VIDEO: Nukuu za Nyerere zinavyopamba shule ya Tabora Boy’s

Muktasari:
Moja kati ya viongozi waliosoma katika shule hiyo ni Rais wa kwanza wa Tanzania, mwalimu Julius Nyerere ambaye Oktoba 14, 2019 ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu kifo chake.
Tabora. Umewahi kufika Shule ya Sekondari ya wavulana ya Tabora nchini Tanzania.
Tabora Boys ni moja kati ya shule kongwe nchini yenye historia ya kuvutia, inayopambwa na viongozi mbalimbali waliosoma katika shule hiyo.
Moja kati ya viongozi waliosoma katika shule hiyo ni Rais wa kwanza wa Tanzania, mwalimu Julius Nyerere ambaye Oktoba 14, 2019 ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu kifo chake.
Mwananchi limeitembelea shule hiyo katika safari iliyoratibiwa na Wizara ya Elimu.
Mkuu wa Shule hiyo, Deogratius Mwambuzi amesema Mwalimu Nyerere alijiunga na shule hiyo Machi 9, 1937 hadi Desemba 1942 alipohitimu na kwenda kuendelea na masomo yake Chuo Kikuu Makerere nchini Uganda.
Mwambuzi ambaye ni mkuu wa shule hiyo wa 33 tangu ilipoanzishwa amesema, “kumbukumbu zinaonyesha mwalimu Nyerere alisajiliwa namba 590 kwa jina la Kambarage Nyerere na jina la Julius lilikuja baadaye baada ya kubatizwa katika Kanisa Katoliki hapa Tabora.”
Mkuu huyo wa shule amesema wameamua kuweka nukuu za mwalimu Nyerere ili wanafunzi waweze kujifunza na kutambua nini ambacho Baba huyo wa Taifa la Tanzania alikiamini, kukisimamia na alikuwa nani nchini na barani Afrika.
Wanafunzi wa shule hiyo waliozungumza na Mwananchi wamesema nukuu hizo zinawajenga na wanazitumia kufikia malengo yao, wanatamani kuishi katika falsafa za Nyerere.
Katika chumba cha historia ya Tanu, kumesheheni vifaa vya kumbukumbu kama picha, majina ya waliokuwa viongozi mbalimbali wa shule hiyo pamoja na ramani ya Tanzania.
Ramani hiyo inaonyesha alipozaliwa Nyerere, mikoa aliyopita kutangaza falsafa ya ujamaa na kujitegemea pamoja na eneo la Mlima Kilimanjaro ambao Desemba 9, 1961 bendera ya Tanganyika kwa mara ya kwanza.
Mwalimu Nyerere alikuwa Waziri Mkuu wa kwanza wa Tanganyika baada ya kupata Uhuru Desemba 9, 1961 hadi 1962. Mwaka 1963 hadi 1964 alikuwa Rais wa Tanganyika.
Baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar Aprili 26, 1964, Mwalimu Nyerere akawa Rais wa Tanzania kati ya mwaka 1964 hadi 1985.