Halmashauri ya Momba taabani, Jafo ampa maagizo RC

Waziri wa Nchi Ofisi Rais Tamisemi, Seleiman Jafo

Muktasari:

Halmashauri ya wilaya ya Momba mkoani Songwe itawekwa katika uangalizi maalumu ili iweze kufanya vizuri huku mkuu wa mkoa huo akipewa maagizo ya kuhakikisha anaisimamia halmashauri hiyo.

Momba. Halmashauri ya Wilaya Momba mkoani Songwe nchini Tanzania, imewekwa katika uangalizi maalumu ili kuinusuru iweze kujisimamia na kujiendesha.

Uamuzi huo umetolewa leo Jumatatu Desemba 16, 2019 na Waziri wa Nchi Ofisi Rais Tamisemi, Seleiman Jafo wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri hiyo mjini Chitete kuwa ina hali mbaya inayotishia kuweza kujiendesha.

Amesema halmashauri hiyo inafanya vibaya katika maeneo yote, ikiwa ni pamoja na usimamizi wa miradi, ushirikiano baina ya wafanyakazi haupo na ukusanyaji wa mapato ya ndani ambapo hadi sasa imekusanya Sh320 milioni sawa na asilimia 24 ya lengo lililowekwa.

Jafo amesema kufuatia hali hiyo ofisi yake itatoa mashine 30 za kukusanyia mapato ili zisaidie kukusanyia mapato ili ipate uwezo wa kujiendesha na kumtaka mkuu wa mkoa wa Songwe (RC), Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela kuwa karibu zaidi na halmashauri hiyo.

Waziri Jafo ameonya mtindo wa matumizi ya fedha za umma bila kupitia benki aliouita ni matumizi ya fedha mbichi hali ambayo inaidhoofisha zaidi halmashauri ya Momba ambayo ina hali mbaya.

Waziri huyo yuko katika ziara ya kikazi ya siku moja ambapo tayari ametembelea halmashauri ya Momba na kukagua ujenzi wa Soko la kimataifa la mazao Kakozi na kuzungumza na watendaji kisha kukagua mradi wa ujenzi wa Ofisi ya mkuu wa mkoa Songwe kisha ataelekea halmashauri ya wilaya Ileje.