Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mkapa: Tanzania haijachangamkia fursa za kibiashara kama Rwanda

Mwenyekiti wa Taasisi ya Mazingira ya Uwekezaji Afrika (ICF), Benjamin Mkapa

Muktasari:

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuhusu utendaji wa taasisi hiyo kwa miaka sita, Mkapa, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema Rwanda ilijitokeza zaidi kwenye taasisi hiyo kuomba misaada kuliko Tanzania na nchi nyingine

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Taasisi ya Mazingira ya Uwekezaji Afrika (ICF), Benjamin Mkapa amesema Rwanda imefanikiwa zaidi kwenye uwekezaji na biashara kuliko Tanzania kwa sababu ya kuchangamkia fursa za taasisi hiyo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam kuhusu utendaji wa taasisi hiyo kwa miaka sita, Mkapa, ambaye aliongoza Serikali ya Awamu ya Tatu, alisema Rwanda ilijitokeza zaidi kwenye taasisi hiyo kuomba misaada kuliko Tanzania na nchi nyingine.

“Nimesema kuwa kazi yetu ilikuwa ya kuhitaji, sasa kama Serikali haina juhudi binafsi za uwekezaji na biashara na mnajaribu kuwaonyesha mianya lakini hawajali kufanya mabadiliko, unafanyaje?” alihoji Mkapa.

“Kwa Kiswahili tunasema “chema chajiuza, kibaya chajitembeza”. Sasa ndiyo hivyo tena. Sisi hatukutaka kuwa wabaya, tulitaka kuwa wema. Sasa kama hukuombwa, kwa nini ujilazimishe kwa watu huko?

“Kwa nini Rwanda wamefanikiwa sana? Ni kwa sababu walikuwa macho. Walikuwa makini katika utekelezaji, wakitekeleza vizuri kwa kushirikiana nasi na wakiomba zaidi tutakwenda kusaidia zaidi.”

Pia alisema ilikuwa rahisi kuwasaidia kwa sababu mataifa mengine yalikuwa tayari kuwasaidia pamoja na taasisi yao.

“Tumeombwa, tulitazama uwezo wetu mdogo na hiyo ndiyo ilikuwa kazi tuliyoifanya. Hakuna siri. Ukitaka mabadiliko lazima uwe tayari kufanya mabadiliko,” alisema.

Hata hivyo, alisema taasisi hiyo ilishirikiana na Tanzania kuboresha Mahakama ya Biashara, kuboresha bandari na kupunguza vizuizi barabarani ili kurahisisha usafirishaji wa bidhaa katika nchi za Rwanda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Akizungumzia ufanisi wa taasisi hiyo, Mkapa alisema kulikuwa na miradi 73 iliyokuwa ikitekelezwa katika nchi 36 za Afrika ambayo imerahisisha uwekezaji na biashara.

“Tumeweza kuunda mahakama tisa za biashara katika nchi za Rwanda, Burkina Faso na Sierra Leone zenye lengo la kufanikisha kumaliza mashauri ya kibiashara. Tumeanzisha pia mahakama nne za usuluhishi ambazo ziko Ivory Coast, Nigeria, Rwanda na Togo,” alisema Mkapa.

“Pia tumesaidia nchi kuwa na mfumo wa kielektroniki wa soko la pamoja katika nchi za Kenya, Senegal, Tanzania na Sao Tome kwa lengo la kurahisisha biashara ya kutoa mizigo forodhani.”

Alisema wamesaidia kuanzisha mifumo sita ya mitandao ya kodi inayosaidia biashara katika nchi za Cape Verde, Rwanda, Senegal, Zambia na mifumo mitano ya usajili wa biashara kama Rwanda, Burkina Faso na Cap Verde.

“Rwanda ilikuwa inachukua siku 16 kusajili biashara, sasa inachukua saa sita tu. Ilikuwa inachukua siku 23 na nusu kufuatilia na kulipa kodi, sasa yoyote anaweza kufanya mara moja kupitia mtandao. Watu wanaweza kusajili ardhi ndani ya siku mbili badala ya siku saba ilivyokuwa kabla ya kushirikiana nasi,” alisema.

Kwa Tanzania, Mkapa alisema zaidi ya waajiriwa na wamiliki 1,000 wa biashara za kati na ndogo wamepewa mafunzo ya biashara katika dirisha moja la biashara ya jinsi ya kutoa mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam.

“Zambia, watu wamewezeshwa kulipa kodi kupitia mtandao kwa siku moja badala ya siku 10. Mashauri mahakamani yanapelekwa haraka na kwa uwazi,” alisema.

Ofisa mtendaji mkuu wa taasisi hiyo, William Asiko alisema miradi hiyo iliyotekelezwa kati ya mwaka 2007 na 2016, imewezesha biashara nyingi kusajiliwa, kulipa kodi zao kwa urahisi, kusuluhisha migogoro ya kibiashara, kupitisha mizigo kupitia forodha kwa njia ya haraka, rahisi na iliyo wazi.