Mbabe wa Idi Amin Uganda atimiza miaka 100 Tanzania

Mkuu wa Majeshi mstaafu Jenerali David Msuguri akiwa katika Misa ya kutimiza Miaka 100,Nyumbani kwake Wilaya Butiama Mkoani Mara. Picha na Johari Shani
Muktasari:
Mkuu wa majeshi mstaafu nchini Tanzania, Jenerali David Msuguli aliyezaliwa Januari 4, 1920 leo Jumamosi anasherehekea miaka 100 ya kuzaliwa katika hafla ya kifamilia na kidini inayofanyika nyumbani kwake kijiji cha Butiama mkoani Mara.
Butiama. Mkuu wa Majeshi mstaafu nchini Tanzania, Jenerali David Musuguri maarufu ‘Chakaza’ ametimiza umri wa karne moja tangu alipozaliwa Januari 4, 1920.
Hafla ya kuadhimisha miaka 100 ya Jenerali Msuguli zinafanyika leo Jumamosi Januari 4, 2020 nyumbani kwake kijiji cha Butiama mkoani Mara kwa ibada maalum inayoongozwa na Askofu wa Jimbo Katoliki la Musoma, Michael Msonganzila.
Mmoja wa wana familia, Bahame Nyanduga amesema pamoja na ibada, maadhimisho hayo pia yatahusisha shughuli na sherehe za kifamilia.
Pamoja na ngazi mbalimbali za kijeshi, Jenerali Msuguri alikuwa Mkuu wa Majeshi kati ya mwaka 1980 hadi 1988.
Ibada ya shukrani inayofanyika nyumbani kwa mkuu huyo wa jeshi mstaafu imehudhuriwa na viongozi kadhaa wakiongozwa na mbunge wa Musoma vijijini (CCM), Profesa Sospeter Muhongo.
Wakati wa vita ya Kagera, Jenerali Musuguri aliongoza vikosi vya Tanzania kumpiga aliyekuwa Rais wa Uganda, Idd Amin Dada mwaka 1979.
Katika moja ya mahojiano yake, Jenerali Msuguri aliwahi kusema alichukizwa na unyama ambao Idd Amin alikuwa anaufanya na angetokea akamkamata angemchinja.
Msingi wa viti hiyo ilitokana na Idd Amin kuuvamia mkoa wa Kagera Novemba 1978 hali ambayo rais wa wakati huo, Mwalimu Nyerere hakukubaliana nao na kutangaza kumpiga na kumwondoa.
Katika uvamizi huo uliofanywa na Idd Amin alishusha bendera ya Tanzania kuamua kupandisha bendera ya Uganda huku Watanzania ambao hawakuwa na hatia wakubwa kwa wadogo waliuawa na wengine kupata vilema vya kudumu.
Katika moja ya mahojiano aliyowahi kuwafanya Jenerali Msuguri alisema kwenye uwanja wa vita majeshi ya Idd Amin yalipigwa na majeshi ya Tanzania na kusababisha Idd Amin kukimbilia Libya kuomba hifadhi baada ya kuzidiwa
Endelea kufuatilia Mwananchi kwa habari zaidi