa na hata pale palipohitaji undava, Aggrey ni nahodha wa zamani wa Kipanga na Taifa Stars. Katika mechi hiyo ya Aprili 13, 2014 iliyowapa taji Azam, alisimama mkoba sambamba na Morad.
Licha ya Mwegane Yeya kufunga bao la kufutia machozi kabla ya kutolewa kwa kadi nyekundu, lakini jasho lilimtoka kama ilivyokuwa kwa Nonga na wengine waliocheza eneo la ushambuliaji kwa ukabaji wa beki huyo wa kazi na kuibebesha Azam taji pekee la Ligi.
Kwa sasa Morris ni kocha wa timu ya taifa ya Vijana U17, Serengeti Boys aliyopewa baada ya kusomea ukocha alipostaafu kwa heshima Azam misimu michache iliyopita.
MICHAEL BALOU
Kiungo mkabaji huyo aliyekuwa pacha wa Kipre Tcheche waliosajiliwa kutoka Ivory Coast, ndie aliyesimama kati siku hiyo na kupelekeshana na viungo wa Mbeya City akiwamo mkongwe Steven Mazanda na Anthony Matogolo na kukata umeme sana.
Kiungo huyo, waliyeshirikiana na kina Mudathir Yahya, Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na Himid Mao na kuifanya iwe na kiungo cha kukata na shoka, aliondoka Azam mwaka 2016 baada ya kumaliza mkataba na kumfuata pacha wake, Kipre Tchetche aliyekuwa akicheza Al Nahda ya Oman.
HIMID MAO ‘NINJA’
Nyota huyo aliyekuwa mkali wao katika eneo la kiungo mkabaji, ndiye aliyecheza kama namba saba siku ya mechi hiyo na kukata umeme kwelikweli huku akisambaza mipira kwa wachezaji wa eneo la ushambuliaji.
Ninja, anayeitumikia pia timu ya taifa, Taifa Stars aliondoka Azam 2018 baada ya kuuzwa katika klabu ya Petrojet ya Misri na kucheza soka la kulipwa katika klabu kadhaa kabla ya kutua Talaea El Gaish iliyopo Ligi Kuu anayoitumikia hadi sasa.

SALUM ABUBAKAR ‘SURE BOY’
Kiungo mshambuliaji huyo anayemudu kucheza pia kama mkabaji, alikuwa sehemu ya kikosi kilichoshuka uwanjani na kuihakikishia Azam ubingwa wa kwanza na wa pekee wa Ligi Kuu katika mchezo huo dhidi ya Mbeya City.
Mkali huyo, alikuwa mchezaji muhimu wa kikosi hicho akiwa mmoja ya waasisi walianza nao katika Ligi Kuu mara ilipopanda daraja na kwa sasa anakipiga Yanga aliyojiunga nayo misimu mitatu iliyopita na kukusanya mataji zaidi akiwa na wababe hao.
GAUDENCE MWAIKIMBA
Mshambuliaji aliyekuwa mwili jumba aliyewahi kutamba na klabu za Ashanti United, Moro United, Yanga na Taifa Stars, alikuwa mmoja ya wachezaji mahiri wa Azam kipindi hicho na alihusika kufunga bao la kwanza lililotengeneza njia ya ubingwa.
Mwaikimba alipokea pasi tamu ya Erasto Nyoni na kutumbukiza mpira wavuni mbele ya kipa David Burhan katika dk43 kabla ya Bocco kufunga bao la ushindi wakati matokeo yakiwa 1-1 kutokana na wenyeji Mbeya City kulichomoa dakika ya 70 ya mchezo huo.
Kwa sasa Mwaikimba anaendelea na mishemishe zake baada ya kustaafu soka la ushindani tangu aliposikika akikipiga Boma FC ya Kyela Mbeya.
JOHN BOCCO ‘ADEBAYOR’
Straika huyu aliyetumika kama namba 10 katika pambano hilo la Mbeya akipokezana na Mwaikimba, ndiye aliyeihakikisha Azam kubeba taji hilo, kama alivyoipandisha daraja 2007.
Bocco alifunga bao la ushindi dakika ya 86 akiupoka mpira mbele ya mabeki wa Mbeya City walioshindwa kuokoa mpira wa Kipre Tchetche na kuzua tafrani kwa wachezaji na mashabiki wa timu wenyeji.
