Uchaguzi palepale, asema Jafo

Dar es Salaam. Serikali imeendelea kusimamia msimamo wake kuwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa ulifanyika Novemba 24 mwaka huu, licha ya vyama saba vya upinzani kujitoa.

Tayari vyama vya Chadema, NLD, ACT-Wazalendo, NCCR-Mageuzi, UPDP, CUF na Chauma kwa nyakati tofauti vimetangaza kujitoa katika uchaguzi huo, huku vikiitaka Ofisi ya Rais (Tamisemi) kuacha kutumia nemba za vyama vyao katika karatasi za kupigia kura.

Vyama hivyo vimejitoa vikidai kutotendewa haki kwa wagombea wao, huku baadhi ya viongozi wa vyama hivyo wakiitaka Serikali kuufuta mchakato mzima na kiitishwe kikao kati ya viongozi hao na Serikali kwa ajili ya kutafuta suluhisho ya pamoja.

Wakati viongozi hao wakieleza hayo, baadhi ya viongozi wa dini juzi, walishauri kuwepo kwa meza ya mazungumzo itakayowakutanisha pande mbili huku wengine wakitaka uchaguzi huo usimamiwe na chombo huru.

Hata hivyo, akizungumza na Mwananchi jana kwa simu kuhusu kauli ya viongozi wa dini, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tamisemi), Selemani Jafo alijibu kwa kifupi “No Comment”.

Lakini alifafanua kuwa Serikali inaendelea na maandalizi ya uchaguzi huo.

Alisema baada ya hatua ya kurejesha fomu na wagombea kupitishwa, hatua inayofuata sasa ni ya kampeni itakayoanza Novemba 17.

Akizungumzia madai ya vyama kujitoa, Jafo alisisitiza mchakato wote unaendeshwa kisheria na kikanuni na kwamba kanuni zinaeleza mgombea hawezi kujitoa kwa matamko.

Alisema tatizo la baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa ni kutosoma kanuni za uchaguzi huo hasa ile ya 19 inayozungumzia mgombea kujitoa.

Hivyo, alisisitiza kuwa hakuna jina la mgombea litakalotolewa kama atakuwa amekidhi vigezo na jina likapitishwa kwa ajili ya kupigiwa kura.

“Hatuwezi kuyaondoa eti kwa sababu tu viongozi wao wa kitaifa wanasema chama kimejitoa kwenye uchaguzi huu. Wasome Kanuni, na sisi Serikali kama tutaamua kuwasikiliza wao, tutakuwa tunavunja kanuni Namba 19.”