Serikali yaendelea kumkaba koo Lissu kesi ya ubunge wake

Dar es Salaam. Serikali imemuwekea pingamizi la awali mbunge wa zamani wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu katika maombi yake ya kibali cha kukata rufaa kupigania ubunge wake, ikiiomba Mahakama Kuu iyatupe maombi hayo bila kuyasikiliza.

Lissu amefungua maombi hayo jijini Dar es Salaam dhidi ya Spika wa Bunge na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) akiomba kibali cha kukata rufaa katika Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi wa Mahakama Kuu kuhusu suala hilo.

Awali Serikali ilifanikiwa kuishawishi Mahakama Kuu kutupa shauri la awali la mbunge huyo lililofunguliwa na kaka yake, Alute Mughwai aliyekuwa akiomba kibali cha kufungua shauri kutaka amri ya kutengua tangazo la Spika kuwa ubunge wa Lissu umekoma kutokana na utoro na kutojaza fomu za madeni na madili.

Katika uamuzi wake wa Septemba 9, 2019 uliotolewa na Jaji Sirilius Matupa, mahakama ilitupa maombi hayo ikikubaliana na hoja za Serikali kuwa Lissu hakupaswa kufungua maombi ya namna hiyo, bali alipaswa kufungua shauri la kupinga kufanyika kwa uchaguzi mdogo wa kujaza nafasi yake.

Lakini Lissu hakukubaliana na uamuzi wala maelekezo, ndipo akafungua maombi mengine akiomba kibali cha kukata rufaa kupinga uamuzi huo.

Maombi hayo yalipangwa kusikilizwa jana na Jaji Yose Mlyambina, lakini yalikwama baada ya Serikali kuibuka na pingamizi la awali, ikiiomba maombi hayo ya Lissu yatupiliwe mbali, kwa hoja mbili.

Katika hoja hizo, Serikali inadai maombi hayo hayastahili kwa kuwa yanakiuka sheria na kwamba kwa kuwa yako kinyume cha sheria, basi ni ya usumbufu yanayolenga kuharibu taratibu za kimahakama.

Kufuatia pingamizi hilo la awali, mahakama imesimamisha usikilizwaji wa maombi ya Lissu badala yake ikasikiliza kwanza pingamizi hilo la Serikali, huku ikipanga kulitolea uamuzi Aprili 21, mwaka huu.

Uamuzi huo ndio utakaotoa hatima ya maombi hayo ya Lissu, ama kutupiliwa mbali au kuendelea kusikilizwa.

Ikiwa mahakama itakubaliana na pingamizi la Serikali, basi itayatupilia mbali, kinyume chake itayasikiliza maombi hayo na kisha kuyatolea uamuzi ama wa kumpa kibali cha kukata rufaa au kumkatalia.

Wakati wa usikilizaji wa pingamizi hilo, mawakili wa Serikali, Alesia Mbuya na Erigi Rumisha kwa nyakati tofauti waliieleza mahakama kuwa uamuzi ambao Lissu anaombea kibali kuupinga ni uamuzi mdogo, ambao kulingana na amri ya Mahakama Kuu, hauwezi kukatiwa rufaa.

Huku wakirejea uamuzi wa kesi mbalimbali zilizokwishaamuriwa na Mahakama ya Rufani kuhusiana na rufaa dhidi ya uamuzi au amri za mahakama ambazo hazigusii hoja za msingi wa kesi, walisema mahakama hiyo ilishaweka kanuni kuwa uamuzi au amri kama hizo haziwezi kukatiwa rufaa.

“Hivyo, mahakama hii inafungwa na maamuzi haya ya Mahakama ya Rufani,” alisema wakili Mbuya na kusisitiza kuwa tayari mwombaji anazuiliwa kukata rufaa kwa uamuzi kama huo, basi maombi hayo ni ya usumbufu na yanalenga kuharibu mwenendo wa taratibu za mahakama.

Akijibu pingamizi hilo, wakili wa Lissu, Peter Kibatala alisema uamuzi ambao hauwezi kukatiwa rufaa ni ule ambao licha ya kutolewa, shauri la msingi linakuwa linaendelea mahakamani.

Alisema baada ya uamuzi wa Jaji Matupa bila kujali maneno aliyoyatumia wakati anatupilia mbali maombi hayo, hatima yake ulimnyima mteja wake (Lissu) kibali alichokuwa anakiomba na hakuna shauri lingine lililobaki mahakamani.

Wakili Kibatala pia alisema kutupiliwa kwa maombi hayo ni moja ya sababu za rufaa yao kwa kuwa wanaamini uamuzi huo haukuwa sahihi.

Juni 28, 2019, wakati akiahirisha mkutano wa 15 wa Bunge, Spika Job Ndugai alitangaza kukoma kwa ubunge wa Lissu akisema kuwa si yeye aliyemvua ubunge bali ni matakwa ya Katiba.

Ndugai alitaja sababu za uamuzi huo kuwa ni kutokuhudhuria vikao vya Bunge kwa muda mrefu bila kumjulisha Spika kwa maandishi mahali aliko na kutokukutoa taarifa za mali na madeni kwa mujibu wa Sheria ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Baada ya kuvuliwa ubunge, Tume ya uchaguli ilitangaza jimbo kuwa wazi na akachaguliwa mbunge mwingine Miraji Mtaturu (CCM) aliyepita bila kupingwa.