Mikopo Udsm yawaponza viongozi Daruso, watano wasimamishwa

Dar es Salaam. Madai ya mikopo ya wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (Udsm) yamechukua sura mpya baada ya viongozi watano wa serikali ya wanafunzi (Daruso) kusimamishwa masomo kwa muda usiojulikana.
Uongozi wa Udsm jana ulitangaza kuwasimamisha viongozi hao ili kusubiri hatima yao watakapoitwa katika kikao cha nidhamu.
Hata hivyo wadau mbalimbali waliozungumza na Mwananchi walipinga hatua hiyo wakitaka madai ya wanafunzi hao yatekelezwe na si kuwasimamisha masomo.
Waliosimamishwa ni rais wa Daruso, Hamis Mussa; waziri wa mikopo, Joseph Malecela; mwenyekiti wa Bunge, Kasim Ititi; mwenyekiti wa ndaki ya sayansi asilia na tumizi (Conas), Milanga Hussein na Judith Mariki ambaye ni waziri wa habari, mawasiliano, jumuiya za wanafunzi na mambo ya nje.
Taarifa ya makamu mkuu wa Udsm, Profesa William Anangisye ilisema kwamba wanaendelea kuchunguza na kufuatilia mienendo ya wanafunzi wote na kila atakayebainika kuhusika kwa namna moja au nyingine atachukuliwa hatua stahiki za kinidhamu na kisheria.
Jumatatu iliyopita, Daruso walitoa madai yao wakitaka yatekelezwe ndani ya saa 72 vinginevyo wanafunzi wenye matatizo pamoja na viongozi wa Daruso watakwenda ofisi za Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) Mwenge jijini Dar es Salaam.
Uongozi Udsm ulichukua uamuzi huo kutekeleza agizo la Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako aliowapa saa 24 kuhakikisha wanachukuliwa hatua wote waliohusika kutoa tamko hilo.
Baada ya tamko hilo, naibu waziri wa Elimu, William Ole Nasha aliagiza uongozi HESLB kukutana na uongozi wa Udsm na Daruso kuangazia changamoto hizo na baada ya kikao, mkurugenzi mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru alisema wanashughulikia changamoto hizo na za wanafunzi wa vyuo vingine.
Uamuzi huo umewaibua Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) wakisema wapo tayari kwenda mahakamani kuwatetetea.
Mwenyekiti wa Bavicha, John Pambalu alilaani kitendo cha uongozi wa Udsm akisema wanafunzi hao wametolewa kafara kwa sababu walikuwa wakiwatetea wenzao.
“Tumeshazungumza na wanasheria wa Chadema na wapo tayari kuwatetea mahakamani,” alisema.
Awali wabunge Esther Matiko na Mchungaji Peter Msigwa waliungana mkono hatua ya Daruso kutaka kugomea kwani ni haki kudai haki yao na si kusimamishwa.
Mwenyekiti ngome ya vijana ya ACT Wazalendo, Bonifacia Mapunda alilaani uamuzi huo akisema Serikali ipeleke fedha HESLB na iwaagize kuwalipa wanafunzi hao haraka.
“Rais atimize ahadi yake aliyoitoa kipindi cha kampeni kuwa mwanafunzi akicheleweshewa mkopo wake aliyefanya hivyo atafukuzwa haraka,” alisema Mapunda.
“Waziri wa Elimu, Ndalichako awajibike kwa kushindwa kutatua tatizo hili kwa muda mrefu na kuchochea vurugu zaidi,” aliongeza.