Pacha waliokuwa wameungana warejea Tanzania

Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Ramadhani Mwinyi (kushoto) na Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mohammed Almarik wakiwa wamewakumbatia mapacha, Marryness na Anosia baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) jana. Mapacha hao walitenganisha katika Hospitali ya Mfalme Abdallah Saudi Arabia hivi karibuni. Watatu kushoto ni Mama wa watoto hao, Jonensia Jovetus. Picha na Anthony Siame

Muktasari:

Watoto pacha waliokuwa wameungana Anisia na Merynes Bernard wamerejea nchini Tanzania kutokea Saudi Arabia walikokuwa wakipatiwa matibabu ya kutenganishwa baada ya kuzaliwa wakiwa wameungana

Dar es Salaam. Mapacha waliokuwa wameungana Anisia na Merynes Bernard wamerejea nchini Tanzania wakitokea Saudi Arabia walikokuwa wamepelekwa kwa ajili ya matibabu.

Mapacha hao walizaliwa Januari 2018 Kyaka, Misenyi mkoani Kagera wakiwa wameungana, walipelekwa Saudi Arabia Julai 8, 2018 baada ya Mfalme Salman kutoa idhini ya kufanyika kwa upasuaji kwa gharama ya Serikali ya Saudia. 

Baada ya kurejea nchini leo Ijumaa Agosti 30,2019 Jonensia Jovitus ambaye ni mama wa mapacha hao sura yake ilionekana yenye nuru na tabasamu ikiwa ni ishara ya kufurahia hali mpya ya watoto wake.

Akizungumza kwa sura yenye tabasamu mara baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Jonensia amewashukuru Watanzania kwa moyo wa kumsaidia hasa katika kipindi cha ujauzito alipokuwa hawezi kufanya kitu chochote.

"Tumbo langu lilikuwa kubwa na sikuweza kufanya lolote lakini kutokana na watu wanaonizunguka walinisaidia hadi kuhakikisha najifungua salama.”

Mama huyo alisema japo watoto hao walikuwa wameungana, “lakini nilimshukuru Mungu na hatimaye leo wametenganishwa."

Akizungumzia operesheni ilivyokuwa, Daktari Bingwa wa upasuaji wa watoto kutoka Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH), Petronia Ngiloi amesema upasuaji huo umefanyika kwa saa 14 chini ya madaktari bingwa 35.

“Upasuaji huu umefanikiwa kwa asilimia kubwa na watoto wote wamerejea wakiwa na afya safi,” amesema

Amesema watoto hao walipozaliwa walikuwa na miguu mitatu ambapo mmoja ulikuwa umeungana lakini baada ya kufanyika uchunguzi ulionekana hauwezi kufanya kazi.

“Mnaweza kusema mmoja angekuwa na miguu miwili mwingine mmoja lakini kwa sababu ulikuwa hauna kazi, ngozi yake ilitumika kuziba sehemu zile ulipofanyika upasuaji,” amesema Dk Ngiloi

Naye Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mohammed El Malik amesema yote yaliyofanyika yanatokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili huku akimshukuru mfalme kwa kuchukua hatua hiyo ya kuwasaidia.