Soko la kimataifa la nafaka Kibaigwa ladorora
Muktasari:
Soko la kimataifa la nafaka la Kibaigwa mkoani hapa, limeshindwa kuuza mazao nje ya nchi kutokana na upungufu mkubwa wa mazao uliosababishwa na ukame katika msimu wa kilimo uliopita.
Dodoma. Soko la kimataifa la nafaka la Kibaigwa mkoani hapa, limeshindwa kuuza mazao nje ya nchi kutokana na upungufu mkubwa wa mazao uliosababishwa na ukame katika msimu wa kilimo uliopita.
Akizungumza jana mjini hapa, Meneja wa soko hilo, Kusekwa Dalaly alisema kwa sasa wanapokea mazao kidogo hali inayosababisha washindwe kusafirisha hata nje ya Mkoa wa Dodoma.
“Siku nyingine tunapokea hadi tani moja kwa siku. Hatuwezi kusafirisha, tunayauza hapa hapa Dodoma,” alisema Dalaly.
Dalaly alisema Juni mwaka jana, kilo moja ya mahindi ilikuwa ikiuzwa kati ya Sh580 hadi 600, lakini sasa yanauzwa kati ya Sh620 hadi 630.
Mfanyabiashara wa mahindi katika soko hilo, Idd Rafael alisema hivi sasa wamefikia hatua ya kununua mahindi yanayodaiwa kuzalishwa Uganda kwa sababu ya Tanzania yameadimika sokoni hapo.
Mama mmoja anayesafisha mahindi sokoni hapo, Grace Samson alisema kutokana na kupungua kwa mahindi yanayoingizwa katika soko hilo, wanakosa kazi za vibarua vya kupeta mahindi.
Mkulima wa mahindi wilayani Kongwa, Machite Mwaluko aliiomba Serikali kuwapa mitaji wakulima waweze kuongeza uzalishaji wa mazao. Mwaka jana, soko hilo lilipokea tani 27,756.56 za mahindi ikiwa ni pungufu ya karibu tani 56,315.08 zilizopokewa mwaka juzi.