Mwalimu Mwakasege alivyoongoza maombi mbele ya jeneza la mwanaye

Mwalimu Christopher Mwakasege (kulia) akiwa na Joshua Mwakasege enzi za uhai wake. Picha ya Mtandao.
Muktasari:
- Mwalimu wa Neno la Mungu, Mchungaji Christopher Mwakasege amefiwa na mtoto wake wa pekee wa kiume, Joshua Mwakasege aliyekuwa mtumishi wa Benki ya Dunia hapa nchini. Hata hivyo msiba huo licha ya kuwaumiza wengi lakini wengi pia wamevutwa na hatua ya Mchungaji Mwakasege kuweza kuhimili uchungu kwa siku tatu tangu alipopokea taarifa na kuendelea kumtumikia Mungu akiwa kwenye semina mkoani Mbeya.
Katika wakati unaotarajia kuona baba akimwaga machozi ni pale anapompoteza mwanaye wa kiume wa pekee. Lakini hali haiwi hivyo.
Badala yake msiba unageuka sehemu ya maombi kwa watu kutubu dhambi na kutengeneza upya uhusiano baina yao na Mungu.
Hali hiyo ndiyo iliyojitokeza wakati wa kuaga mwili wa Joshua Mwakasege, mtoto wa Mwalimu wa Neno la Mungu, Mchungaji Christopher Mwakasege katika ibada iliyofanyika kwenye Kanisa la Kiinjili la Kirutheli Tanzania (KKKT), Mbezi Beach (Jogoo).
“Kama kuna mtu anataka kuokoka anyoshe mkono wake na apite mbele. Tengeneza uhusiano wako na Mungu kwa sababu hujui kifurushi cha siku zako za kuishi kimebaki kiasi gani,” alisema Mwakasege.
Mwalimu Mwakasege alilazimika kuongoza maombi hayo baada ya waombolezaji waliokuwa wamefurika katika ibada ya kuaga mwili wa Joshua kutaka waisikie sauti yake.
Joshua aliagwa juzi katika Kanisa la Mbezi Beach (Jogoo) baada ya kifo chake kilichotokana na kuugua ghafla Octoba 11, mwaka huu akiwa kazini na kukimbizwa katika Hospitali ya Aga Khan ambako alifariki siku hiyo hiyo, saa tatu usiku.
Kilichowashangaza wengi, ni uwezo wa Mwalimu Mwakasege kuhimili maumivu makali ya kifo cha mwanaye na kumudu kuongoza maombi akiwaombea waombolezaji.
Mwalimu Mwakasege alianza kwa kuimba na moja kati ya nyimbo alizoanzisha ni ule wa ‘Salama Rohoni Mwangu”. Pia, alitumia nafasi hiyo kumshukuru Mungu akisema ‘Hata katika hili bado wewe ni Mungu na utabaki kuwa Mungu, ni salama rohoni mwangu”.
“Njoo mbele,” aliwaita waumumini wapite mbele kwa ajili ya maombi.
Waumini walipita mbele na kusimama katika eneo ambalo pia mwili wa Joshua ulikuwa umehifadhiwa ndani ya jeneza kubwa, jeupe.
Huku wakiwa wamenyosha mikono yao juu, Mwalimu Mwakasege aliwaongoza sala ya toba.
Awali Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Alex Malasusa alimpa nafasi Mwalimu Mwakasege atoe neno la shukrani baada ya waombolezaji hao kuonyesha hamu ya kutaka kumsikiliza.
Lakini pia kabla hajapewa nafasi hiyo, kila kiongozi wakiwamo wa Serikali waliosimama kuzungumza walimtia moyo Mwakasege kutokana na msiba huo.
Hata hivyo, aliposimama alionyesha kuwatia moyo waombolezaji huku akisisitiza kuwa, kifo cha mwanae hakitavunja uhusiano baina yake na Mungu.
“Unapopita kwenye jaribu kama hili, hata sisi ni binadamu tunaumia na kuwa na maswali mengi pia, tofauti yetu na wengine, sisi tuna wito ndani yetu.”
Katika ibada hiyo viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa walihudhuria.
Miongoni mwa waliohudhuria ni Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ambaye pia alionekana kuimba kwa hisia kali huku akiwa amenyosha mikono yake juu wakati Mwalimu Mwakasege alipokuwa akiimbisha.
