Miaka miwili bila Azory Gwanda

Muktasari:

Leo inatimia miaka miwili kamili tangu mwandishi wa habari, Azory Gwanda atoweke katika mazingira ya kutatanisha.


Dar es Salaam. Leo inatimia miaka miwili kamili tangu mwandishi wa habari, Azory Gwanda atoweke katika mazingira ya kutatanisha.

Katika kuadhimisha kumbukumbu yake, Kampuni ya Mwananchi Communications Ltd imepanga kupanda mti na kuzindua picha maalumu kama ishara ya heshima na utambuzi wa mchango wa mwandishi huyo katika tasnia ya habari nchini.

Gwanda anasadikika kuchukuliwa na watu wasiojulikana wakati matukio ya mauaji yalipokuwa yakitokea mara kwa mara katika wilaya ya Kibiti mkoani Pwani.

Alikuwa akiandika habari hizo wakati taarifa za kutoweka kwake zilipoibuka mara ya kwanza. Habari hizo zilikuwa zikichapishwa katika matoleo kadhaa ya magazeti ya The Citizen na Mwananchi. Tangu kutoweka kwake, hakuna kinachojulikana kuhusiana na hatima ya kupatikana kwake.

Serikali imekuwa ikisema inachunguza anapoweza kuwepo pamoja na matukio ya watu wengine yanayofanana na ya Gwanda, hadi sasa hakujawa na matokeo yoyote yanayoweza kusaidia kupatikana kwake.

Katika siku za karibuni kumekuwa na matamko mbalimbali kutoka kwa wanaharakati wa haki za binadamu, waandishi wa habari na mashirika yao ikiwamo Kamati ya Kulinda Waandishi wa Habari (CPJ) kuitaka Serikali kulipa kipaumbele tatizo la kutoweka kwa Gwanda huku kampeni kama vile #MrudisheniAzory zikiendelea kwenye mitandao ya kijamii.

Mwaka jana, Gwanda alishinda Tuzo ya Daudi Mwangosi kama hatua ya kutambua mchango wake katika tasnia ya habari nchini. Tuzo hiyo huandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania kama kumbukumbu ya mwandishi wa habari Daudi Mwangosi ambaye aliuawa na polisi wakati wa maandamano yaliyotokea Iringa, Septemba 2012.

Mei mwaka huu, jina la Gwanda lilikuwamo katika orodha ya “Kesi 10 Muhimu” za waandishi wa habari duniani kote zilizokusanywa na shirika la One Free Press Coalition, ambalo ni mjumuiko wa wahariri mashuhuri 30 wa vyombo vya habari vya Reuters, Quartz, The Financial Times, India Today, TIME, Washington Post na vyombo vingine. Wahariri hao hutumia ushawishi wao kuwatetea waandishi waliofikwa na majanga mbalimbali wakati wa kutekeleza majukumu yao.

Katika mahojiano yake na BBC, katika kipindi cha ‘Focus on Africa’, Waziri wa Mambo ya Nje, Profesa Palamagamba Kabudi alisema Gwanda alikuwa amepotea na kuuawa katika wilaya ya Rufiji, akiongeza kwamba serikali imeweza kudhibiti ugaidi katika eneo hilo.

Hata hivyo, baadaye Profesa Kabudi alikanusha taarifa kwamba amethibitisha kifo cha Gwanda badala yake alisema kwamba watu hawakuelewa vizuri kile alichokisema.

Alisema kwamba alichokuwa anamaanisha ni kwamba kilichojitokeza mkoani huko ni kitu kibaya kuwahi kutokea na kilipelekea watu wengi kupotea na hata wengine kuuawa.