Wenyeviti Serikali za mitaa watakiwa kuchangisha fedha ujenzi wa madarasa

Wenyeviti wa vitongoji vya Mamlaka ya Mji mdogo wa Mirerani Wilayani Simanjiro Mkoani Manyara, wakila kiapo kushika nafasi zao leo. Picha na Joseph Lyimo

Muktasari:

Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zephania Chaula amewapa mwezi mmoja wenyeviti 24 wa vitongoji vya mji mdogo wa Mirerani kuchangisha mchango wa  ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa mapya ya shule za msingi.


Mirerani. Mkuu wa Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, Zephania Chaula  amewapa mwezi mmoja wenyeviti 24 wa vitongoji vya mji mdogo wa Mirerani kuchangisha mchango wa  ujenzi wa vyumba 10 vya madarasa mapya ya shule za msingi.

Ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Novemba 27, 2019 katika hafla fupi ya kuapishwa wenyeviti 24 wa vitongoji vya mamlaka ya mji mdogo wa Mirerani waliochaguliwa Novemba 24, 2019 kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Chaula amesema wenyeviti hao wanatakiwa kusimama michango ya ujenzi wa madarasa, kwamba kila kaya itatoa Sh5,000.

Amesema mji mdogo wa Mirerani una shule sita za msingi ambazo ni Mirerani, Jitegemee, Songambele, Tanzanite, Endiamtu na Zaire.

"Hakikisheni mnasimamia hilo kwa kukusanya michango ili shule zitakapofunguliwa mwezi Januari wanafunzi wa darasa la kwanza waingie darasani," amesema Chaula.

Mwenyekiti wa kitongoji cha Tanesco, Justin Abraham amesema watasimama kuhakikisha maagizo ya mkuu huyo wa wilaya yanatekelezwa kwa muda muafaka.

Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Mirerani, Godfrey Haule akizungumza baada ya kuwaapisha wenyeviti hao amewataka wasiwe na upendeleo.