VIDEO: Nancy Sumari: Ni muhimu watoto kutambua haki zao

Muktasari:
Nancy Sumari, mlimbwende wa Tanzania mwaka 2005 ameandika kitabu cha Haki kinachoelezea sheria ya mtoto ya mwaka 2009, akiwa na lengo la kuwakinga watoto na vitendo vya ukatili kwa kuzitambua haki zinazowalinda.
Dar es Salaam. Mlimbwende wa Tanzania mwaka 2005, Nancy Sumari amesema kuna umuhimu wa kuwafundisha watoto kutambua haki zao.
Amesema jambo hilo litawasaidia kujilinda na kukabiliana na unyanyasaji dhidi yao aliodai kuwa siku za hivi karibuni umeshika kasi.
Nancy mwenye shahada ya usimamizi wa biashara ameeleza hayo katika mahojiano maalum na Mwananchi Digital wakati akitambulisha kitabu chake cha Haki kinachoelezea masuala mbalimbali ya haki za watoto.
“Nimesukumwa kuandika kitabu baada ya kuona matukio ya unyanyasaji kwa watoto yanakithiri, huku wengi wao wakiwa hawatambui haki zao.”
“Kupitia kitabu hicho nimerahisisha kwa kuianisha sheria ya mtoto ya mwaka 2009, lengo ni kuhakikisha wanatambua haki zao, ”amesema Nancy.
Mkurugenzi huyo wa Blogu ya Bongo5 amesema, “hata mwanangu Zuri alipokisoma kitabu hiki aliniambia yeye alikuwa anajua haki ni kwa ajili ya watu wazima, hii inaonyesha watoto wengi hawalitambui hili.”
Amefafanua kuwa kitabu hicho kimeandikwa kwa lugha ya Kiswahili na kina michoro na picha kwa ajili ya kuwavutia watoto kusoma.
Mrembo huyo mwenye umri wa miaka 33 licha ya kuwa mjasiriamali pia ni Mkurugenzi wa Jenga Hub, taasisi inayotoa mafunzo ya matumizi ya vifaa vya teknolojia pamoja na ujuzi wa kompyuta kwa programu za watoto wa miaka saba hadi 12.
Mbali ya kitabu hicho, ameandika kingine 'Nyota Yako' alichokitoa mwaka 2013 kinachozungumzia wanawake waliofanya mambo makubwa katika nyanja mbalimbali nchini.
"Ninaamini utaratibu huu wa kuandika vitabu ipo siku na mimi nitaandika kitabu kuhusu maisha yangu kama alivyofanya Rais wetu mstaafu Benjamin Mkapa.”
“Kwa namna nilivyokisoma kina mengi ya kujifunza ninaamini kila historia ya mtu kwenye maisha yake ina mafunzo kwa watu wengine," amesema.
Nancy ametoa wito kwa taasisi mbalimbali kuendelea kuelimisha jamii kuhusu masuala ya haki na kuongeza kuwa kukosekana elimu ndio huchangia kuwatendea watoto ukatili wa kijinsia na kuwanyima haki zao.