NEC yatangaza kuhamia Dodoma

Muktasari:

Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk Wilson Charles amesema shughuli za uchaguzi mwaka 2020 zitafanyikia Dodoma baada ya ofisi hiyo kuhamia makao makuu hayo ya nchi.

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) nchini Tanzania imetangaza kuhamishia ofisi zake jijini Dodoma kutoka Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa NEC, DK Wilson Charles amesema mwaka 2020 ni mwaka wa uchaguzi, mambo yote yanayohusu uchaguzi yatafanyikia Dodoma.

Taarifa iliyotolewa na NEC leo Jumanne Januari 7, 2020 imemnukuu Dk Mahera akisema hayo mara baada ya kufanya ziara kwenye eneo la Njedengwa, jijini Dodoma zinapojengwa ofisi za tume hiyo na kujionea maendeleo ya ujenzi ambao unafanywa na Shirika la Uzalishaji Mali la Jeshi la Kujenga Taifa (Suma JKT).

Dk Charles amesema JKT ambao walikabidhiwa mradi huo baada ya Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) kushindwa kukamilisha mradi kwa wakati uliopangwa, wameihakikishia NEC mradi huo utakamilika Aprili 2020.

“Mkandarasi wa kwanza alikuwa TBA, baada ya kuwa ameondolewa imetuchukua kama mwezi mzima kuweka utaratibu wa kuandaa michoro upya kwa sababu michoro ilikuwa imekosewa sana.”

“Kwa ushirikiano wa Chuo cha Ardhi na Suma JKT kazi imeanza na inaenda kwa kasi kubwa,” amesema Dk Charles

Dk Charels amesema Suma JKT imeweka vijana zaidi 300 kwenye eneo hilo la ujenzi na tume tayari imelipatia shirika hilo malipo ya awali kwa ajili ya kazi hiyo.

“Sisi tumeshawapatia malipo ya awali na kazi imeanza kwa kasi kubwa, kwa pamoja majengo yote matatu yaani ghala, jengo la kutangazia matokeo na ofisi hii yenye ghorofa nane vyote vitaendelea kwa wakati mmoja,” amesema Dk Charles

Amesema Mkuu wa Jeshi la Kujenga Taifa, Brigedia Jenerali Charles Mbuge amemhakikishia itakapofika Aprili 2020 mradi huo utakuwa umefikia hatua nzuri sana.

Kwa upande wake, Lazaro Masanja ambaye ni mhandisi miradi wa Suma JKT amesema nguvu kazi ya vijana 300 iliyowekwa na jeshi hilo kwenye mradi huo inaashiria jeshi lipo makini kuhakikisha unakamilika mapema iwezekanavyo.

“Kama ilivyo kauli mbiu ya mkuu wa JKT ‘Jeshi halishindwi’ kwa hiyo sisi matarajio yetu ni kwamba mwezi wa nne tutakuwa aidha tumekabidhi au tuko kwenye maandalizi ya kukabidhi kazi hii,” amesema.