Kamati za Bunge Tanzania kuchambua ripoti ya CAG, marekebisho ya sheria

Muktasari:

Kamati za Bunge zitaanza kukutana kuanzia Agosti 19 hadi Septemba 2, 2019 jijini Dodoma zikifanya uchambuzi wa miswada ya sheria, kupokea taarifa mbalimbali, uchambuzi wa taarifa ya Mdhibiti na mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG, sheria ndogo na taarifa ya uwekezaji wa mitaji ya umma.

Dar es Salaam. Kamati za Bunge nchini Tanzania zitaanza kukutana kuanzia Agosti 19 hadi Septemba 2, 2019 jijini Dodoma zikifanya uchambuzi wa miswada ya sheria, kupokea taarifa mbalimbali, uchambuzi wa taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG, sheria ndogo na taarifa ya uwekezaji wa mitaji ya umma.

 Spika wa Bunge, Job Ndugai leo Ijumaa Agosti 16,2019  amezitaka Kamati hizo kukutana kabla ya kuanza kwa mkutano wa 16 wa Bunge uliopangwa kuanza  Septemba 3, 2019 kwa mujibu wa Kanuni ya 117 (5) ya Kanuni za Kudumu za Bunge hilo.       

Taarifa iliyotolewa na kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha Ofisi ya Bunge imetaja shughuli zilizopangwa kutekelezwa na kamati hizo ni pamoja na uchambuzi wa miswada ya sheria ambapo miswada mitatu ya sheria inatarajiwa kujadiliwa na kamati mbili zilizopelekewa miswada hiyo kwa mujibu wa Kanuni ya 84(1). 

 

Taarifa hiyo imezitaja kamati na miswada hiyo kuwa pamoja na kamati ya utawala na serikali za mitaa itakayochambua na kujadili ‘Muswada wa Sheria ya Serikali Mtandao wa Mwaka 2019’.

 

Kamati ya Katiba na Sheria itachambua na kujadili miswada miwili ambayo ni ‘Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.4) wa Mwaka 2019’ [The Written Laws (Miscellaneous Amendments) (No. 4) Bill, 2019]; na ‘Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria Mbalimbali (Na.5) wa Mwaka 2019,” imesema taarifa hiyo.

 

Taarifa hiyo pia imetaja shughuli ya kupokea taarifa mbalimbali za wizara na taasisi ambapo kamati tisa za sekta na Kamati ya Bajeti zitachambua taarifa za taasisi na Wizara za Serikali kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali kwa mujibu wa Kifungu cha 7(1), kifungu cha 7(2) (i) (ii) (iii) na (iv) na Kifungu cha 9(a) vya Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Bunge. 

Kuhusu uchambuzi wa taarifa hiyo imesema kamati zinazosimamia matumizi ya fedha za umma ambazo ni Kamati ya Hesabu za Serikali (PAC) na Kamati ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) zitachambua Taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha unaoishia  Juni 30, 2018.

 

“Kamati ya Bunge ya Sheria Ndogo itachambua sheria ndogo  zilizowasilishwa bungeni wakati wa Mkutano wa 15 wa Bunge. Madhumuni ni kutekeleza majukumu yake yaliyoainishwa katika Kifungu cha 11 cha nyongeza ya nane ya Kanuni za Bunge,” imesema taarifa hiyo.”

 

Shughuli nyingine iliyotajwa ni uchambuzi wa taarifa za uwekezaji wa mitaji ya umma ambapo Kamati ya Uwekezaji wa Mitaji ya Umma (PIC) itachambua Taarifa ya Uwekezaji wa taasisi/mashirika saba kwa mujibu wa Kifungu cha 12 (a) (b) cha Nyongeza ya Nane ya Kanuni za Kudumu za Bunge.