Bugando yaokoa Sh2 bilioni kwa matibabu ya saratani

Muktasari:

  • Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) jijini Dar es Salaam nchini Tanzania imefanikiwa kuokoa zaidi ya Sh2 bilioni kwa wananchi wa kanda ya ziwa kusafiri kwenda jijini Dar es Salaam kupata matibabu ya saratani kila mwaka, tangu kusimikwa kwa mitambo ya kutoa tiba ya mionzi.


Dar es Salaam. Kununuliwa kwa mashine nne za mionzi, kumeiwezesha Hospitali ya Rufaa ya Kanda ya Bugando (BMC) jijini Mwanza nchini Tanzania kuokoa zaidi ya Sh2 bilioni fedha zilizotumika kusafirisha wagonjwa kwa matibabu nje ya kanda ya ziwa.

Akizungumza na maofisa wa habari Wizara ya Afya na taasisi zake jijini Mwanza jana Ijumaa Septemba 6, 2019 Mkurugenzi  Mkuu wa Hospitali hiyo, Profesa Abel Makubi alisema kuanza kwa tiba ya saratani katika hospitali hiyo ya kanda imesaidia kuokoa kiwango cha fedha hizo kutoka kwa wananchi wa kanda ya ziwa.

Alisema awali iliwalazimu kusafiri  hadi Jijini Dar es Salaam kupata huduma hizo kwenye Hospitali ya Saratani ya Ocean Road.

“Tunaishukuru Wizara ya Afya  ambayo ilitupatia kiasi cha Sh5.5 bilioni kwa ajili ya kujenga jengo  la saratani. Kama hospitali  tumeweza kununua  mashine nne za mionzi na dawa kwa kushirikiana na wafadhili wengine."

Aidha, alisema hivi sasa asilimia 90 ya wagonjwa hawapewi rufaa bali wanapata huduma hivyo kuwaondolea adha ya kusafiri na kupata huduma mbali ambapo awali zaidi ya asilimia 50 ya wagonjwa wa saratani wa Ocean Road walikuwa wakitoka kanda hiyo.

Naye Mtaalam wa Tiba Mionzi wa Idara ya Saratani wa BMC, Alex Mpugi alisema kabla ya mashine hizo walikua wakitoa huduma za saratani kwa kutumia kemikali.

"Naomba nitoe wito kwa wananchi hususan wanawake  kujitokeza kufanya uchunguzi wa saratani ya shingo ya uzazi na matiti kila siku ya Jumanne na Alhamis," alisisitiza Mpungi.

Mkurugenzi wa Upasuaji Dk Fabian Massaga  alisema, Hospitali  imefanikiwa kufanya ukarabati na upanuzi wa vyumba vya upasuaji kutoka vyumba sita hadi kumi na tatu ambapo vyumba viwili hutumika kwa upasuaji wa dharura na kimoja kwa ajili ya upasuaji  kwa akina mama wajawazito.

Alisema kwa upande wa upasuaji  wameweza kuongeza idadi ya wagonjwa kutoka 25 hadi 50 hivyo kupunguza idadi ya wagonjwa wengi waliokuwa wanasubiri upasuaji kwa miezi mitatu lakini hivi sasa wanafanyiwa upasuaji ndani ya wiki moja.

Hata hivyo, Dk Massaga alisema upanuzi huo umeendana na ununuzi wa vifaa vipya na vya kisasa  ikiwemo vitanda vya kufanyia upasuaji, taa maalumu za vyumba vya upasuaji na mashine za kisasa za kutolea dawa ya usingizi.

Vifaa hivi vimeagizwa moja kwa moja viwandani kwa takribani Sh1.4 bilioni badala ya Sh3 bilioni kama wangenunua kwa wauzaji hapa nchini.