Tanzania yaingiza wasanii 16 tuzo za Afrimma, ‘Inama’ ya Diamond yatajwa kwenye vipengele sita

Muktasari:

Wimbo ‘Inama’ wa Diamond Platnumz umetajwa katika vipengele sita katika tuzo za Afrimma zinazotarajiwa kufanyika Novemba, 2019 nchini Marekani.

Dar es Salaam. Wimbo ‘Inama’ wa Diamond Platnumz umetajwa katika vipengele sita katika tuzo za Afrimma zinazotarajiwa kufanyika Novemba, 2019 nchini Marekani.

Katika wimbo huo Diamond amemshirikisha  mwanamuziki kutoka  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC),  Fally Ipupa.

Vipengele alivyotajwa kuwania tuzo kupitia wimbo huo ni msanii bora wa mwaka, msanii anayeburudisha , msanii bora wa Afrika Mashariki, wimbo bora wa kushirikishwa, wimbo bora wa mwaka na video bora ya mwaka.

Tanzania pekee ukimtoa Diamond imeingiza wasanii 15 katika tuzo hizo, wakiwamo wawili kutoka Lebo ya Wasafi inayoongozwa na Diamond ambao ni Harmonize na Rayvanny.

Wasanii wengine ni Ali Kiba, Jux, Ommy Dimpoz ambao pamoja na Rayvanny na Harmonize wameingia katika kipengele cha msanii bora wa kiume Afrika Mashariki.

 Vanessa Mdee na Nandy wameingia kwenye kipengele cha msanii bora wa kike Afrika Mashariki.

Pia yupo mwongozaji wa muziki Kenny, watayarishaji wa muziki Kimambo na S2Kizzy, Bujini ambaye ni  mcheza shoo wa Diamond, DJ Ommy kwa upande wa maDJ na mtangazaji wa redio Times,  Lil Ommy.

Pia Aika na Nahreel wameingia katika kundi bora kupitia kundi lao la Navykenzo wakichuana na Saut Sol wa nchini Kenya.