Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Papa Potwe, samaki asiyeliwa, kivutio cha utalii

Muktasari:

Wavuvi wengi wanakiri kushangazwa na tabia za samaki huyo pindi wawapo baharini. Wanasema baadhi yao waliwahi kuokolewa na Papa Potwe wakati walipokutwa na dhoruba baharini wakiwa kwenye shughuli zao za uvuvi.

Wapo wanaomuita Papa Potwe na wengine ‘Papa Mwema’ kwa ukarimu na tabia yake ya upole baharini.

Wavuvi wengi wanakiri kushangazwa na tabia za samaki huyo pindi wawapo baharini. Wanasema baadhi yao waliwahi kuokolewa na Papa Potwe wakati walipokutwa na dhoruba baharini wakiwa kwenye shughuli zao za uvuvi.

“Nilijikuta juu ya mgongo wa Papa Potwe, siku mashua yangu ilipotoboka kwa bahati mbaya na kuanza kuzama. Tunamuita ‘Papa Mwema’ kwa sababu anaweza kukuokoa ukikutwa na jambo gumu baharini,” anasema mvuvi wa Kilindoni, Mafia, Ismail Rajab.

Huruhusiwi kumuona Papa Potwe bila kulipia Sh25,000. Hili linamfanya samaki huyo awe kitega uchumi cha wilaya ya Mafia.

Papa Potwe wanapatikana kwa wingi katika bahari ya Hindi, pwani ya kisiwa cha Mafia. Mafia ni moja kati ya wilaya 6 za mkoa wa Pwani ambayo mji wake mkuu unaitwa Kilindoni.

Mazingira ya bahari katika kisiwa hicho yamejulikana zaidi haswa baada ya kuanzishwa Hifadhi ya Bahari (Mafia Island Marine Park - MIMP) na maeneo tengefu.

Shughuli kuu ya wakazi wa kisiwa cha Mafia ni uvuvi. Hata hivyo uzuri, wema na tabia nyingine za ‘Papa Potwe’ vimekipa heshima nyingine zaidi kisiwa hicho nje na ndani ya nchi kutokana na samaki hao kugeuka kivutio cha utalii.

Watembeza watalii wanasema wageni wengi wanaofika kwenye kisiwa hicho huwa wanaulizia kwanza anakopatikana Papa Potwe ili walipie na kwenda kumtizama.

“Mgeni anayetaka kumuona Papa Potwe ni lazima alipie. Kiuhalisia samaki hawa ni chanzo kikubwa cha mapato ya wilaya yetu na sisi wenyewe kutokana na uhakika wa kipato,” anasema Mkurugenzi wa Kampuni ya Utalii ya Whole Safari iliyopo kisiwani Mafia, Liberatus Mokoki.

Watalii wanaoenda Mafia kumtizama samaki huyo huogelea kwa kumzunguka papa huyo mwenye madoa madoa ya kupendeza na wakati mwingine huwa wanamgusa huku yeye akiwa ametulia tuli, akiwatazama.

Wataalamu wa viumbe hai baharini wanasema uvuvi haramu na uharibifu wa mazingira ni vitu vinavyomfanya samaki huyo kuwa kwenye mazingira magumu.

Usalama wa Papa Potwe unaufanya Shirika la Hifadhi ya Mazingira Duniani (WWF) kuamua kuisaidia jamii ya Pwani ya Mafia kumtunza na kumuenzi Papa Potwe, ili aendelee kuwa kivutio cha utalii na chanzo cha mapato ya kudumu.

Akizungumza katika maadhimisho ya siku ya wavuvi duniani yaliyofanyiwa Kilindoni, Mafia mratibu wa Mradi wa Raslimali za Bahari wa WWF ambaye ni mtaalamu wa viumbe hai baharini Dk Mathias Igulu anasema uhai wa Papa Potwe katika Pwani ya Mafia, ni muhimu kwa hifadhi ya bahari.

 

Samaki mpole mlinzi wa viumbe

Dk Igulu anasema mbali na faida yake kiuchumi, samaki huyo anapoonekana baharini huashiria uhai wa viumbe wengine kuzunguka kwenye eneo lake.

“Ni samaki mpole zaidi duniani, unaweza kumshika na wala asiwe na hofu yoyote, anaweza kucheza na watu na haliwi. Wageni wengi wanaokuja Mafia hutaka kumuona Papa Potwe ambaye tusipokuwa makini anaweza kutoweka. Tumeandaa maadhimisho haya ili kuwajulisha wananchi kwamba maisha ya samaki hawa ni uhai wetu,” anasema Dk Igulu.

Anasema WWF wanaendelea na mkakati wa kuwashirikisha wananchi wa Mafia wakiwamo wavuvi katika kuwalinda na kuwatunza samaki hao kwa kuthamini mazingira ya ufukwe wa bahari.

Mhifadhi Shirikishi Jamii wa Hifadhi ya Bahari - Mafia Albert Makalla anakiri kuwa utalii wa Papa Potwe unakiongezea hadhi kisiwa hicho. Makalla anasema samaki huyo anakabiliwa na mazingira magumu kutokana na uvuvi haramu unaofanywa na baadhi ya wavuvi katika maeneo hayo.

Mkurugenzi wa hoteli za kitalii za Meremeta, Abdulkadir Meremeta anasema utalii wa bahari kwenye kisiwa hicho unabebwa na Papa Potwe ambao lazima watunzwe ili wasipotee.

“Wageni wengi wanaofikia kwenye hoteli zangu hutumia muda wao mwingi kwenye utalii wa bahari na wengi huulizia walipo Papa Potwe,” anasema.

