Sintofahamu yatanda matibabu bure kwa wajawazito, wazee

Muktasari:

  • Sera ya Afya ya mwaka 2007 inataka huduma za Afya kwa wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupata huduma bure, lakini kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya makundi hayo, baadhi kutokana na kutozwa fedha za matibabu, wengine kwa kutofahamu mchakato unaowezesha kupata huduma hiyo.

Dar/mikoani. Ni majira ya saa 6:45 mchana, kijana mmoja amejiinamia katika mojawapo ya baraza za Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).

Kwa karibu dakika 55 amejikunja akionekana mwenye mawazo, mithili ya mtu mwenye tatizo kubwa asiye na suluhisho.

Ni taswira ambayo unaweza kuiona kwa watu kadhaa hospitalini hapa, ambako kuna idadi kubwa ya wagonjwa wanaoingia na kutoka, achilia mbali wanaokuja kutembelea ndugu zao waliolazwa kama kijana huyu anayejitambulisha kuwa ni Khalfan Idd (24).

“Ninafanya kazi ya kuuza maji barabarani. Mtaji wangu haufiki hata Sh50,000 nitatoa wapi Sh700,000?” anasema wakati nilipomuhoji sababu za kujiinamia kwa muda mrefu.

“Sina ndugu kusema atanisaidia. Sielewi nifanye nini na leo ni siku ya nne tangu (mke wangu) ameruhusiwa ila hawezi kuondoka mpaka deni lilipwe. Anavyozidi kukaa, pia bili inaongezeka.”

Mkewe Khalfan alilazwa hospitalini hapo kwa ajili ya kujifungua na gharama za matibabu zimefikia Sh700,000 baada ya kujifungua watoto pacha na kulazwa hospitalini hapo kwa muda mrefu.

Sera ya Afya ya mwaka 2007 inataka huduma za Afya kwa wazee, wajawazito na watoto wenye umri chini ya miaka mitano kupata huduma bure, lakini kumekuwepo na malalamiko kutoka kwa baadhi ya makundi hayo, baadhi kutokana na kutozwa fedha za matibabu, wengine kwa kutofahamu mchakato unaowezesha kupata huduma hiyo.

Khalfan ni mmoja wa kati ya watu wengi waliokumbana na kadhia hiyo ambao hawajui kama wanatakiwa kulipia huduma waliyopata Muhimbili.

Mkazi mwingine wa Dar es Salaam, Naomi Msigwa anasema mgonjwa wake alipelekwa Muhimbili kwa rufaa kutoka Amana, lakini sasa anatakiwa kulipia gharama za matibabu.

“Kwa kweli huduma zao ni nzuri sana na tumezifurahia mno. Tatizo aliporuhusiwa tumeletewa bili ya malipo ya Sh246,000 kwa kweli tulishangaa,” alisema.

“Hatuna uwezo. Tulichokifanya ni kujichangisha kama tunavyochangisha harusi, ndiyo leo tumelipia.”

Na si hao wawili pekee. Mama aliyejitambulisha kwa jina la Asha, ambaye alikuwa amelazwa na mtoto wake wakati mwandishi akifuatilia habari hii, pia alikumbana na hali hiyo.

“Hakuna cha bure. Watoto wetu wakilazwa hapa tunaambiwa lazima kulipia kitanda. Hivyo mtoto atatibiwa lakini unajua mwisho wa siku bili ya kitanda na mengineyo utaletewa,” alisema Asha.

Hali hiyo pia iko katika hospitali nyingine za jijini Dar es Salaam na mikoani, ambako baadhi wanakiri kuwa kuna mpango mzuri wa kushughulikia wazee baada ya kupatiwa vitambulisho.

Lakini, mkuu wa kitengo cha mawasiliano kwa umma Muhimbili, Aminiel Aligaesha alisema wanaolipishwa ni wale ambao hawakufuata utaratibu.

“Tunapokea wagonjwa ambao hawajafika Muhimbili kwa rufaa. Hawa lazima walipie au kuchangia huduma,” alisema.

“Wapo ambao wana bima za afya sasa usilipie huduma kwa sababu umeambiwa ni bure? Lazima utachangia ili kusaidia ile asilimia 60 ambayo tunawapa msamaha.”

kauli kama hiyo aliitoa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu aliyesema pamoja na sera ya matibabu ya mama wajawazito, wazee na watoto chini ya miaka mitano ni bure, lazima kufuata taratibu.

“Kwa Muhimbili, kama mwanamke amejipeleka anatakiwa alipie. Lakini kama amefika huko kwa rufaa akitokea Mwananyamala, Temeke na kwingineko basi anatakiwa kutibiwa bure,” alisema Ummy Mwalimu.

Hali hiyo haina tofauti na mkoani Arusha ambako makundi hayo yameanza kupatiwa huduma bure baada ya kukamilika kwa uhakiki.

Wakiwa katika Hospitali ya Kaloleni, St Elizabeth na baadhi ya vituo vya afya, baadhi ya wazee walisema wanapata huduma hiyo bure.

“Ingawa naona sio magonjwa yote, ila haya madogo madogo ya uzee kama homa na malaria tunapimwa na tunapewa dawa bure,” alisema Ramahani Isihaka ambaye ni mkazi wa Kaloleni.