Tukio la kuchanganya udongo wa Muungano na miujiza yake

Mwalimu Julius Nyerere akichanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar kuashiria Muungano wa nchi hizo mbili, na yeye kuwa Rais wa Kwanza wa Jamuri ya Muungano wa Tanzania.
Muktasari:
- Uteuzi na kupende-kezwa majina ya vijana 100 kutoka Zanzibar ambao waliungana na wenzao wa Tanganyika ulifanywa na Halmashauri Kuu ya ASP Youth League, wiki moja kabla ya siku ya Muungano walichezeshwa gwaride la Muungano, nyakati za asubuhi na jioni wakiongozwa na Bi Mwakemwa.
Kazi ya kuchanganya udongo wa Tanganyika na Zanzibar ilianza saa tatu asubuhi na kulikuwa na miujiza mingi.
Zanzibar. Wakati Watanzania wakiadhimisha miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, siku ulipochanganywa udongo wa pande mbili za Muungano kulikuwa na mazingira ya ajabu na mabadiliko ya vipindi vya hali ya hewa vilivyowababaisha na kuwashangaza watu wengi waliohudhuria sherehe hizo.
Sherehe za kuchanganya udongo wa pande mbili uliowekwa kwenye vibuyu viwili tofauti zilifanyika Aprili 26, 1964 kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam na Mwalimu Nyerere alichanganya udongo kwa kuumimina ndani ya chungu kuashiria Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Mmoja kati ya watu waliobeba udongo wa Zanzibar na kuchanganywa na ule wa Tanganyika, Hassan Omar Mzee (66) akihojiwa na Mwananchi nyumbani kwake huko Kibweni nje ya Mji wa Unguja, anaitaja siku hiyo ilikuwa ya aina yake atakayoikumbuka maishani. Wakati wa tukio hilo alikuwa na umri wa miaka 16.
Hassan anasema kazi ya kuchanganya udogo wa Tanganyika na Zanzibar ilianza saa tatu asubuhi na kukiwa na manyunyu ya mvua, jua lisilounguza likiwaka na kupotea na mawingu yaliyokuwa na kivuli cha ubaridi yakiwa yametulizana juu ya anga huku ukimya ukitawala eneo la uwanja.
Anasimulia kuwa lilikuwa tukio la aina yake ambalo liliwashangaza viongozi wengi wa nje na ndani, waliohudhuria na kushuhudia kitendo hicho cha kijasiri na cha kihistoria kilichofanywa na viongozi wa mataifa ya Tanganyika na Zanzibar, Mwalimu Julius Nyerere na Sheikh Abeid Amani Karume (wote kwa sasa ni marehemu).
Mshangao huo unatokana na mazimio ya harakati za vikao vingi vya viongozi wa Kiafrika, walikuwa na lengo la kuungana baada ya kujikomboa kutoka kwenye ukoloni, lakini maazimio hayo yaliwashinda viongozi wengi pia Nyerere na Karume walitekeleza kwa vitendo.
Anasema siyo Mwalimu Nyerere wala Mzee Karume walionekana kuwa na hofu ya kupoteza madaraka ya nchi zao, hawakutaka kuendekeza fahari ya vyeo vyao na badala yake walichokitanguliza mbele ni nia na azma ya kujenga umoja wa kitaifa wa watu wao.
Jamhuri ya watu wa Zanzibar na ile ya Tanganyika ndipo zilipokufa. Mabeberu na wakoloni wakipigwa na butwaa kuona kitendo hicho kikitokea na viongozi wa pande mbili wakiwa na nyuso za furaha na bashasha pia wananchi wengine wakionekana kutokwa na machozi ya furaha kutokana na tukio hilo.
Akielezea tukio hilo, Hassan anawataja wenzake wengine watatu walioshiriki katika kazi ya kubeba udongo wa pande mbili za Muungano ni Hassan Kheir Mrema na Sifaheri Kunda kutoka Tanzania Bara na Khadija Abbas kutoka Zanzibar.
Wenzao wanawake walibeba vibuyu vidogo na vikubwa vyenye udongo na wanaume walibeba chungu kimoja kilichochanganyiwa udongo, tukio lilifanyika katikati ya Uwanja wa Taifa ambako jukwaa maalumu lilijengwa.
“Siku hiyo tuliamka mapema tukiwa tumepewa mavazi maalumu, wanaume tulivaa shati na suruali zilizoshonwa kwa vitenge, wenzetu wa kike walivaa mavazi maalumu ya khanga zilizozingatia utamaduni wa Mwafrika,” anaeleza Hassan.
Anasema kabla ya kazi hiyo kufanyika, kulikuwa na mazoezi ya vitendo wiki moja nyuma yake, jinsi ya utaratibu mzima utakavyokuwa hadi kuchanganywa udongo wakiongozwa na Bi Mwakemwa, ndiye aliyekuwa mwenyeji wao tokea walipowasili Dar es Salaam na kupiga kambi Uwanja wa Taifa. Hassan anaeleza ilipofika saa tatu juu ya alama wananchi kutoka Tanganyika na Zanzibar walikusanyika na kukaa kwenye jukwaa la Uwanja wa Taifa kwa utulivu, wakisubiri kuona na kushuhudia tukio la kihistoria likifanyika ili kuziunganisha nchi mbili kuwa Taifa moja.
