Watu milioni 1.4 wanaishi na virusi vya Ukimwi

Muktasari:
- Taarifa kutoka taasisi ya Egpaf – Boresha Afya inasema kwamba hadi kufikia Oktoba 2016 asilimia 70 ya watu wanaoishi na VVU ndio waliopima kufahamu hali zao.
Inadaiwa kwamba zaidi ya watu milioni 1.4 wanaishi na virusi vya Ukimwi nchini.
Taarifa kutoka taasisi ya Egpaf – Boresha Afya inasema kwamba hadi kufikia Oktoba 2016 asilimia 70 ya watu wanaoishi na VVU ndio waliopima kufahamu hali zao.
Mkurugenzi Mkazi wa Taasisi ya Egpaf, Jeroen Van’t Pad Bosch alisema zinahitajika juhudi kubwa ili Tanzania ifikie lengo la asilimia 90 ya watu wanaoishi na VVU kupima afya na kujitambua.
Alisema Shirika la Maendeleo ya Kimataifa la Marekani (Usaid) limetoa Dola129 milioni (zaidi ya Sh260 bilioni) kwa ajili ya kutekeleza mradi wa Egpaf - Boresha Afya unaotekelezwa katika mikoa sita hapa nchini kwa ajili ya mradi wa upimaji VVU.
Bosch alisema mradi huo unahamasisha upimaji wa virusi kwa watoto, vijana na wazazi wanapofika kwa mara ya kwanza kupata huduma za kliniki na kushauriwa kupima.
Alisema kuwa Egpaf inafanya kazi kwa ushirikiano na vituo vya afya vya Serikali na mashirika binafsi katika mikoa hiyo kwa lengo la kuhakikisha watu 170,000 wanapimwa VVU.
“Takwimu zinaonyesha kuwa wanawake wanaopima VVU ni wengi kuliko wanaume, ambapo asilimia 82 ya wanawake wanaoishi na VVU nchini tayari wamepima na wanafahamu afya zao huku kwa wanaume wakiwa wachache,” alisema.
Meneja Mradi wa Usaid - Boresha Afya kutoka ofisi ya Egpaf mkoani Arusha, Dk Leo Haule alisema wamekuwa wakitengeneza huduma rafiki kwa vijana ili wapate huduma ambayo itawaridhisha na kufanya wasiache kutumia dawa za kufubaza virusi vya Ukimwi.
Alisema kuwa Egpaf imekuwa ikifanya kazi kwa zaidi ya miaka 10 hivi sasa huku wakisaidiana na Serikali kwa kuweka kipaumbele kumlinda mama na mtoto pamoja na vijana.
Meneja Mwandamizi Huduma za Jamii kutoka taasisi hiyo, Daniel Lukumay alisema wana utaratibu wa kufanya kambi ya watoto wanaoishi na VVU kila mwaka ambao wanahudumiwa katika hospitali mbalimbali kupitia shirika hilo kutoka mikoa sita.
Pia, Lukumay alisema tangu waanze kuwakutanisha watoto ili kushiriki michezo mbalimbali, imesaidia kuleta mafanikio kutokana na wengi wao kutojisikia wapweke kutokana na hali walizonazo sambamba na kuwa mabalozi wa wengine popote wanapokuwa.