Serikali ya Tanzania yasema haikupata shinikizo ili kubadili sheria ya takwimu

Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa(NBS), Dk Albina Chuwa 

Muktasari:

Serikali ya Tanzania imesema haikupata shinikizo lolote kutoka kwa wabia wa maendeleo kwa ajili ya kufanya marekebisho ya vifungu vya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2018, kama ilivyoelezwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe 

Dar es Salaam. Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu ya Taifa(NBS), Dk Albina Chuwa amesema Serikali ya Tanzania haikupata shinikizo lolote kutoka kwa wabia wa maendeleo kwa ajili ya kufanya marekebisho ya vifungu vya Sheria ya Takwimu ya mwaka 2018.

Siku chache zilizopita, Bunge la Tanzania lilipitisha marekebisho ya Sheria ya Takwimu kwa mwaka 2019, ikiwa ni mwaka mmoja baada ya kuanza utekelezaji wa Sheria ya Takwimu ya mwaka 2018, iliyolalamikiwa kuwa na baadhi ya vifungu hatari kwa maendeleo ya kazi za tafiti nchini.

Kabla ya Bunge la Tanzania kupitisha mabadiliko hayo, Kiongozi wa chama cha upinzani Tanzania cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, akilalamikia Serikali ya Tanzania kupuuza maoni ya wadau wa ndani na kukubali shinikizo la wabia wa maendeleo waliotishia kuinyima Serikali mkopo wa miradi ya elimu hadi itakapoondoa vikwazo vya uandaaji wa takwimu mbadala.

Leo Jumanne Julai 2, 2019, Dk Chuwa akizungumza katika mkutano wa kuijadili namna gani Tanzania inaweza kutumia takwimu za asasi zisizokuwa za kiserikali kabla ya kuanza utekelezaji wa mabadiliko ya sheria hiyo amesema Hii ni nchi na ina utawala wake.

“Tumefanya mabadiliko ya kisheria kwa sababu sheria yoyote ikitungwa, ikafanya kazi lazima iwe na upungufu, mfano kifungu cha (6) kinachoeleza majukumu ya NBS, kilizuia kuratibu takwimu za asasi zisizokuwa za kiserikali, sasa tuna pengo la takwimu, tunakwendaje kuziba pengo hilo,” amesema  

Mkutano huo wa NBS, umewakutanisha wadau wa asasi zisizokuwa za kiserikali, Benki ya Dunia, wabia wa maendeleo (DFID), viongozi wa taasisi za takwimu za serikali kutoka nchi za Ghana na Burundi pamoja na kamisheni ya Umoja wa Mataifa inayosimamia takwimu, lengo ni kupata uzoefu na mwelekeo wa kuandaa mwongozo wa uandaaji wa tafiti Tanzania.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Hakielimu, John Kalage amesema Sheria ya mwaka 2018, ilifunga mikono  wadau katika utoaji wa tafiti, ikiwamo Hakielimu iliyokuwa imewasilisha taarifa nne za utafiti kwa ajili ya kupata kibali tangu Februari mwaka 2019 lakini haikuwa imekubaliwa.

“Lakini mabadiliko haya yanaturuhusu sasa kuendelea na kazi ya ukusanyaji wa takwimu zitakazokuwa na mchango mkubwa wa kuziba mwanya unaohitajika. Kwa mfano ni asilimia 40 tu ya tafiti zilizokidhi mahitaji katika utekelezaji wa malengo ya SDGs,” amesema Kalege.

Kalage amesema baadhi ya vifungu kandamizi katika sheria iliyofanyiwa marekebisho ni pamoja na kukosa ruhusa ya kukosoa takwimu za serikali pamoja na kuwapo kwa vipingamizi vya uzalishaji na usambazaji wa takwimu bila kibali cha NBS, ambaye anaweza kukubali au kukataa kutoa kibali hicho.