Nandy avunja ukimya kuhusu Ruge Mutahaba

Muktasari:
Baada ya kimya cha muda mrefu tangu kitokee kifo cha Mkurugenzi wa Vipindi na uzalishaji wa Clouds Media Group Ruge Mutahaba, mwanamuziki Nandy ameeleza hisia zake
Dar es Salaam. Mwanamuziki Nandy ‘African Princess’ amevunja ukimya na kumzunguzia Ruge Mutahaba kwa kuandika ujumbe katika ukurasa wake wa Instagram akimuelezea alivyomfahamu.
Msanii huyo kipindi chote cha msiba aligusa hisia za wengi kutokana na namna alivyoonekana wakati wote akiwa sehemu ya familia ya Ruge jambo lililoibua maswali kuhusu uhusiano wake na marehemu.
Katika ujumbe wake Nandy amemuelezea Ruge kama rafiki yake wa karibu aliyeelewa ndoto zake na kumpa moyo wa kupambana.
Ujumbe huo uliokwenda sambamba na video inayomuonyesha Ruge akicheza na mbwa unasomeka: “ Kila mtu ana mtu ambaye ameumbwa na Mungu kwa ajili yake, jinsi ya kukutana na huyo mtu inaweza ikawa safari ni ndefu, ikawa na matuta na mara nyingine inaweza ikachosha lakini mwisho wa siku kila kitu kinakuja kuwa sawa.
“Wanaweza kutokea wachache ambao watakuelewa na pia kuelewa ndoto zako hata kama unazifanya mwenyewe. Watanzania wanakupenda umegusa maisha yao kwa namna tofauti ulizaliwa kuwa kiongozi, ulikuwa na moyo wa kutoa.”
Ameendelea kumuelezea Ruge akisema: Ulikuwa rafiki yangu wa karibu sana, ulikuwa kila kitu kwangu. Ruge ulielewa ndoto yangu na ulinipa moyo wa kupambana hata kama nilikuwa nataka kukata tamaa.”
“Nakuhakikishia nitakufanya ujivunie, nitaendelea kuzienzi na kuziishi hekima zako na nitafanya juhudi kufikia malengo tuliyopanga pamoja. Nakupenda sana na nitaendelea kukupenda hata kama haupo nasi.”