Engen yaendelea kujiimarisha Kanda ya Ziwa

Muktasari:

Mwanza ni mji ambao ni mhimu kwa biashara katika Kanda ya Ziwa  na nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda, ndio maana kampuni nyingi kama Engen zimeendelea kuwekeza katika jiji hilo maarufu kama Rock City.

Mwanza. Mwanza ni mji ambao ni muhimu kwa biashara katika Kanda ya Ziwa  na nchi jirani za Kenya, Uganda na Rwanda, ndio maana kampuni nyingi kama Engen zimeendelea kuwekeza katika jiji hilo maarufu kama Rock City.

Kampuni ya mafuta ya Engen Petroleum (T) Limited, imekuwa ikifanya kazi nchini Tanzania kwa zaidi ya miaka 20 kitu ambacho kimeifanya iwe kampuni yenye mafanikiyo na yenye ubunifu ambayo hutoa bidhaa bora za mafuta.

Jana wakati akifungua vituo viwili Jijini Mwanza, Mkurugenzi Mtendaji wa Engen, Bwana Paul Muhato aliuhakikishia umma juu ya kuendelea kuwepo kwenye soko sanjari na ukuaji wa uchumi nchini wakianzia na jiji la Mwanza katika mikoa iliyopo Kanda ya Ziwa.

“Uamuzi huo wa kuongeza vituo katika mikoa mbalimbali nchini  ni hatua mojawapo katika mpango wa ukuaji wa kampuni kwa sasa.  Tunaendelea kuangalia maeneo ya kimkakati nchini kote kwa ajili ya maendeleo na ununuzi wa vituo vya rejareja ili kutumikia vyema soko la Tanzania,” alisema Bw Muhato

Kwa sasa Engen ina vituo 10 vinavyopatikana katika mikoa ya Dar es Salaam, Morogoro, Dodoma, Tanga, Moshi, Arusha na Mwanza.

“Lakini idadi hii itaongezeka katika kipindi cha miaka michache ijayo”,   alisema Bw Muhato alipokuwa  akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa vituo viwili vya Mafuta katika jiji la Mwanza.

Mjini Mwanza vimefunguliwa vituo vipya viwili ambacho kimoja kipo maeneo ya Sinai na kingine kinapatikana Mkuyuni.

"Tukiwa tunakusudia kuweka mteja kama kipaumbele cha kwanza, tunatarajia angalau vituo 4 zaidi katika maeneo ya kimkakati ili kuhakikisha wateja wetu wanapata huduma za kiwango cha juu kwa muda wote.”

Anasema kwamba wataendelea kusisitiza umuhimu wa kuwa na mafuta bora na mafuta yanayotolewa na wahudumu waliofundishwa vizuri wakitoa huduma kwa masaa 24 kila siku.

“Wateja pia watafurahia huduma zingine kadhaa kama vile maduka, migahawa ya hali ya juu, Sehemu ya matengenezo ya magari, mahali pa kuosha gari na huduma zingine, zote zikiwa chini ya paa moja. "Alihitimisha Bw Muhato.