Meya Ubungo atoa utetezi kesi ya kina Mbowe

Dar es Salaam. Meya wa Ubungo, Boniface Jacob ameieleza mahakama kuwa hawajawahi kupokea malalamiko yoyote kutoka kwa wananchi kuhusiana na hotuba zilizotolewa na viongozi wa Chadema katika mkutano wa kufunga kampeni ya uchaguzi wa ubunge wa Kinondoni.

Uchaguzi huo ulifanyika viwanja vya Buibui Mwananyamala Februari 16 mwaka juzi ambapo katika uchaguzi huo, Maulid Mtulia wa CCM aliibuka mshindi kwa kumshinda Salum Mwalimu wa Chadema. Mtulia alirejea kuongoza jimbo hilo baada ya kujiuzulu akiwa CUF na kutimkia CCM.

Jacob, ambaye pia ni diwani wa Ubungo (Chadema) jijini Dar es Salaam, alitoa kauli hiyo jana katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati akitoa ushahidi katika kesi hiyo ya uchochezi inayowakabili viongozi tisa wa Chadema mbele ya hakimu mkazi mkuu, Thomas Simba.

Meya huyo ambaye ni shahidi wa 10 katika kesi hiyo aliieleza mahakama kuwa kupitia hotuba hizo viongozi walipongezwa na wananchi.

Meya huyo alitoa ushahidi huo wa upande wa utetezi akiongozwa na Wakili Peter Kibatala na wenzake Profesa Abdallah Safari na Hekima Mwasipu huku upande wa Mashtaka ukiwakilishwa na mawakili Faraja Nchimbi, Wankyo Simon na Salim Msemo.

Jacob aliyaeleza hayo mahakamani hapo baada ya kuulizwa kama kuliwahi kutokea malalamiko yoyote juu ya hotuba hizo.

Alisema Mbowe alitumia muda mwingi kwenye hotuba yake kuhamasisha wananchi kwenda kupiga kura na umuhimu wake.

Pia alidai kuwa Mbowe alimnadi mgombea Mwalimu na kueleza kwa nini walimsimamisha na kwamba baada ya kuhutubia alimkaribisha Mwalimu aongee na kisha yeye Jacob alifunga mkutano.

Alidai ana uzoefu katika usimamizi wa uchaguzi na kuongeza kwenye uchaguzi mdogo wa ubunge wa Kinondoni alishiriki kama msaidizi wa aliyekuwa meneja wa kampeni Saed Kubenea.

Alibainisha kuwa katika mkutano huo uliofanyika siku ya Jumamosi ya Februari 16, 2018, wazungumzaji wakuu walikuwa ni Mwenyekiti Mbowe na Mwalimu.

“Siku hiyo ya kampeni mimi nilifika katika viwanja vya Buibui kwa mkutano wa mwisho wa kampeni uliokuwa unafanyika kati ya saa 8.00 mchana na saa 9.00 alasiri, ambapo nilitokea manispaa ya Kinondoni ambako niliapishwa na kusimamia mawakala wa vituo wa chama changu waapishwe.

“Wakati muda wa kampeni ukikaribia aliletwa Mbunge wa Viti maalum, Suzan Lyimo na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko wanisaidie kuwasimamia nikaenda kwenye mkutano wa kampeni kwa kutumia usafiri wa pikipiki,” aliongeza Jacob, ambaye pia ni mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema.

Alibainisha hali barabarani ilikuwa imechangamka kwa sababu ilikuwa siku ya kampeni, barabara zilifurika watu na magari wakati wakielekea kwenye mikutano ya vyama vya siasa kwa ajili ya kufunga kampeni. Akiongozwa na Wakili Kibatala, Jacob alidai katika mkutano huo waliondoka kwa amani na yeye alishirikiana na Mkuu wa Upelelezi Wilaya (OCD) kuangalia usalama na kwamba viongozi wakuu wa Chadema waliondoka kwa kutumia magari yao.

Alieleza kulikuwa na njia mbili ambapo baadhi walikwenda uelekeo wa Morocco na wengine makao makuu ya chama hicho mtaa wa Ufipa, Kinondoni.

Kesi hiyo inaendelea leo, ambapo washitakiwa ni wabunge na viongozi wa Chadema ambao ni pamoja na mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, katibu mkuu, John Mnyika, naibu katibu mkuu Zanzibar, Mwalimu, aliyekuwa katibu mkuu wa Chadema, Dk Vicent Mashinji, mbunge wa Tarime Mjini, Esther Matiko, mbunge wa Bunda, Ester Bulaya, mbunge wa Kawe, Halima Mdee, Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche na Mbunge wa Iringa mjini, Mchungaji Peter Msigwa.

Wanakabiliwa na mashtaka 13, ikiwemo kula njama, kufanya mkusanyiko wenye ghasia, kuhamasisha hisia za chuki, kushawishi hali ya kutoridhika, uchochezi na kushawishi utendaji jinai.