Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Hotuba ya Mwalimu Nyerere: Hatuwezi kuendelea kupuuza Katiba

Muktasari:

Machi 14, 1995, Mwalimu Nyerere alizungumza na wanahabari kwenye ukumbi wa Tanzania Room Hoteli ya Kilimanjaro, Dar es Salaam na kusema kuwa ingawa haiwezekani kumpata Rais asiye na kabila, hatutamkataa mtu kwa sababu ya kabila lake, wala hatutamchagua mtu kwa sababu ya kabila lake. Aliasa pia kuepukana na udini. Ungana na mwandishi William Shao katika hotuba hiyo...

Sasa hapa katikati kumetokea na kupuuza puuza Katiba. Ufa wetu wa pili. Hatuwezi kuendelea kupuuza Katiba. Katiba ndiyo sheria ya msingi. Sheria nyingine zoooote zinatokana na Katiba. Haiwezi kupuuzwa.

Hatuwezi kuendelea na utaratibu wa kupuuza Katiba ya nchi yetu. Au kuwa na Rais anayeona haya kuitetea Katiba. Naye amechaguliwa kwa mujibu wa Katiba hiyo ameapa kuilinda Katiba hiyo halafu anaona haya kuitetea Katiba hiyo.

Mtu ambaye hawezi kuitetea Katiba ya nchi yetu hawezi kuilinda hawezi kuisimamia baada ya kiapo hatufai (vifijo). Hafai. Aende akaendeleze shamba lake huko. Hawezi kuwa Rais wa nchi yetu.

Tunamchagua kwa mujibu wa Katiba, tunamwapisha kwa Katiba, ailinde, aitetee kwa moyo thabiti kabisa bila woga. Hawezi, hatumtaki … anaweza kuwa rafiki yetu sana. Anaweza kuwa kabla hajafika kwenye vikao vyetu hatuanzi kwa kunywa chai au brand (kilevi), lakini hiyo ni shauri nyingine, lakini kwa urais wa nchi hatufai.

Tumeuona ufa huo wa kutojali Katiba. Ufa wa tatu unafuatana kabisa. Nchi zote duniani zinaongozwa na watu. Mimi niliwahi kupata heshima ya kuiongoza nchi hii. Sasa leo Rais Mwinyi anaiongoza. Na sasa tunazungumza kuona ni nani baadaye … tutazungumza nani anafaa anatarajiwa kuongoza. Nchi zinaongozwa na watu, kumbe zitaongozwa na nani? Hatuna malaika, hatuna eh, … ndiyo alivyotaka Mwenyezi Mungu nchi hizi tuziongoze wenyewe. Sisi hawa hawa.

Lakini haziongozwi kutokana na akili za mtu. Zinaongozwa kutokana na sheria. Ni kweli nchi zinaongozwa na watu, lakini hao watu wanaongozwa na sheria.

Watu ni muhimu. Lazima kuwe na viongozi imara ndio maana nazungumza, ndio maana tunazungumza, ndio maana niko hapa nazungumza habari ya kupata viongozi imara. Lakini wanaongozwa na sheria.

Haiwezekani mtu ana-anapata ushauri kwa mkewe tu kesho tunakuta jambo fulani limetokea … (kicheko toka kwa waandishi). Huko kucheka kunaonyesha kwamba umuhimu wa sheria mnaelewa (kicheko zaidi). Hamwezi kutawaliwa … hata hamjui, maana hata hamjui kesho mkewe atamwambia nini (kicheko zaidi).

Nimesema tunataka Rais anayejua kwamba Muungano wetu umetikiswa, na hiyo inamkera. Anakerwa na hiyo. Na kwamba tukimpata kazi yake moja ni kusimamia hilo. Tunataka Rais wetu anayejua tumechezea chezea Katiba kidogo. Na hiyo inamkera. Akipata nafasi, akipewa nafasi na wananchi wenzake atalisimamia hili la kucheza- cheza na Katiba.

Tumeona utaratibu, sheria za nchi hazi … — watu wanajaribu kuendesha nchi bila kujali sheria za nchi. Kuendesha tu mambo bila kujali sheria. Tunataka mtu wa kuwa kiongozi wetu ambaye hiyo inamkera. Huwezi kuendesha nchi bila utaratibu wa sheria, watu hawatajua kesho kutatokea nini. Na watu wanataka wajue. Wanakaa katika majumba yao wanajua wanatawaliwa na sheria kwa hiyo hawana wasiwasi.

Zamani tulikuwa na kitu kinaitwa miiko ya uongozi. Zingine zilikuwa, wakati wa Tanu, ziko zinaitwa kanuni tu za Tanu. Na kanuni moja ya Tanu, ambayo baadaye tukairithi katika CCM, au tukairithisha CCM, inasema ‘rushwa ni adui wa haki. Sitatoa wala sitapokea rushwa.’

Msije mkadhani kwamba wakati wa awamu ya kwanza palikuwa hapana rushwa. Ilikuwapo. Lakini tulikuwa wakali. Tulikuwa wakali sana. Siku za mwanzo kabisa kabisa tulitaka watu wajue hivyo. Tulitaka wajue kwamba tutakuwa wakali sana na wala rushwa ndani ya serikali au na watoa rushwa. Mwanzo kabisa … tulitaka kila mtu ajue.

Tukapitisha sheria kwamba mtu akila rushwa … aliyetoa, aliyepokea, Wazanaki wanasema “wote mazanyanga, wote mazanyanga (kicheko), wote watapata msukosuko. Hatukuwa tunatania.

Kwa hiyo tukatengeneza sheria ili tuwafundishe watu hawa kuwa jambo hili hatulipendi, akiishakuthibitika mahakamani kwamba kala rushwa, akiisha kuthibitika mahakamani kwamba katoa rushwa, hatukumwachia hakimu uamuzi wa adhabu.

