Polisi wapinga aliyechana kitabu cha dini kupewa dhamana, apelekwa mahabusu
Muktasari:
Mahakama ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imemnyima dhamana Daniel Maleki aliyefikishwa katika mahakama hiyo jana Ijumaa Februari 7, 2020 baada ya kuchana kitabu cha dini.
Morogoro. Mahakama ya Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro imemnyima dhamana Daniel Maleki aliyefikishwa katika mahakama hiyo jana Ijumaa Februari 7, 2020 baada ya kuchana kitabu cha dini.
Akizungumza na Mwananchi leo Jumamosi Februari 8, 2020 Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mutafungwa amesema kutokana na kulinda usalama wa mtuhumiwa huyo wameiomba mahakama kuzuia dhamana ombi ambalo limekubaliwa.
Amesema ombi hilo la kuzua dhamana liliwasilishwa mahakamani hapo na polisi chini ya kifungu namba 148 kifungu kidogo cha 5 (d) cha sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai.
Akieleza tukio hilo, Mutafungwa amesema lilitokea saa 8 mchana eneo la Uhindini Wilaya ya Kilosa ambapo Maleki alichana 'Juzuu Amma' ambacho ni kitabu kitakatifu cha dini ya Kiislamu.
Amesema alirudishwa mahabusu katika gereza la Kiberege Wilaya ya Kilombero hadi Februari 20, 2020 kesi hiyo itakapotajwa tena na kwamba upelelezi bado unaendelea.
Jana Maleki alichana kitabu cha dini na picha zake za video kusambaa mitandaoni.
Baada ya kufanya kitendo hicho Waziri wa Tamisemi, Seleman Jafo alimuagiza mkurugenzi mtendaji wa Halmashauri hiyo kumsimamisha kazi.
Katika video hiyo mtumishi huyo anaonekana akichana karatasi na kuzitupa chini, huku sauti zikisikika za watu wanaomtazama kumuuliza sababu za kuchana na yeye kujibu: “Nimeamua tu.”