Sugu apigilia mstari kauli ‘maendeleo hayana vyama’

Rais John Magufuli akisalimiana na Mbunge wa Mbeya Mjini (chadema).Rais yupo mkoani Mbeya kwa ziara ya kiserikali.Picha ya Maktaba.

Muktasari:

Sugu aliendelea kumweleza Rais Magufuli na baadhi ya wananchi wa Mbeya na viongozi na wanachama wa CCM wanamweleza habari ambazo si kweli, kwamba wapinzani wanapinga kila kitu kinachofanywa na Rais Magufuli na Serikali yake.

Kuna kauli maarufu ambayo Watanzania wameanza kuizoea ya Rais John Magufuli kwamba “maendeleo hayana chama”. Ni kauli ambayo amekuwa akiirudia karibu kila mahala anakwenda.

Hata katika ziara yake mkoani Mbeya aliyoianza Aprili 26, Rais Magufuli pia amekuwa akirejea, akimaanisha kuwa Watanzania wote wanatakiwa kushiriki shughuli za maendeleo bila kubaguana kwa itikadi za kisiasa.

Katika ziara hiyo ya kwanza mkoani humo tangu achaguliwe kushika wadhifa huo, Rais alitua katika Jiji la Mbeya lenye jimbo la Mbeya Majini ambalo mbunge wake ni Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu kupitia Chadema.

Akiwa jijini humo alifanya mkutano wa hadhara katika viwanja vya Rwandanzovwe ambapo viongozi mbalimbali wa kiserikali na kisiasa walipata fursa ya kuzungumza mbele ya Rais Magufuli.

Miongoni mwa wanasiasa waliopata fursa hiyo ni Mbunge Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ambaye alitumia takriban dakika tisa kueleza mambo mbalimbali ya kijamii, kisiasa na hata kiuchumi yanayowasibu wapiga kura wake.

Katika hotuba hiyo iliyokuwa ikikatizwa na sauti zilizomtaka amalize, Sugu alimweleza Rais Magufuli kwamba ingawa wananchi wa Jiji la Mbeya kumpenda (Rais Magufuli), lakini kuna mgawanyiko mkubwa wa kisiasa ndani ya jiji hilo.

Alisema watu wa Mbeya bila kujali vyama vyao wanamuunga mkono Rais Magufuli, hata yeye (Sugu) ni miongoni mwa watu wanaomuunga mkono Rais na ataendelea kumuunga mkono ingawa hana mpango wa kukihama chama chake na kujiunga na chama anachokiongoza Rais Magufuli.

Pengine hapa Sugu alikuwa anatuma ujumbe kuhusu wabunge na madiwani wa Chadema na baadhi ya vyama vya upinzani ambao wamekuwa wanahama vyama vyao wakieleza sababu ya kumuunga mkono Rais Magufuli.

Ujumbe wa wanasiasa hao umekuwa ukizua utata, kwamba wanahama chama kuunga mkono anayesema maendeleo hayana chama. Wakosoaji wamekuwa wakisema wanasiasa hao wangeweza kushiriki shughuli mbalimbali za kuleta maendeleo bila kuhama vyama vyao, kama anavyoeleza Sugu

Sugu aliendelea kumweleza Rais Magufuli na baadhi ya wananchi wa Mbeya na viongozi na wanachama wa CCM wanamweleza habari ambazo si kweli, kwamba wapinzani wanapinga kila kitu kinachofanywa na Rais Magufuli na Serikali yake.

Badala yake, Sugu alisema wapinzani wanamuunga mkono Rais kwa mambo mengi, japokuwa wanakosoa mengine machache, lakini mazuri wanayomuunga mkono hayasemwi.

Kwa mujibu wa Sugu watu wanaopeleka taarifa wana tabia ya kumfikishia Rais za mambo ambayo wapinzani hawaridhiki nayo, lakini kwa yale ambayo wanamuunga mkono Rais hawamwelezi.

Sugu alisema kwenda mbali zaidi akisema hata kama yapo mambo wanayomuunga mkono Rais na Serikali yake, wapinzani pia wanayo haki ya kikatiba ya kutoa mawazo yao mbadala hata kama hayafanani ya fikra za Rais.

Baada ya maelezo hayo, ndipo Sugu akatoa fursa adhimu kwamba yuko tayari kujitolea kufanya maridhiano ya kisiasa jijini Mbeya ili kuondoa ‘mafundo fundo’ ya kisiasa kwa wakazi wa Mbeya na ikiwezekana hata kitaifa.

Mgawanyiko mkutanoni

Kabla ya kutoa ombi hilo, Sugu alisema hata pale mkutanoni kulikuwa na mgawanyiko mkubwa wa kisiasa kufikia hatua ya kubaguana, hali iliyoashiria siasa za Jiji la Mbeya zilivyo.

Alitoa mfano kwamba licha ya wanachama na viongozi wa vyama vya upinzani kujitokeza kwa wingi kufika uwanjani hapo kumsikiliza Rais Magufuli, wanachama hao walibaguliwa na kuachwa wakae mbali, huku wanachama wa CCM wakipewa viti vya mbele.

“Mheshimiwa Rais, hata hapa ukiangalia tulivyokaa, utaona kabisa kuna mgawanyiko mkubwa miongoni mwetu wanasiasa wa Mbeya. Watu wote wa Chadema wapo hapa lakini wapo kule nyuma, naomba hebu wana Chadema nyosheni mikono huko mliko (watu walinyoosha mikono huku wakimshangilia Sugu)... watu hao wamekuja kukusikiliza na walitamani na wao kuja huku mbele lakini wamebanwa,” alisema Sugu na kuongeza….

“Na wewe Mheshimiwa Rais unasema hutaki vyama na badala yake unataka umoja na mshikamano wa kitaifa. Mimi nimekushika, nakufuata na mimi ni miongoni mwa watu wanaokuunga mkono bila kuhama chama. Nitaendelea kukuunga mkono mpaka mwisho nikiwa ndani ya chama changu,” alisisitiza Sugu..

Sugu alimsihi Rais Magufuli akatae kuambiwa maneno kwamba watu wa Mbeya hawampendi, na kwamba wanapanga kumfanyia fujo kwani hakuna mtu mwenye akili timamu anapanga njama za kumfanyia fujo Rais.

Alisema ‘Mr. President (Rais) wasikuambie mambo haya eti matusi, mara eti hatukupendi, si kweli. Walikuwa wanasema watu wa Mbeya…. Na jana Mwenyekiti wangu wa Chadema alikamatwa kwa sababu eti alikuwa anapanga wafanye fujo mbele ya Rais, hicho kitu hakiwezekani watu na akili zao hawezi kupanga kumfanyia fujo Rais’.

Akizungumza na maelfu ya wananchi waliojitokeza kumsikiliza, Rais Magufuli aliwahakikishia wakazi wa Jiji hilo kuwa anawapenda na kuwataka wafanye kazi ili wajiletee maendeleo yao na taifa kwa ujumla.

Pengine kauli hizo za Sugu zinaweza kufungua ukurasa mpya wa mahusiano ya kisiasa katika maeneo mengine nchini ili kuiishi kauli ya Rais ya “maendeleo hayana vyama.”