Wanahabari watoa maazimio 10 kuhusu Azory Gwanda

Dodoma. Mashirika 11 yanayounda Umoja wa Haki ya Kupata Habari (CoRi) na wanahabari wanaohudhuria maadhimisho ya siku ya uhuru wa vyombo vya habari duniani, wametoa maazimio 10 kuhusu kutekwa kwa mwandishi wa habari kujitegemea wa Mwananchi Communications Ltd (MCL), Azory Gwanda.

Akisoma maazimio hayo yatakayosainiwa na waandishi wote wa habari na wadau wa habari nchini, Katibu Mtendaji wa Baraza la habari Tanzania(MCT), Kajubi Mukajanga alisema baada ya kusainiwa, yatapelekwa kwa mawaziri wa Mambo ya Ndani, Habari na Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora.

Miongoni mwa makubaliano hayo ambayo hadi jana yalikuwa yamesainiwa na wanahabari na wadau 140 ni kutaka waziri wa Mambo ya Ndani, atamke rasmi kupotea kwa Azory ili hatua za umakini zianze kuchukuliwa.

Mukajanga alisema azimio hilo pia linataka utaratibu wa utekelezaji wa majukumu ya polisi namba 232 ambao unaelezea hatua za kuchukuliwa mtu anapopotea ufuatwe na Serikali itenge rasilimali za kutamfuta Azory, “tunataka Jeshi la Polisi litoe taarifa za mara kwa mara za uchunguzi wa Azory ikiwezekana kila baada ya mwezi au wiki.”

Alisema pia imekubaliwa kuwa wahariri wa vyombo vya habari, wachapishe habari za Azory kama mtu aliyepotea.

Alisema Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imeombwa ifanyie kazi suala la kupotea kwa Azory na kwamba wameazimia kumuomba mkuu wa jamii wa mabalozi nchini awe tayari kutoa msaada wowote ambao serikali itaomba katika kumtafuta Gwanda. Azimio jingine linataka vyombo vya habari, kuchapisha mitaani, kwenye luninga na sehemu mbalimbali kuwa Azory amepotea na yeyote atakayemuona au kujua alipo atoe taarifa.

Umoja huo pia imeazimia kila mwisho wa mwezi vyombo vya habari kutoa taarifa juu ya kupotea kwake na kutengenezwa wimbo maalum wa kumtafuta.

Soma

CoRi inaundwa na MCT, UTPC, Sikika, THRDC, Tamwa, Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Twaweza East Africa, Policy Forum, Misa-Tan, Jukwaa la Wahariri (TEF), Jamii Forum na TLS