Tetemeko la ardhi lazua taharuki Katavi, watoto wawili wajeruhiwa

Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera
Muktasari:
Tetemeko la ardhi lenye ukubwa wa 55 vipimo vya Ritcha limetokea mkoani Katavi nchini Tanzania na kusababisha madhara ya nyumba kutengeneza nyufa pamoja na kujeruhi watoto wawili.
Katavi. Hofu imetanda kwa wakazi wa Mkoa wa Katavi nchini Tanzania kufuatia kuibuka tetemeko la ardhi ambalo linakadiriwa kuwa na ukubwa wa 5.5 katika vipimo vya Ritcha.
Akizungumza na Mwananchi Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Juma Homera amesema tukio hilo limetokea usiku wa kuamkia leo Jumatatu Septemba 9, 2019 saa 9:40 usiku.
Homera amesema watoto wawili wa familia ya Magashi Itenga mkazi wa kijiji cha Jilabela Manispaa ya Mpanda, wamejeruhiwa na kupata majeraha madogo baada ya kuangukiwa na ukuta wa nyumba wakiwa wamelala .
“Tetemeko hili limedumu kwa dakika tatu, mpaka sasa tumepokea taarifa za watoto wawili, miaka saba na mwingine minane, wameangukiwa na ukuta, walipata matibabu katika zahanati ya Inteka na hali zao zinaendelea vizuri,” amesema Homera.
Amesema hakuna madhara mengine yaliyojitokeza tofauti na hilo, licha ya nyumba nyingi kupata nyufa kutokana na kuta kubomoka.
Kamishina wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Katavi, Regina Kaombwe amewataka wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga na maafa kupitia elimu wanayowapatia.
“Wananchi watumie elimu tunayowafundisha walale uvunguni mwa kitanda na wasimame kwenye nguzo za nyumba pindi wanapoona viashiria vya tetemeko la ardhi, wasitoke nje maana ni hatari,” amesema Regina.
Amina Rajabu ni mkazi wa Majengo Manispaa ya Mpanda amesema tetemeko hilo halijawahi kutokea na limesababisha mshtuko mkubwa.
“Kwa kweli lilikuwa babu kubwa sijawahi kuliona, mimi nilitoka nje nikasahau watoto ndani, cha kushangaza limerudia kama mara tatu ila naamini mwaka huu kutakuwa na mvua ya kutosha,”amesema Amina.
Kamanda wa Jeshi la polisi Mkoa wa Katavi, Benjamini Kuzaga amesema licha ya kutokea tetemeko hilo bado hawajapokea taarifa za madhara yoyote yaliyotokea.
“Limetokea ila Jeshi la polisi hatujapata taarifa za mtu kuripoti kupata madhara yaliyosababishwa na tetemeko hilo,” amesema Kuzaga.