Ofisa uvuvi wa wilaya ya Mafia, Prisillah Tarimo anakiri kuwa Papa Potwe ni kati ya viumbe hai wa baharini anayechangia pato la halmashauri ya wilaya hiyo. Anasema wilaya hiyo imekuwa ikikusanya zaidi ya Sh500 milioni kutokana na sekta ya shughuli za baharini.

Katibu tawala wa wilaya ya Mafia, Gilbert Sandagile anasema rasilimali za bahari zinaongoza katika uchumi wa wilaya hiyo na hivyo lazima kuwe na jitihada za kuzilinda.

“Papa Potwe wamezalisha ajira kwenye kisiwa chetu, hivyo ni wajibu wetu kutunza mazingira ya bahari vinginevyo watatoweka na tutaanza kukosa watalii,” anasema.

Kutokana na hali hiyo, WWF imeamua kuanza kushirikisha wananchi katika ulinzi wa rasilimali za bahari kwa kuwasaidia kuunda vikundi vya ulinzi vya kupambana na tabia zote zinazohatarisha viumbe hai wa bahari ikiwamo uvuvi haramu.

 

Kwa nini haliwi

Bado haijathibitika sababu hasa japo zipo tetesi kwamba, urafiki wake na watu ndio ambao umesababisha asiliwe.

Dk Igulu anasema wamekuwa wakiwasihi wananchi wasiwadhuru kwa namna yoyote ile hata kama ni kweli haliwi.

“Tunaendelea na utafiti na ni kweli kwamba wavuvi hawamvui samaki huyu kwa sababu haliwi. Tukipata majibu ya kitaalamu tutakuwa na nguvu ya kusema,” anasema.

 

Papa Potwe na utalii

Umuhimu wa samaki hao kwenye sekta ya utalii unaigusa wilaya ya Mafia kwa namna nyingine na kuandaa mikakati ya kuhakikisha anatunzwa.

Katibu tawala wa wilaya hiyo, anasema watahakikisha wanashirikiana na mashirika kama WWF kuhakikisha rasilimali za bahari zinaendelea kuwa salama. Anasema ili kuwalinda samaki hao lazima wapambane na wavuvi haramu wanaohatarisha uwepo wa viumbe hai baharini.

“Serikali itaendelea kupambana na uvuvi wa kutumia sumu ambao unatishia maisha ya samaki hawa muhimu kwa uchumi wa Mafia,” anasema.

Anawataka wananchi wa Mafia kutoa taarifa za watu wanaojihusisha na uvuvi haramu ili hatua za kisheria dhidi yao ziweze kuchukuliwa.

 

Utunzaji mazingira ya bahari

Mwenyekiti wa kijiji cha Kilimani, Omari Amiri anasema japo wao wanaona samaki huyo ni wa kawaida, wamekuwa wakipokea wageni wengi wanaopenda kwenda kumuona.

“Tunachofanya sisi ni kusimamia utunzaji wa mazingira ya bahari,” anasema.

Hata hivyo anakiri kuwa shughuli za utalii wa baharini zinachangia kuongeza mapato ya kijiji chake ikiwamo, kuwawezesha vijana kupata ajira.

Anaiomba Serikali na mashirika yanayojihusisha katika masuala ya baharini wakiwamo WWF kuendelea kutoa elimu ya mazingira kwa wananchi ili wamtunze samaki huyo.

Mvuvi Athumani Juma anasema japo kuna wakati samaki hao huwa wanaharibu mitumbwi yao hawawezi kuwavua wala kuwaua, kutokana na wanavyoonekana.

“Akiingia kwenye nyavu huwa kuna namna ya kumtoa vinginevyo huharibu, hata hivyo hatumdhuru,” anasema.

Hasira za wavuvi kwa samaki huyo ni pale anapoamua kuharibu vyavu zilizotegeshwa baharini kwa ajili ya kuvua ili awaokoe samaki wadogo walionaswa.

“Huwa anaweza kuchana nyavu na usiambulie chochote, hapo ndipo huwa tunapata hasira kutaka kumuumiza lakini tukikumbuka wema wake, tunamuachia,” anasema Juma.

 

Bahari ndiyo mapato, maisha yetu

Ofisa uvuvi wa Mafia, Tarimo anasema changamoto kubwa ni uvuvi haramu na kwamba, wanaendelea na jitihada za kupambana nao.

Dk Igulu anasema uvuvi wa kutumia sumu na baruti uliwasukuma WWF kuunda vikundi vya ulinzi shirikishi katika pwani ya bahari ya Hindi, ili kusaidia ulinzi.

“Tuligundua kwa kutumia ulinzi shirikishi wa rasilimali za bahari tutaweza kutunza mazingira ya bahari. Hadi sasa kuna vikundi vya ulinzi zaidi ya 160 katika pwani yote ya bahari,”anasema.

Hivi karibuni, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan alisema Serikali itatumia kikosi maalumu cha kukabiliana na uvuvi haramu unaoendelea katika bahari ili kudhibiti tatizo hilo ambalo limeathiri mazalia ya samaki na kutishia kupungua kwao.

Anasema katika kuhakikisha kazi hiyo inafanyika, watatumia wataalamu wa mazingira ambao watafanya tathmini ya uharibifu katika bahari ili waweze kuchukua hatua ya kukabiliana na hali hiyo.

“Bahari yetu ndiyo mapato yetu, bahari yetu ndiyo maisha yetu, tumeitumia vibaya mapato yamepungua na maisha hayawi mazuri hivyo ni muhimu tuitunze ili iendelee kutulea…,” anasema Makamu wa Rais.