Magufuli awasili kikao cha kamati kuu CCM

Muktasari:

Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli leo asubuhi Jumatano Februari 12, 2020 amewasili katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam  kushiriki kikao cha kamati kuu.

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli leo asubuhi Jumatano Februari 12, 2020 amewasili katika ofisi ndogo za chama hicho zilizopo mtaa wa Lumumba, Dar es Salaam  kushiriki kikao cha kamati kuu.

Ulinzi kuanzia mwanzo hadi mwisho wa mtaa huo zimeimarishwa , huku barabara inayopita mbele ya ofisi hizo ikifungwa na kusababisha magari kutumia njia nyingine kwenda na kuingia katikati ya jiji na maeneo mbalimbali.

Magufuli aliwasili katika ofisi hizo saa 4:15 asubuhi muda mfupi baada ya kuwasili  Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein.

Nini kitajiri kamati kuu

Kamati kuu inakutana ikiwa ni siku chache baada ya kamati ndogo ya usalama na maadili kuwahoji makada watatu kwa kukiuka maadili.

Wapo wanaotegemea kuwa vigogo hao wataadhibiwa na wapo wanaoamini kuwa CCM inamaliza mambo yake kwa maridhiano na hivyo hawataadhibiwa.

Bernard Membe, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na mmoja wa makada 38 walioomba ridhaa ya kugombea urais, Abdulrahman Kinana na Yusuf Makamba, waliokuwa makatibu wakuu wa CCM katika kipindi cha miaka kumi ya Serikali ya Awamu ya Nne, walihojiwa kwa kukiuka maadili ya chama hicho Alhamisi na Jumatatu.

Kinana na Makamba walikiandikia chama hicho barua ya kulalamika kutolindwa kuchafuliwa na mtu ambaye anajiita mwanaharakati wa Serikali ya Awamu ya Tano na kutuhumu kuwa mtu huyo analindwa na watu wenye mamlaka.

Baadaye sauti zao pamoja na ya Membe na makada wengine watatu zilisambaa mitandaoni zikizungumzia barua hiyo na kulaumu uongozi kuwa unasababisha chama kupoteza mvuto na hivyo kuitwa mbele ya kamati hiyo ndogo ambayo imeshamaliza kuwahoji.

Licha ya Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally na wa uenezi, Humphrey Polepole kutopatikana kueleza kitakachojadiliwa katika kikao cha Kamati Kuu, kutokana na uzito wa suala hilo kuna uwezekano mkubwa wa kulijadili.

Endelea kufuatilia Mwananchi kwa taarifa zaidi