Anayepumulia mashine alazwa tena Mloganzila

Muktasari:
- Wiki moja baada ya kuanza kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Taifa Muhimbili – Mloganzila, Dar es Salaam mgonjwa anayeishi kwa kupumua kwa msaada wa mashine Hamadi Awadh amelazwa tena katika hospitali hiyo kutokana na maradhi ya kushindwa kupumua vizuri kupitia mashine hiyo.
Dar es Salaam. Mgonjwa anayeishi kwa kupumua kwa mashine Hamadi Awadh (28) amelazwa Hospitali ya Taifa Muhimbili- Mloganzila, Dar es Salaam nchini Tanzania kufuatia tatizo la kushindwa kupumua.
Mwananchi imefika nyumbani kwa Awadh Kipawa, Dar es Salaam leo Jumatatu Septemba 23, 2019 kwa ajili ya kujua maendeleo ya mgonjwa huyo.
Kwa mujibu wa mke wa Awadh, Catherine Kulekana mgonjwa huyo alipelekwa hospitali Septemba 20, 2019 baada ya hali yake kubadilika.
“Kwanza alianza kushindwa kulala usiku baadaye hali yake ikawa inabadilika, Ijumaa tuliamka akiwa hajisikii vizuri na tatizo lilianza alipoanza kumeza dawa za moyo ambazo alipewa hospitalini alipokwenda kliniki.”
“Alivyoanza kumeza hilo tatizo likaanza. Nilimpigia simu daktari wake nikamweleza kuhusu hali yake, wakasema ingekuja ‘ambulance’ (gari la wagonjwa) ya dharura lakini mpaka mchana ilishindikana hivyo saa saba ikaja kutoka Mloganzila ikamchukua na tangu hapo amelazwa mpaka sasa ilikuwa saa asubuhi),” amesema Catherine aliyewasili nyumbani kwake akitokea Mloganzila.
Akizungumza na Mwananchi kwa simu, Awadh amesema kwa sasa anaendelea na matibabu akiwa chini ya uangalizi wa madaktari kwa siku tatu.
“Nililetwa Ijumaa hali yangu ilikuwa mbaya tangu nilipoanza kutumia dawa ambazo zilipatiwa lakini kwa sasa naendelea vizuri na madaktari wamesema wataweza kuniruhusu leo kama hali yangu itaendelea vizuri,” amesema Awadh.