UCHOKOZI WA EDO: Zitto ajibiwe ili mechi isiishe kwa sare

Zitto Kabwe anasumbua kwelikweli. Sijui kwa nini. Dunia ikienda mashariki, yeye anajaribu kwenda magharibi. Wakati mwingine rafiki zangu wa Kigoma ndivyo walivyo. Wabishi, wanatuvuruga sana.

Majuzi nilisoma utetezi wa Serikali kuhusu fedha inayoitwa Dola kupanda. Aliyeongea alitoa hoja nzuri. Alituambia kwamba huu sio msimu wa utalii. Dola nyingi haziingizwi nchini na wale wazungu wanaokuja kushangaa simba na ndugu zake na kupanda milima.

Hoja nyingine ikawa wazi kwamba hatukuuza korosho zetu nje, hilo ni kweli halina mjadala. Kuna sehemu tumejiumiza ama kwa makusudi au kwa bahati mbaya, lakini ukweli ni kwamba tumejiumiza. Kuna siku Namba Moja atakuja kutupa mrejesho kuhusu kilichoendelea. Huwa namkubali kwa kuwa mwanadamu mkweli.

Baada ya kauli zile niliamua kujiridhisha kama aliyetoa hoja alikuwa amesema kweli. Wakati mwingine mwanadamu inabidi uishi kwa kujifariji tu kwamba watu wenye kazi zao wanazifanya kwa usahihi na wanajua wanachokisema.

Ghafla akaibuka Zitto kutoka kusikojulikana. Simu zake zikirudishwa kutoka Polisi anakuwa msumbufu sana. Akaandika mitandaoni sababu ndefu kwa nini dola imepanda. Akajazia sababu zake nyingi. Akaingiza uchaguzi wa Zanzibar. Kupigwa risasi Tundu Lissu, akaweka na hiyo ya korosho. Akajaza sababu nyingi kweli. Wakati mwingine anachomekea na kile kiingereza chake cha hapa na pale.

Kufikia hapo, Zitto akawa amenivuruga kwelikweli. Nikajiuliza, nimsikilize yeye au yule aliyezungumza awali? Nikagundua kwamba yule wa awali inabidi aongee tena na akanushe hoja za Zitto kwa akili. Nikimaanisha atutengenezee mrejesho unaoonyesha kwamba hao wafadhili wanaotupa fedha hawajaacha kufanya hivyo kwa sababu ya risasi za Tundu Lissu.

Akirudi na majibu hayo sisi tulioishia darasa la saba huku maskani, tutaelewa na tutaacha kumsikiliza Zitto. Hapo mechi itakuwa 2-1. Kwa sasa mechi inakuwa sare na mijadala kama hii mizito ya kupanda kwa dola nchini mwetu inahitaji majibu ya uhakika.

Shilingi yetu ikishuka kwa kasi hii tunaweza kwenda dukani kwa Mangi kununua mkate huku tukiwa tumebeba noti zetu katika mfuko wa rambo. Si kitu kizuri. Mechi hii isiishe sare kirahisi. Nataka kuamini kwamba labda Zitto hajasema kweli.