Tukasema atakwenda ndani muda usiopungua miaka miwili. Atapata viboko 24. 12 siku anaingia, 12 siku anatoka akamwonyeshe mkewe (kicheko kirefu). Wengine wadogo hamjui ninyi. Hamjui.

Basi tukapata habari waziri wetu wa Sheria amehongwa. Hatukuwa na utani hata kidogo. Tukapata habari waziri wetu wa Sheria amehongwa. Tukampata aliyemhonga, akakiri kwamba amemhonga. Akaingia ndani akapata vile viboko vyake.

Lakini ndiyo siku zetu za mwanzo zile tunataka kuwaonyesha hawa wakubwa kwamba we don’t need disturbance (hatutaki usumbufu). Lakini kuna mahakimu, mahakimu wetu wakati ule Waingereza unajua mahakimu … …

Hawaipendi sheria ile. Hawaipendi sheria ile hata kidogo. Kwanza inawalazimisha adhabu. Hawaipendi sheria inayowatamkia adhabu kwamba wao hawana hiari. Akishasema huyu amekosa basi, hakuna tena kusema sema tumpe adhabu gani. Imetamkwa ndani ya sheria. Hawapendi kabisa sheria hiyo kwa sababu hiyo ya kuwalazimishia adhabu.

Pili, hawapendi mtu kutandikwa. Hata mimi nilikuwa sipendi kutandikwa. Lakini nilikuwa zaidi … rushwa nilikuwa nachukia zaidi kuliko kumtandika mtu.

Rushwa ni adui wa haki. Ukishakuwa mla rushwa watu maskini hawana kitu. Serikali lazima itishe wala rushwa. Kwa hiyo mimi sipendi kumtandika mtu, lakini rushwa nachukia zaidi.

Kwa hiyo tukapitisha sheria. Majaji hawa Waingereza hawapendi. Nasema kwanza hawapendi tumewawekea adhabu ambayo wao hawana hiari nayo, pili, ni kutandika na hawapendi kutandika, tatu wanamheshimu sana mheshimiwa yule aliyehongwa.

Basi wakatafuta tafuta njia wakamwachia. Pamoja na kwamba wamemfunga aliyemhonga, huyu wakatafuta njia njia wakamwachia kwa sababu sheria na haki ni vitu viwili mbalimbali, siyo! Nautoa mfano huo kuwaambieni tulikuwa very serious (makini sana).

Safari moja Mgiriki mmoja alipita pita humu anajitapatapa ooh, anasema mimi serikali yote ya Tanzania iko mfukoni mwangu. Nikasema mshenzi sana huyu, loh! Serikali yote ya Tanzania iko … , ana mfuko mpana kiasi gani (kicheko).

Sasa mniwie radhi. Mniwie radhi, ingawa nasema lazima kuendesha nchi kwa mujibu wa sheria. Nikaona huyu mshenzi anasema hivi? Nikajua anahonga watu. Hawezi kusema hivyo bila kuwa anahonga watu. Lakini ni vigumu sana kumpata.

Nikaona lakini hata hivyo nitamfundisha tu. Nikamtia ndani. Nikamtia ndani. Nikatiwa msukosuko hapa nikatiwa msukosuko hapa Mwalimu mwachie nikawaambia simwachii hana adabu.

Mzee Kenyatta akaniletea ujumbe bwana huyu mtu tunamfahamu mwachie nikamwambia simwachii hata kidogo. Simwachii. Siwezi kumwachia hana adabu anasema serikali yangu yote iko mfukoni mwake (kicheko). Simwachii hata kidogo. Nikamwambia yule mama aliyetumwa na Kenyatta nikamwambia nenda kamwambie Mzee namheshmu sana lakini huyu hatoki. Siku moja niko Msasani pale nikaambiwa anakuja … kuna ujumbe anakuja Baba Askofu kuja kukuona.

Anatoka wapi? Anatoka Kenya. Akaja. Baba Askofu wa Greek Orthodoxy … Akaja Msasani kwangu pale. Akaniambia bwana ana ujumbe wangu. Nikamwambia njoo twende katika kijumba … pale Msasani nina kachumba kangu kadogo akanipa barua. Naisoma barua inatoka kwa Baba Askofu Makarios. Mwalimu tafadhali umwachie huyu mtu.

Basi nikamwambia Baba Askofu, tazama Baba Askofu, huyu mtu mshenzi. Nadhani hata ninyi mnajua kwamba ni mshenzi. Sasa wamenifata watu wengi, pamoja na kaka yangu kwa sababu kaka yangu alikuwa na marafiki zake Wagiriki wakanifatafata hapa Krismasi wakajazana tele hapa. Nikamwambia kaka yangu wacha … Wahuni hawa mimi sikubali.

Nikamwambia wamenifata watu wengi … nimekataa, pamoja na mkewe kanifata nikamwambia siwezi kumwachia mumeo mtu wa ovyo. Sasa Baba wewe umekuja eh Baba Askofu. Barua yenyewe ya Baba Askofu Makarios. Sasa siwezi kukupeleka mikono mitupu.

Mpelekee habari Baba Askofu Makarios mwambie hivi: Mwalimu yuko tayari kumwachia. Lakini mumhamishe East Africa arudi Cyprus akae asionekane tena East Africa. Nikaletewa assurance (uthibitisho) kutoka kwa Baba Askofu nikamheshimu nikamwachia. Sijui kama aliwahi … sikupata kumsikia tena.

Nawaambieni hadithi hiyo kwamba hatukuwa na utani utani juu ya mambo haya. Juu ya rushwa hatukuwa na utani na mtu. Rushwa ni jambo hatari kabisa.

Itaendelea kesho...