Wengine waliokuwapo ni Naibu Spika Dk Tulia Akson, Mawaziri wakuu wastaafu, Edward Lowasa na Fredrick Sumaye, Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na Wabunge Mwigulu Nchemba (Iramba) na Nape Nnauye (Mtama).
Wengine ni Spika Mstaafu wa Bunge, Anne Makinda, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Amon Mpanju, Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu, Balozi Ombeni Sefue na Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Godwin Gondwe.
Aliwasiliana na mwanae kabla ya kifo
Mwakasege anasema wakati kifo cha mwanae kinatokea alikuwa mkoani Mbeya akiendelea na semina za kufundisha neno la Mungu kama ilivyo kawaida.
Anasema awali aliwasiliana na mwanae, lakini kwa sababu mazungumzo yao hayakufika mwisho, na alikuwa akiwahi kufundisha watu aliahidi wangewasiliana baadae.
“Joshua nilikuwa namwita bwanamdogo, tuliongea na nikasema nikitoka kwenye semina basi tutaongea tena,” anasimulia.
Anasema baada ya semina alimpigia simu mwanae kama alivyo ahidi.
“Lakini nikashangaa simu inaita tu bila kupokelewa, baadae mlinzi alipokea na kusema Joshua amekimbizwa hospitali,” anasema.
Anasema baadae simu ilipokelewa na mlinzi wa World Bank, Ofisi ndogo za Dar es Salaam alikokuwa akifanya kazi mtoto wake na kuambiwa kuwa, Joshua anaumwa na amekimbizwa hospitali.
Mwalimu Mwakasege anasema walianza maombi kwa ajili ya kumuombea mwanae wakiwa wote na mkewe, Diana Mwakasege.
Jinsi alivyopokea taarifa za kifo
Anasema wakati maombi yakiendelea akapigiwa simu na daktari na kupewa taarifa za kifo cha mwanae.
“Nilipopewa taarifa na daktari akisema ‘tumejitahidi kuokoa uhai wa mwanao lakini hayupo’ ilikuwa ngumu sana. Kitu cha kwanza nilichowaza ni namna ya kumweleza mke wangu,” anasema.
Anasema kwa sababu anaujua moyo wa mkewe ilibidi amwambie ukweli kwamba Joshua amefariki.
“Fikiria wakati ambapo mke wangu anaomba kwa ajili ya mwanae anapewa taarifa za kifo inakuwaje! Ilibidi nimweleze kilichotokea na nikamsihi anyamaze,” anasema.
Mwalimu Mwakasege anasimulia kwamba waliendelea na maombi kubwa kumshukuru Mungu kwa sababu ya jambo lililotokea.
“Kwa kweli hatukulala, kulipokucha tukawa na vitu vitatu. Je tunamweleza nini Mungu? Tukakubaliana kumwambia kwamba haijalishi hali gani tunapitia ila tunataka kumhakikishia kwamba ni Mungu wetu atabaki kuwa Mungu wetu,” anasema na kuongeza; “Jambo la pili tutaendelea kumtumikia na jambo la mwisho, kamwe hatuwezi kukasirika kwa sababu ya hili.”
Amalizia siku tatu za semina
Mwalimu Mwakasege anasema baada ya kumhakikishia Mungu kwamba wataendelea kumtumikia walianza kuwaza juu ya semina ambayo ilibaki siku tatu imalizike.
“Ilikuwa Alhamisi, kwa hiyo tulibakiza Ijumaa, Jumapili na Jumatatu. Tuliwaza namna tutakavyo waacha watu zaidi ya 10,000 wanaohudhuria semina kwa sababu ya msiba,” anasema.
Anasema ilibidi wakubaliane kwamba hata kama msiba umetokea lazima wamalize siku zote tatu zilizobaki.
“Ni rahisi kuona tunaendelea na semina mkadhani ilikuwa uamuzi mwepesi lakini ilikuwa ngumu, tuliwashirikisha ndugu na jamaa wote tukakubaliana lazima tumalize,” anasema. Anasema miaka ya 1980 wakati wanaanza huduma hiyo walimuahidi Mungu kwamba, watamtumikia katika kipindi chote cha maisha yao.
