Balozi Marekani amtembelea mke wa Azory Gwanda

Muktasari:

  • Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk Inmi Patterson amemtembelea Anna Pinoni ambaye ni mke wa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda.

Dar es Salaam. Kaimu Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dk Inmi Patterson amemtembelea Anna Pinoni ambaye ni mke wa mwandishi wa habari wa kujitegemea wa kampuni ya Mwananchi Communication Limited (MCL) mkoani Pwani, Azory Gwanda.

Azory alitekwa na watu wasiojulikana Novemba 27, 2017 ambapo kwa mujibu wa Anna, siku hiyo asubuhi watu wanne wakiwa katika gari aina ya Toyota Land Cruiser nyeupe, walifika katikati ya mji wa Kibiti, sehemu ambayo Azory hupatikana mara kwa mara, na kumchukua.

Watu hao walimpeleka hadi shambani ambako mkewe alikuwa akilima na akamuaga kuwa anaenda kazini, lakini hajarudi hadi leo.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatano Desemba 18, 2019 Anna amesema, “balozi alikuja nyumbani jana baada ya kunipigia simu kunieleza kuwa ubalozi wa Marekani watanitembelea nyumbani.”

“Aliniambia yeye kama mama anajua maisha ninayoishi kwa sasa ni ya shida,  na akasema anapata uchungu kama mama.”

Amebainisha kuwa balozi huyo alimletea chakula kwa ajili ya sikukuu ya Krisimasi, “kwa kweli tulizungumza kuhusu maisha na juhudi za kumtafuta Azory.”

Ukurasa wa mtandao wa kijamii wa Twitter wa ubalozi wa Marekani nchini Tanzania uliweka ujumbe wa balozi huyo kumtembelea Anna nyumbani kwake Kibiti mkoani Pwani.

 

Ilivyokuwa

Baada ya tukio la kutoweka kwa mwandishi huyo wa kujitegemea,  Anna alisimulia kuwa siku gari ilipokwenda shambani mumewe alikuwa amekaa kiti cha nyuma, alimuita kutokea upande huo wa gari na kumuuliza alikoweka ufunguo wa nyumba yao.

Anna alieleza kuwa alilisogelea gari na kuzungumza naye kutokea dirishani na kumweleza alipouficha ufunguo, huku Azory akimwambia amepata safari ya dharura na kama asingerudi siku hiyo ya Novemba 21,2017  basi angerudi siku inayofuata.

Anasema gari hilo liliondoka na kwenda nyumbani ambako alieleza kuwa aliporudi alikuta kuna upekuzi umefanyika kwa sababu alikuta vitu viko shaghalabaghala.

Kwa ujumla taarifa za kutoweka kwa Azory zilitangazwa kwa mara ya kwanza Desemba 7, 2017 katika mkutano uliowakutanisha wadau mbalimbali wa habari. Mkutano huo ulifanyika ofisi za makao makuu ya MCL zilizopo Tabata Relini, Dar es Salaam.

Baadaye, MCL iliendesha kampeni ya kumtangaza Azory kwenye kurasa za mbele za magazeti ya Mwananchi, The Citizen na Mwanaspoti na mitandao yake kwa kipindi cha siku 100.

Licha ya juhudi zote hizo, hadi leo hakuna taarifa iliyotolewa na chombo chochote kuhusu mahali Azory alipo.