VIDEO: Wabunge wataka mfumo wa elimu ufumuliwe

Dodoma. Wabunge jana waliweka kando itikadi zao za kisiasa na kusimama pamoja kuichambua sekta ya elimu wakisema mfumo wake unahitaji kufumuliwa ili uwe na tija kwa mustakabali wa kizazi kijacho.

Hayo yalijitokeza katika mjadala wa bajeti ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ya mwaka 2019/20.

Hoja hizo za wabunge, zinafanana na zilizowahi kutolewa mara mbili kwa nyakati tofauti na Rais mstaafu, Benjamin Mkapa aliyesema kuna janga katika elimu nchini na kushauri kuitishwa kwa mdahalo wa wazi, utakaoshirikisha makundi yote ya jamii kwa ajili ya kujadili suala hilo.

Machi 18, mwaka jana katika hafla kumuaga Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Profesa Idris Kikula, Mkapa alisema, “ninaamini kabisa kwamba tuna crisis (janga) ninasoma katika magazeti, ninaletewa presentation (mawasilisho) kutoka sekta binafsi, walimu, private university (vyuo vikuu binafsi). Napata pia minong’ono kutoka kwa vyuo vya umma kwamba kuna (crisis) katika elimu.”

Alisema wapo watu wanaolalamika juu ya lugha, ratiba, ushirikiano, lakini pia juu ya ushirikishwaji wa wahitimu, wanaofanya kazi na wazazi ili kuamua Taifa linakwendaje katika elimu siku zijazo.

“Kwa nini ukisoma katika orodha ya shule zetu za sekondari kwenye ufaulu wao katika 10 za kwanza ukiangalia unaweza kuwa na uhakika kuwa nane si za Serikali ni za watu binafsi? Kama Serikali ndio mhimili mkuu wa elimu, kuna kasoro gani?” alihoji Mkapa

Katika mjadala wa elimu, karibu kila mbunge aliyesimama kuchangia kwa siku mbili tangu juzi aligusia changamoto inayoikabili sekta hiyo.

Mbunge wa Serengeti (CCM), Chacha Marwa alisema sheria ya elimu ni ya muda mrefu na hivyo imezeeka na kuchakaa, “Ukiangalia sheria iliyoanzisha sekta ya elimu tunalingana nayo umri, mimi sasa ni mzee mfumo wa elimu ambao hauwezi kujibu matatizo ya nchihuo umezeeka umechakaa ni lazima uangaliwe upya,” alisema Marwa.

Marwa aliungwa mkono na Sixtus Mapunda (Mbinga Mjini- CCM) aliyesema mfumo wa elimu nchini unapaswa kumwezesha mtu anapohitimu aweze kuishi.

“Unakuwa na injinia hawezi hata kutengeneza barabara, unakuwa na daktari badala ya kupasua mguu anapasua kichwa… tunatengeneza watu ambao hawajaelimika. Kuna mambo mawili lazima uangalie ndio yatakayotusaidia. Jambo la kwanza sera yetu ya elimu ya mwaka 2014 ina changamoto,” alisema.

Mapunda alisema haitekelezeki kwa sababu stadi haijafanyika vizuri na changamoto nyingine zinatengenezwa kwa nyaraka na miongozo.

Alitoa mfano waraka namba 5 wa mwaka 2011 ambao unasema kwa mwaka, mwanafunzi atahudhuria siku 194 lakini kama kutakuwa na mtoro hatafukuzwa shule hadi siku 90 mfululizo.

“Waraka unatengeneza mazingira ya mwanafunzi kuwa mtoro. Kwa sababu hatahudhuria siku 30 atakuja siku mbili, hatahudhuria tena siku 30 atakuja siku tatu,” alisema.

Mapunda ambaye kauli yake ilizungumzwa pia na Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Suzan Lyimo alisema waraka huo unasababisha uzembe shuleni na kuiomba Serikali kuufuta.

Lyimo ambaye ni waziri kivuli wa elimu alisema viwango vya ufaulu kwa mwanafunzi anayetakiwa kwenda kidato cha tatu anatakiwa kuwa na ufaulu wa masomo mawili katika daraja D katika mitihani ya kidato cha nne.

Alisema hiyo inaonyesha kutengeneza ufaulu mdogo tangu awali kwa sababu haitegemewi mtu mwenye D mbili afanye vizuri katika mitihani ya kumalizia shule.

Mbunge wa Kahama Mjini (CCM), Jumanne Kishimba alisema changamoto ya ukosefu wa ajira nchini inafanya fedha wanazowekeza wazazi katika elimu ya juu kufanana na mchezo wa upatu.

Alisema tatizo la ajira nchini ni kubwa kuliko hata la Katiba Mpya na kutaka iundwe tume kuchunguza mfumo wake kama alivyoshauri Rais mstaafu Mkapa.

Alisema hivi karibuni, zilitangazwa ajira katika Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) wakaenda watu 40, 000 kwenye usaili wakati waliohitajika ni 70 tu na kueleza kwamba suala hilo ni la kukatisha tamaa vyuo vinavyozalisha wanafunzi hao.

Alisema mtu anauza mifugo yake na kwenda kusomesha lakini wanapomaliza wanaachwa wakazunguke mtaani na shahada walizopata, “...hali ni mbaya sana mitaani watu wana shahada kila kona.”