“Tuliahidi kuwa sisi na watoto wetu tutamtumikia Mungu kwa hiyo hata watoto nilipowaeleza kuwa kaka yao hayupo walipokea, na wao wakahoji itakuwaje kuhusu semina? Nilifurahi kwamba hata watoto wanawaza kuhusu Mungu,” anasema.
Semina yaendelea
Katika mitandao ya kijamii, tayari taarifa za kifo cha Joshua zilikuwa zimeshasambaa.
Lakini kihalisia taarifa hizo hazikumfanya Mwalimu Mwakasege kuacha semina akiwafundisha watu neno la Mungu kupitia semina iliyoanza kabla ya kifo hicho.
“Sikuwaeleza watu kuhusu msiba ulionikuta, niliwaacha hadi siku ya mwisho,” anasema.
Anasema kama angewaeleza kuhusu msiba huo huzuni ingetanda na angeshindwa kuendelea kuwafundisha.
Ijumaa ilikuwaje?
Anasema Ijumaa, siku ya kwanza ya semina baada ya kifo cha mwanae ilikuwa ngumu hasa mmoja wa waimbaji alipoanzisha wimbo uliotaja maneno ya kumshukuru Mungu.
“Sikusimama kuimba nilijua ningetoa machozi. Jumamosi ilikuwa ngumu zaidi na tunamshukuru Mungu kwa sababu ya jambo hili gumu,” anasimulia.
Askofu ahubiri
Akihubiri katika ibada hiyo, Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam Jackson Sostenes anasema Mungu aliamua kumpitisha Mwalimu Mwakasege kwenye jaribu hilo akitaka kupima utumishi wake.
“Mwakasege amejipambanua wazi kwamba anaishi yale anayofundisha pamoja na kupitia kipindi kigumu lakini hakuacha kuwafundisha watu neno la Mungu, hakuacha semina,” anasema. Anasema kifo cha Joshua ni somo kwa watu wengine kujiuliza maswali kuhusu maisha yao duniani.
“Joshua ameuvua mwili unaoharibika na kuuvaa mwingine, huzuni ya kifo hiki inaongezeka kwa sababu ni ghafla, lakini tuwe na tumaini kwamba ipo siku tutakutana tena,” anasimulia.
Nasaha za viongozi
Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda aliposimama kutakiwa kuzungumza kuhusu msiba huo aliishia kuimba wimbo wa tenzi za rohoni ‘Nataka kumjua Yesu’.
Mbowe ambaye pia ni mbunge wa Hai, akizungumza kwa niaba ya wabunge alisema haijalishi kiongozi wa chama au Serikali, kifo cha Joshua na namna baba yake alivyofanya kinapaswa kuwakumbusha kuishi yale wanayoyasema.
“Mungu alipenda kutumia tukio hili kukufunua kwa dunia, alitaka watu waone kile unachohubiri je unakiishi? Umeonyesha hivyo Mwalimu Mwakasege, tunajifunza kwako.
Naibu Spika Dk Akson alisema kupitia msiba huo amejifunza namna ya kulea watoto.
“Watoto wanapaswa kuishi kama sisi tunavyoishi haijalishi tupo nao au hatupo nao. Pole sana Mwalimu Mwakasege kifo hiki cha Joshua ni fundisho kubwa kwetu,” anasema.
Naye Spika mstaafu Makinda alisema alimfahamu Mwalimu Mwakasege muda mrefu na siku zote amekuwa akijifunza mambo mengi yahusuyo maisha kupitia yeye.
“Tukiwa Uingereza alinipatia kitabu kinachoeleza namna ya kujenga nyumba. Kile kitabu kilinifundisha kwamba sipaswi kujenga nyumba ya vyumba vitatu ila vinne kikiwamo cha wageni ili wanapokuja, watoto wasigeuke watumwa kwenye nyumba yao kwa kuhama hama,” anasema.
Mwili wa Joshua uliwasili kanisani saa tano na kutoka saa 12 jioni. Hata hivyo, licha ya kuwa hapo kwa muda mrefu waliohudhuria waliendelea kuvumilia, wakitamani ibada iendelee hasa maombi yaliyoongozwa na Mwakasege yalipoanza.
Leo mwili huo unazikwa nyumbani kwao Tukuyu, Mkoani Mbeya baada ya kuwasili jana ukitokea jijini Dar es Salaam.