Kwa sasa mkongwe huyo anakipiga JKT Tanzania aliyojiunga nayo msimu huu baada ya kuitumikia Simba kwa misimu saba na kutwaa nao mataji manne ya Ligi Kuu tangu 2017-18 ilipomsajili sambamba na Nyoni, Manula na Shomary Kapombe.
Bocco ndiye anayeshikilia rekodi ya mfungaji wa muda wote wa Ligi Kuu akiwa na mabao 156 kupitia misimu 17, lakini akiitumikia Azam misimu tisa na kuifungia mabao zaidi ya 80 ya Ligi akibeba nayo mataji kibao ikiwamo kuwa mfungaji bora 2011-12 kabla ya kuhamia Simba na kuendelea ubabe akitwaa pia kiatu hicho 2020-21.
KIPRE TCHETCHE
Nyota anayeendelea kuimbwa Chamazi, Kipre Tchetche licha ya kwamba hakufunga bao katika mechi hiyo ya ubingwa, ni mmoja wa wachezaji walioibeba Azam msimu huo na mingine kabla ya kutimkia Oman 2015.
Alitua Azam 2011 akitokea klabu ya JC Abidjan akiwa na pacha wake, Kipre Balou na kukiwasha kinoma akitwaa Kiatu cha Dhahabu msimu wa 2012-2013 kwa mabao 17.
Katika mchezo huo ndiye pekee aliyebadilishwa kwa kumpumzishwa dakika ya 51 na nafasi yake kuchukuliwa na Kelvin Friday.
Baada ya kuipa Azam ubingwa wa Ligi Kuu kisha mataji ya Kombe la Mapinduzi na Kombe la Kagame 2015, mwamba alitimkia Oman kujiunga na Al Nahda kisha kupita Al Suwaiq na kuibukia Malaysia anakoendelea kukipiga hadi sasa akiwa na Kuching City.
AKIBA:
Benchini kulikuwa na wachezaji wa akiba saba na mmoja tu, Kelvin Friday ndiye aliyeinuliwa kuingia uwanjani kipindi cha pili, kumpokea Kipre Tchetche.
Wengine walioishia kuwa washangiliaji ni kipa Mwadini Ally aliyekuwa akijiandaa kukabidhi mikoba kwa Manula aliyekuwa chipukizi kipindi hicho na kuaminika zaidi kikosini.
Pia kulikuwa na David Mwantika beki wa kati mwili jumba, Jabir Aziz ‘Stima’, kiungo fundi wa mpira, Brian Umony, raia wa Uganda aliyewahi kurejea nchini kuitumikia Simba, Mudathir Yahya na Khamis Mcha ‘Vialli’ ambao bado wanaendelea kukiwasha.
HAWA PIA WALIKUWAPO
Kikosi hicho kilikuwa na nyota wengine kama Mkenya Jockins Atudo na Abdalla Khamis, viungo Frank Domayo, Faridi Mussa, Mnyarwanda Ally Niyonzima na Yahya Zayd na Seif Rashid Karihe aliyepo Mashujaa kwa sasa.
KOCHA
Timu hiyo kwa msimu huo ilifundishwa na makocha wawili kila mmoja akiiongoza katika mechi 13 bila ya kupoteza, Mcameroon Joseph Omog, ndiye aliyewapa ubingwa akiipokea timu katikati ya msimu kutoka kwa kocha Muingereza, Stewart Hall.
Omog alikomaa na mechi 13 zilizosalia bila kupoteza kama alivyofanya mtangulizi wake na kuiwezesha Azam kubeba taji hilo la kwanza na la pekee la Ligi Kuu kwa timu hiyo, kisha kuendelea na moto kabla ya kuachana na timu ilipotolewa na Al Merrikh katika mechi ya awali ya michuano ya CAF. Omog aliwahi kurudi nchini kuitumia Simba.
Kocha huo aliyekuwa ametokea klabu ya AC Leopards ya Congo Brazzaville aliyotwaa nayo ubingwa wa Kombe la Shirikisho Afrika 2012-2013 kwa sasa amerejea kuinoa tena Leopards.