Anaeleza baada ya kazi hiyo kukamilika, akiwa na wenzake waliondoka hadi kwenye jukwaa kuu wakiwa na vifaa vilivyotumika kubeba udongo na baadaye kwenda kukaa sehemu waliopangiwa kabla ya kuanza safari ya kuelekea Ikulu ya Dar es Salaam.
Anaeleza walipofika Ikulu kulikuwa na tukio kubwa la kihistoria na ulipandwa mti wa mwembe wa kumbukumbu ya Muungano, uliopandwa na Mwalimu Julius Nyerere akishirikiana Mzee Karume, ukapewa jina la mwembe wa Muungano.
“Mimi nilimkabidhi galoni lililokuwa na maji Mwalimu Nyerere ili kuumwagia mti uliopandwa, Hassan Kheri alimkabidhi Mzee Karume galoni jingine na kuumwagia mwembe huo, hadi leo mwembe huo upo, ni mkubwa kuliko yote ndani ya uzio wa Ikulu,” anasema Hassan akiwa bado anaonyesha kuwa na hamu ya tukio hilo.
Baada ya kumalizika kazi hiyo, sehemu ya udongo uliobakia na vifaa vilivyotumika vilipelekwa kwenye Makumbusho ya Taifa, hadi leo vitu hivyo vinaoonekana na kushuhudiwa na wanaokwenda kuitembelea makumbusho hiyo.
“Udongo wa Zanzibar uliochanganywa na ule wa Tanganyika ulitoka eneo la Kizimbani hapa Unguja, ule wa Tanganyika ulichotwa maeneo ya Dar es Salaam, udongo toka maeneo hayo sasa umeliunganisha taifa zima na mipaka yake, sasa tuna Taifa moja la Tanzania na kiti kimoja Umoja wa Mataifa, ” anasema Hassan.
Safari yao kutoka Unguja hadi Dar es Salaam
Akiwa mwanafunzi wa Chuo cha Ufundi Zanzibar mwaka 1964, pia Katibu Mipango wa Umoaj wa Vijana wa ASP ‘Youth League’, jina lake liliteuliwa kuwa katika orodha ya watakaoshiriki tukio la kuzaliwa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Maandalizi ya safari yao yalifanywa na Mwenyekiti wa ASP Youth League ,hayati Seif Bakari Omar mmoja kati ya watu 14 wa mstari wa mbele katika Mapinduzi ya Zanzibar, yakiratibiwa na Katibu Mipango wa ASP hayati Abdallah Said Natepe.
Uteuzi na kupendekezwa majina ya vijana 100 kutoka Zanzibar ambao waliungana na wenzao wa Tanganyika ulifanywa na Halmashauri Kuu ya ASP Youth League, wiki moja kabla ya siku ya Muungano walichezeshwa gwaride la Muungano, nyakati za asubihi na jioni wakiongozwa na Bi Mwakemwa.
Vijana kutoka Zanzibar waliondoka kwa kutumia usafiri wa meli hadi Dar es Salaam, wakapokewa na wenzao kwa furaha, hata hivyo wakati huo hakufahamu kama atapangwa kuwa mmoja kati ya vijana watakaobeba udongo kutoka Zanzibar.
Walipofika na meli yao kutia nanga, wakateremka na kupanda magari yaliyowapeleka kwenye maeneo waliopangiwa kuishi na kufanya mazoezi, kabla ya siku ya tukio hilo kufika.
Hapo ndipo tulipoteuliwa na kuanza kufanya mazoezi ya vitendo katika eneo la uchanganyaji udongo huku wenzao wengine wakicheza gwaride la halaiki ya Muungano. Muda wote walikuwa wenye furaha na wakati mwingi kabla na baada ya kuamka walikuwa wakiimba nyimbo za kulisifia taifa jipya.
Baada ya kumalizika tukio la uchanganyaji udongo kulifanyika karamu na dhifa kubwa ikulu, viongozi wote wa Tanganyika na Zanzibar walihudhuria kabla ya Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano kurudi Zanzibar, kupokewa kwa maandamano makubwa huko Maisara Suleiman, Unguja na Tibirinzi kisiwani Pemba.
Je, Muungano ulipata baraka za wananchi wa Zanzibar?
Hassan anasema hilo halikuwa ni jambo la siri. Kwa miaka mingi ASP iliweka dhamira ya wananchi wa Zanzibar kuungana na wenzao wa Tanganyika huku mara kadhaa wananchi wakiulizwa hadharani wakiuunga mkono mpango huo.
Mzee Karume katika mikutano mingi ya ASP aliyoifanya Zanzibar na Pemba alisikika akiwauliza wananchi “...Je, wananchi mko tayari kwa union na Tanganyika,…wananchi walimjibu bila ya kubabaika …tuko tayari kwa masilahi ya Afrika yote, Mapinduzi na usalama wa nchi zetu,” anasema Hassan.